Licha ya Kuinyima Tanzania Dola Milioni 472....Spidi ya Rais John Magufuli Yatinga Kwa Obama

Licha ya Serikali ya Marekani kuinyima Tanzania Dola za Marekani milioni 472 (Sh.bilioni999.4) kutokana na kushindwa kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, lakini imekunwa na kasi ya Rais John Magufuli katika kupambana vita dhidi ya ubadhilifu na rushwa.

Bodi ya MCC iliyokaa kikao chake Desemba 16, mwaka huu, iliamua kutopigia kura mkataba unaopendekezwa kati ya MCC na Tanzania kutokana na kutofurahishwa na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na kukamatwa chini ya kivuli cha Sheria ya Matumizi ya Mtandao kwa wanaharakati kadhaa Oktoba mwaka huu.

Uchapakazi wa Rais Magufuli kwa kipindi kifupi alichoingia madarakani tangu Novemba 5, mwaka huu mara baada ya kuapishwa, umekuwa gumzo kubwa katika baadhi ya nchi barani Afrika na Ulaya kutokana na kasi yake ya utendaji na kuwaacha viongozi wa nchi hizo kwenye wakati mgumu.

Mojawapo ya marais ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi wake kutokana na kasi ya Rais Magufuli ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata. Kenya ambayo imekuwa ikifuatilia siasa za Tanzania tangu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, imeonyesha kupenda mbinu za Rais Magufuli na wananchi wake wanatamani mtu kama yeye.

Nchi nyingine ni Afrika Kusini, Gazeti la The Sunday Independent linalochapishwa nchini humo, liliwahi kuandika katika tahariri yake hivi karibuni ikiwa na kichwa cha habari kisemacho, “Afrika ifuate mfano wa Tanzania.”

Pia sehemu ya tahariri hiyo ilidokeza kuwa Afrika inahitaji Rais kama Magufuli ambaye ameonyesha kwa dhati nidhamu katika matumizi ya serikali. Vilevile nchi za Ghana, China nazo zimesifu uchapakazi wa Rais Dk. Magufuli.

Marekani kupitia Balozi wake nchini, Mark Childress, imeonyesha kufurahishwa na utendaji wa Rais Magufuli katika nyanja hiyo ya utumbuaji majipu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Balozi Childress alieleza kuwa Marekani kupitia Shirika lake na MCC imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli za kuimarisha vita dhidi ya ubadhilifu na  rushwa.

“MCC imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli za kuimarisha vita dhidi ya ubadhirifu na rushwa. MCC inatumaini kuwa jitihada hizo zitaendelea na kuleta mabadiliko ya kimfumo,” alisema.

Balozi huyo alieleza kuwa MCC inatumaini kuwa jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli kwa sasa zitaendelea na kuleta mabadiliko ya kimfumo.

Rais Magufuli, Novemba 6, mwaka huu, siku moja mara baada ya kuapishwa, alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha (Hazina) kwa kutembea kwa miguu na kutowakuta wafanyakazi wa wizara hiyo ofisini kitendo kilichomkera.

Mbali na kufanya ziara katika wizara hiyo, Rais Magufuli Novemba 9, mwaka huu alifanya ziara ya kushtukiza katika  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako baada ya kushuhudia uozo mwingi alichukua hatua ya kufuta bodi ya wakurugenzi ya hospitali hiyo na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi wake, Dk. Hussein Kidanto.

Rais Magufuli pia Novemba 7, mwaka huu alitangaza kufuta safari za nje za watumishi wa serikali hadi pale atakapotangaza utaratibu mpya.

Alichukua uamuzi wa kufuta safari hizo kutokana na kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha kwa watumishi wa serikali walioko katika wizara, taasisi na idara za serikali ambao wamekuwa wakijipangia safari bila ya utaratibu maalum.

Baada ya kufanya uamuzi huo, Rais Magufuli alieleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.

Siku chache baada ya kutoa agizo hilo,  Rais Magufuli alifyeka msafara wa watumishi wa serikali 50 na kubakia wanne waliokuwa waende katika mkutano wa Jumuiya ya Madola na kuokoa takribani Sh. milioni 700 ambazo zinadaiwa zingetumika kwa watumishi hao katika safari hiyo.

Vilevile, Rais Magufuli Novemba 23, mwaka huu alifuta sherehe za Uhuru na badala yake akaamuru Desemba 9 itakuwa siku ya kufanya usafi nchi nzima ili kuondokana na tatizo la kipindupindu linaoikabili nchi.

Uamuzi wake huo uliokoa zaidi ya Sh. bilioni nne ambazo zilkuwa zitumike katika sherehe hizo na kuelekeza zitumike kupanua barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam kipande cha kutoka Morocco kwenda Mwenge.

Mbali na kufuta sherehe hizo, Rais Magufuli pia alipiga marufuku uchapishaji wa kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama ya fedha za umma na kuagiza kila wizara ijigharamie fedha zake katika kufanya shughuli hizo.

Pia Novemba 20, mwaka huu Rais Magufuli aliagiza zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za uzinduzi wa Bunge la 11 zitumike kununua vitanda vya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Rais Dk. John Magufuli Novemba 27, mwaka huu alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza bandarini na kubaini upotevu wa makontena 349 ambayo yalitoroshwa bandarini hapo bila ya kulipiwa kodi na kusababisha serikali kukosa mapato ya Sh. bilioni 80.

Mbali na kumsimaisha Kamishna huyo, Desemba 16, mwaka huu, Rais Magufuli alimwondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah kwa kile alichoeleza kuwa kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.


CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mara kwa mara mna mchezo/tabia ya kurudiarudia sentensi/maneno yale yale ili sijui stori ionekane ndefu hii inaboa kinoma kwa msomaji jaribuni kubadilika kuhusu hilo

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad