Edwin Mtei: Rais Magufuli asiige kila kitu kutoka kwa Nyerere

Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aanze kasi ya kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu aina ya
ufanyaji kazi wake.

Rais Magufuli alianza kasi hiyo kwa kuzitembelea idara mbalimbali za Serikali zikiwamo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia ameshafika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kushuhudia namna huduma zinavyotolewa. Wananchi wameonekana kufurahishwa na kasi hiyo.

Kitendo cha kufuta sherehe za uhuru zinazofanyika kila Desemba 9 kila mwaka na kasha kuagiza mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa ajili ya sherehe hizi yaelekezwe katika mahitaji muhimu, kimewagusa Watanzania kiasi kwamba baadhi yao wameufananisha uongozi wa Dk Magufuli na ule wa Rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere.

Miongoni mwa watu walioguswa na hatua za Rais Magufuli ni aliyewahi kuwa gavana wa kwanza wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na mwasisi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mtei anasema anamatumaini makubwa na kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Swali: Unamtazamaje Rais Magufuli?
Jibu: Ni mtu mwenye shauku na maendeleo, ni mzuri kama atasimamia na kuishi maneno yake. Ni mtu ambaye atasimamia maendeleo yetu na ninaamini atasimamia ukuaji wa uchumi wetu. Pamoja na kuridhishwa na kasi ya Rais Magufuli, naamini kwamba kwa sehemu kubwa anatekeleza sera na ilani ya Chadema. Kile anachofanya kwa sasa kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwenye ilani na sera zetu na tutashirikiana naye katika kuisadia hii nchi yetu.

Swali: Je, ungepata nafasi ya kumshauri Rais Magufuli ungemwambia nini.
Jibu: (anavuta pumzi) Kwanza ningempongeza kwa kupata ushindi katika hali ngumu sana, lakini ningemshauri maliasili za taifa hili zitumike kwa ajili ya Watanzania wote na wananchi washirikishwe katika kuendeleza nchi yao. Ningemwambia ahakikishe Watanzania wanashirikishwa katika umiliki wa ardhi na kuwekeza. Wao ndiyo wawe wahusika wakuu katika kusimamia rasilimali zao na siyo vinginevyo hata wageni wakiingia nchini wawe kama wabia tu. Nashauri kwamba wageni wanaotaka kuwekeza katika sekta ya madini, wauze hisa zao kwa Serikali ambayo itakuwa ikimiliki hisa nyingi zaidi. Kwa kufanya hivyo, maliasili za Taifa zitatumiwa na wazawa wenyewe. Ningemshauri Rais Magufuli ahakikishe Watanzania wananufaika na rasiliamali zao ambazo walipewa na Mwenyezi Mungu kwa kusudi la kuwakomboa na umaskini.

Swali: Unadhani Rais Magufuli anairejesha Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere?
Jibu: Kwanza unajua mimi napinga siku zote Azimio la Arusha kwa kuwa naamini liliturejesha katika umaskini, hivyo nisingependa Rais Magufuli airejeshe nchi yetu katika enzi za Mwalimu Nyerere. Rais Magufuli anaweza kuchukua mambo machache kutoka kwa Mwalimu Nyerere ikiwamo ufufuaji wa viwanda vilivyokufa. Ningependa airejeshe Tanzania kwa watu wake kufaidi matunda ya rasilimali zao kama wananchi wawe na ajira, mashamba na uchumi wa kuwatajirisha wote na siyo watu wachache.

Swali: Je, ni nini unaona kimebadilika tangu enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa.
Jibu: Mambo mengi yamebadilika sana kama uchumi umepaa na watu wanafaidika kupitia uchumi huo, lakini tatizo lililopo hapa ni kwamba wanaofaidi ni wachache kuliko wale wengi ambao ni maskini wa kutupwa. Tanzania haina mfumo wa kuwabana matajiri kuhakikisha wanawasaidia maskini kuinua uchumi wao ili nchi ipige hatua kwenye maendeleo, lazima iweke mfumo huo.

Swali: Je una maoni gani kuhusu baraza jipya la mawaziri?
Jibu: (Anatabasamu) Kwanza hili siyo baraza dogo hata kidogo, laiti kama angekuwa na mawaziri 18 hadi 24 hapo tungesema baraza ni dogo. Hili nililiona wakati nikiwa gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na mshauri wa Rais katika masuala ya uchumi, Mwalimu Nyerere alikuwa na baraza dogo.
Naamini Rais Magufuli kabla ya kuteua baraza hilo alizingatia watu waadilifu na wenye uzoefu na siyo walafi. Rais Magufuli analenga kuleta mabadiliko nchini kwa lengo la kuwafanya Watanzania wafaidi matunda ya rasilimali zao kama gesi, mafuta na madini, basi baraza hilo halina budi kuendana na kasi yake.

Mawaziri hawana namna ni lazima waendane na kasi yake au waondoke. Ni lazima hili baraza lihakikishe linafanya kama aliyewateua anavyotaka kuwatumikia Watanzania wote.

Chanzo: Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad