Hatma ya Sakata la Dk. Mwaka Kujulikana Leo au Kesho

Hatma ya mtabibu anayemiliki kituo cha afya cha tiba mbadala cha Foreplan Clinic kilichopo Ilala, jijini Dar es Salaam, Dk. Mwaka Juma, itajulikana leo au kesho baada ya serikali kukagua uhalali wa nyaraka zake, ikiwamo cheti cha taaluma ya utabibu.

Hatua ya serikali kumkagua daktari huyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hamis Kigwangalla, kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho cha afya Desemba 14, mwaka huu na kutomkuta Dk. Mwaka na baadhi ya wafanyakazi wanaohusika na utoaji wa tiba.

Hali hiyo ilimshtua Dk. Kigwangalla baada ya kukuta msururu wa wagonjwa wakisubiri kuhudumiwa huku watoa huduma wakiwa hawapo kituoni hapo, ndipo alipotoa agizo la kuchunguzwa kwa kituo hicho na Dk. Mwaka mwenyewe.

Dk. Kigwangalla pia alitoa amri ya kufungwa kwa muda kwa kituo hicho mpaka uchunguzi wa kina utakapokamilika ili kuona kama huduma zinazotolewa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.

Akizungumza na Nipashe jana, Dk. Kigwangalla alisema serikali imeshapokea vyeti vya daktari huyo na kuvikagua kama anastahili kutoa huduma hiyo ya tiba asilia ama la.

Alisema alikabidhiwa ripoti ya Dk. Mwaka Ijumaa iliyopita inayoelezea taaluma yake na kwamba atakapomaliza kuipitia atatoa tamko kuhusiana na hatma ya Dk.Mwaka kupitia mkutano na vyombo vya habari. 

“Suala hilo nitalitolea tamko kesho (leo) au keshokutwa, itategemeana na ratiba yangu… kwa kuwa ripoti niliipokea Ijumaa lakini sikuimaliza kuisoma kutokana na majukumu mengine ya kikazi,” alisema.

Kuhusiana na masuala ya tiba asilia kwa ujumla, Dk. Kigwangalla alisema serikali haizuii bali inawaachia wananchi wenyewe waamue kama zinawasaidia au la.

Alisema masuala ya tiba ya asilia ni imani ya mtu mwenyewe, hivyo jukumu la serikali ni kuhakikisha kunakuwapo na usalama wa tiba hizo na sheria na taratibu zilizopo zinazingatiwa.

Alisema watoaji wa tiba asilia wengi hawafuati mashariti ya utoaji wa dawa hizo na baadhi hukiuka miiko ya utoaji tiba.

Nipashe ilimtafuta Dk. Mwaka jana ili kupata maoni yake kuhusiana na uchunguzi wa nyaraka zake lakini simu yake ya mkononi ilipokewa na mtu mwingine aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake,  ambaye hata hivyo hakutaka kuzungumzia suala hilo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad