Kasi ya Rais Magufuli Haiko Kwenye Makontena Bandarini tu, imepita na TFF Ambapo TRA Imesitisha Safari Ya Timu Ya Taifa Ya Vijana

Ikiwa bado siku moja Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli atimize mwezi mmoja toka aapishwe kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeshuhudia mengi yakitokea katika suala zima la upambanaji na watu wanaokwepa kodi sambamba na kusimamishwa kazi kwa viongozi kadhaa wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) waliopo Bandarini.

December 4 kasi ya Rais John Pombe Magufuli inaonekana kuwashitua viongozi wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), kwani wameanza harakati za kuwaadhibu watu wanaodaiwa kodi.

Juma lililopita Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliaga timu ya Taifa ya Vijana Chini ya umri wa miaka 15 (U15) ikianza ziara yake ya Afrika Mashariki kuanza kucheza na Burundi mjini Kigoma na baadaye Kigali, Rwanda, Kampala, Uganda na mwisho Nairobi Kenya.

Bahati mbaya ziara hiyo itaishia Mwanza na Kigoma kufuatia Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA) kuizuia account ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kwa kushindwa kulipa kodi ya Tsh bilioni  1,637,334,000 (bilioni 1.6 tshs) ikiwa ni kodi kwa kipindi cha 2010 – 2013

Sehemu kubwa ya kodi hiyo ni makato kwenye mishahara (PAYE) ya walimu wa kigeni, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen na vilevile kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazili uliofanyika mwaka 2010.

Walimu wa Timu za Taifa wamekuwa wakilipiwa mishahara na Serikali na hivyo TFF haikuwajibika kuwakata kodi. Aidha, mchezo kati ya Tanzania na Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya Serikali na fedha zake hazikuingizwa katika akaunti za TFF.

Kutokana na hatua hii ya TRA shughuli nyingine za mpira zitakazohathirika  ni:

1. Kulipia madeni ya usafiri, chakula na posho za Timu za Taifa zilizoshiriki mtoano wa kombe la Dunia na mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Challenge Cup)

2. Program za mpira wa Wanawake na vijana zitalazimika kusimama.

3. Mashindano ya kombe la Shirikisho raundi ya pili iko kwenye hatihati kwani hakuna fedha za kugharimia michezo hiyo.

4. Mashindano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoendelea yatalazimika kusimama vilevile. Mashindano haya TFF imekuwa ikiyaendesha bila mdhamini.

5. Vifaa vya michezo (Mipira) kwa ajili ya shule za msingi na vituo vya maendeleo (Regional Football Development Centres) vinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote na TFF haitakuwa na uwezo wa kulipia usafirishaji na ushuru wake.

6. Malipo ya gharama za kambi na karo kwa ajili ya vijana wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 13 walioko shule ya Alliance Academy ya jijini Mwanza.

7. Huduma za kiutawala ikiwa ni pamoja na utunzaji viwanja na majengo, maji, umeme, ulinzi pamoja na mishahara na stahiki nyingine za wafanyakazi

8. Mwelekeo na mwitikio mzuri wa wadhamini uko kwenye hatari ya kupotea pindi mashindano na shughuli wanazozidhamini zitakapofubaa au kusimama kabisa.

9. Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) wa Mwaka 2015 uliopangwa kufanyika Tanga 19-20 Desemba 2015 sasa una hatihati ya kuweza kufanyika.

Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ulipaji kodi na wajibu wa Mamlaka ya Mapato katika kuhakikisha kodi inakusanywa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa,TFF ipo katika mawasiliano na TRA katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwa ni pamoja na kupitia upya mahesabu ili kujua wajibu halisi (net liability) wa TFF na namna ya kulipa au kulipwa kutegemea ulali wa mahesabu.

Kwa taarifa hii TFF inaomba utulivu kwa wanamichezo wote pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka katika vyombo vyote husika ikiwemo TRA na wadau wengine ili jambo hili lipate ufumbuzi wa kudumu utakaoleta tija kwa serikali ya awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla wake.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad