Dk. Didas Masaburi Akubali Yaishe....AFUTA Kesi Ya Kupinga Ubunge Wa Saed Kubenea

Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi ameamua kutoendelea na kesi ya kupinga ushindi wa Saed Kubenea wa Chadema kwenye uchaguzi wa Jimbo la Ubungo aliyokuwa amefungua Mahakama Kuu.

Masaburi, aliyegombea kiti hicho kwa tiketi ya CCM, alifungua kesi hiyo Namba 8 ya mwaka 2015, akidai kuwa Kubenea alitoa rushwa, katika maeneo mbalimbali, huku pia akimlalamikia msimamizi wa uchaguzi kuwa hakumtendea haki.

Jana, mahakama ilitarajia kusikiliza maombi la Masaburi la kutaka nafuu ya gharama za dhamana ya usikilizwaji wa kesi, lakini wakili wake, Clement Kihoko aliwasilisha maombi ya kutaka nafuu ya gharama pamoja na kesi ya msingi.

Wakili Kihoko aliomba kuondoa mahakamani kesi hiyo kwa kutumia kifungu cha 30 (1) cha Kanuni za Uchaguzi Mkuu za Mwaka 2010.

Mawakili wa upande wa walalamikiwa, Nyaronyo Kichere na Frederick Chihwelo walidai kuwa hawana pingamizi na maombi hayo ya nafuu ya gharama, lakini wakaomba walipwe fidia kwenye kesi ya msingi.

Wakili Kihoko alipinga madai hayo ya fidia akisema hadi wanafikia uamuzi wa kuondoa mahakamani maombi na kesi hiyo, upande wa wadaiwa ulikuwa haujawasilisha nyaraka zozote mahakamani ambazo zilipaswa kuwa zimewasilishwa kuhusiana na kesi hiyo, hivyo hawana cha kudai.

Hata hivyo, Wakili Kicheere alidai kuwa licha ya kwamba walikuwa hawajawasilisha nyaraka zozote mahakamani, wamekuwa wakifanya vikao ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti kuhusu kesi hiyo na hivyo kuingia gharama kama za nauli za kuendea mahakamani.

Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu fidia hiyo, Jaji Lugano Mwandambo alikubaliana na maombi ya upande wa wadaiwa, kuwa wanastahili kulipwa fidia na akaamua Masaburi alipe fidia ya asilimia 50 ya gharama walizotumia.

Alisisitiza kwamba hata kama wadaiwa walikuwa hawajawasilisha mahakamani nyaraka zilizokuwa zinahitajika katika kesi hiyo hadi jana, muda wa kuwasilisha nyaraka hizo ulikuwa haujaisha kwa hiyo ni lazima kuna kazi waliyokuwa wameshaifanya.

Kwa uamuzi huo, upande wa walalamikiwa utalazimika kuwasilisha maombi hayo ya fidia pamoja na mchanganuo wa gharama walizozitumia.

Masaburi hakupatikana kueleza sababu za kufuta kesi hiyo na wakili wake alisema alipokea maekezo hayo kutoka kwa mteja wake, lakini hakuambiwa sababu.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Vituko avitaisha hapa duniani,Masaburi tumekula sanaaaaaa hela yake ili tumchaguwe awe mbunge,Leo anabadili kibao,Mwili Tu unaonyesha wewe ni fisadi.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad