Katibu Mkuu Tamisemi Akagua Miundombinu ya Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka

WATOA huduma katika kipindi cha mpito cha mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, kampuni ya UDA-RT wameihakikishia serikali na wananchi kuwa matayarisho yanaendelea vizuri tayari kwa huduma hiyo kuanza Januari 10 mwakani.


Ahadi hii ilitolewa wakati wa ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alipokuwa akikagua miundombinu katika mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma hiyo.


Siku chache zilizopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wahusika wote wa mradi huo kuhakikisha unaanza mara moja ili kupunguza adha ya usafiri Dar es Salaam.

“Tulitaka kujiridhisha kama mabasi haya yako tayari kutoa huduma hii,” alisema Sagini mbele ya waandishi wa habari na kuwataka wahusika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa haraka.

Mabasi 140 yanayomilikiwa na kampuni ya UDA-RT yatatumia mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa ukusanyaji nauli, mifumo ya utoaji taarifa na maeneo maalum ya wazee na walemavu. 

Mwenyekiti wa UDA-RT, Robert Kisena aliwataka wananchi kujali mabasi hayo mara huduma itakapoanza.

“Wananchi wajali mabasi haya, madereva nao wana wajibu wa kuhakikisha magari haya yanadumu,” alisisitiza.

Alisema kuhujumu mabasi hayo mapya au miundombinu ya mradi huo ni sawa na wananchi kujihujumu wenyewe, kwani huduma hiyo ni kwa ajili yao. 

Alisema tayari kazi ya kufunga vifaa vinavyotakiwa katika mabasi hayo imeshakamilika kwa baadhi ya mabasi na inaendelea kwa mengine.

Msemaji wa UDA-RT, Said Mabruk alisema magari yote yanayotakiwa kuanza kwa huduma hiyo ya mpito yana madereva na walishapewa mafunzo na kwamba ni matumaini yao kuwa huduma itaanza kwa wakati uliopangwa.

Awamu ya kwanza inahusisha kilometa 20.9 za njia maalumu kutoka Kimara hadi Kivukoni, barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo- Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi njia panda eneo la Morocco.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad