Viongozi wa makanisa mbalimbali nchini, wametoa salamu za Sikukuu ya Krismasi jana, wakielezea kufurahishwa na kasi ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli.
Wamesisitiza waumini wao, kumuombea Rais na kuwataka wananchi kutii mamlaka, kwa kuwa yamewekwa na Mungu.
Viongozi hao pia, wamewataka watendaji wa Serikali na wananchi walioshiriki ukwepaji kodi, watubu dhambi zao na kurejesha vyote walivyochukua, ambavyo si halali yao.
Pia, wamempa moyo Rais Magufuli kuendelea kutumbua majipu, kwani hata Bibilia inatambua kazi hiyo.
Mbali na ujumbe huo wa viongozi wa dini kwa waumini wao na kwa Watanzania kwa ujumla, Rais Magufuli mwenyewe alishiriki katika ibada ya sikukuu hiyo katika Kanisa la Mtakatifu Petro, jijini Dar es Salaam, ambapo aliwatakia Watanzania wote Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya na kusisitiza waendelee kumuombea yeye na viongozi wengine.
Baada ya kuwatakia sikukuu njema Watanzania, Rais Magufuli aliwakumbusha wananchi kwamba ustawi wa nchi, unatokana na watu kufanya kazi, hivyo baada ya shamrashamra za msimu wa sikukuu, warejee kufanya kazi kwa bidii kwa ujenzi wa Taifa.
Dodoma wamuombea
Mkoani Dodoma katika shamrashamra hizo, Askofu Amos Kinyunyu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, aliwataka Watanzania kuzidi kumuombea Rais Magufuli kutokana na utendaji kazi unaowagusa Watanzania wa hali ya chini.
Alisema wao kama Kanisa, wataendelea kumuombea ili afanye kazi anayoendelea kufanya sasa hivi, kwani hata vitabu vitakatifu, vinataka usawa katika uchumi na kipato kwa kila mtu.
‘’Tunawaomba Watanzania wazidi kumuombea Rais wetu kasi aliyonayo aendelee kuwa nayo, kwani Mungu anapenda haki katika maisha pamoja na uchumi ulio sawa.
‘’Wakati mwingine hii kauli ya Hapa Kazi Tu, inakuwa hata sisi inatuogopesha, lakini Mungu ataendelea kumlinda na kumwongoza,’’ alisema.
Ni jibu la Kanisa
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God la Miyuji Dodoma, Samson Mkuyi alisema utawala wa Rais Magufuli, unaonekana ni jibu la Watanzania wengi pamoja na Kanisa.
Mchungaji Mkuyi alisema wamefurahishwa na utendaji kazi wake hasa upande wa maadili, ikizingatiwa kuwa Kanisa linataka maadili ya kiroho na kimwili.
‘’Tulianza kuomba haya miaka mitano, sisi Kanisa tunamwambia asiogope kwani Mungu yupo pamoja na yeye, tunaendelea kumuombea ili Mungu aendelee kumpa ulinzi,’’ alisema.
Atumbue zaidi
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani alisema; ”Rais ameonekana kutumbua majipu yaliyokuwa yamejificha na katika hili tutaendelea kumuombea ili ayatumbue zaidi, pia na kuwafanya watendaji wafanye kazi kwa usahihi,’’ alisema.
Rais amepatikana
Kanisa la KKKT Dayosisi ya Morogoro mbali na kurejea umuhimu wa kumuombea Dk Magufuli, liliwataka viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, wajitoe kikamilifu kuwatumikia na kuwahudumia wananchi wakiweka mbele maslahi ya taifa.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Paulo ole Mameo, wakati wa mahubiri yake alitaka vyama vyote vya siasa, kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kusema mwito wa Kanisa ni sasa tusonge mbele, uchaguzi umemalizika na Rais amepatikana.
“ Rais wetu ameanza kazi yake vizuri na sasa tumuunge mkono , tushirikiane kwa misingi ya umoja, upendo na amani katika kujenga Taifa na tuliombee lisonge mbele.
“Wale viongozi waliozoea kutenda uovu sasa waache, wasijiingize tena huko, tunataka wawe mfano mzuri katika kuonesha uadilifu wao kwa kusimamia huduma bora mbele ya jamii,” alisema Askofu Mameo.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude, yeye alisisitiza waumini kuhubiri upendo na kudumisha amani iliyopo.
Alipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa hatua zake za kuwajali watu wanyonge, ili wapate huduma bora za kijamii ikiwa ni pamoja na kusimamia nidhamu, uadilifu na utendaji unaozingatia sheria za nchi.
Wakwepa kodi watubu
Katika Kanisa la KKKT Usharika wa Maili Moja Kibaha, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Isai Ntele, aliwataka watu waliokuwa wakijihusisha na ukwepaji kodi hapa nchini, kutubu mbele za Mungu na kurejesha kile walichokwepa na kuonesha utii kwa mamlaka iliyopo madarakani, kwani imewekwa na Mungu.
Mchungaji Ntele alisema Mungu alisikiliza kilio cha Watanzania kwa kuwapa kiongozi ambaye ana uchungu na wananchi wake, kwani ameonesha dhahiri kuwa hataki haki za wanyonge, zipotee kwa kudhulumiwa na wachache.
“Hata Biblia inasema kila mtu aitii mamlaka iliyo Kuu kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na ile iliyopo nimeaminiwa na Mungu, hivyo asiye na mamlaka asipotii, anashindana na agizo la Mungu hivyo watapata hukumu,” alisema.
Wanatufananisha na mbinguni
Mkoani Shinyanga, Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, alisisitiza umuhimu wa kumwombea Rais Magufuli aliyeonesha nia ya kuwatumikia wananchi bila upendeleo, ambaye ameonesha wazi wazi kuwa anamtanguliza Mwenyezi Mungu.
"Kuna baadhi ya watu wanataka kutusadikisha kuwa Tanzania hakuna amani kwa nia zao wenyewe, labda wakilinganisha Tanzania na mbinguni ni sawa, kwa sababu mbinguni kuna utimilifu wake wote, lakini ukilinganisha Tanzania na mataifa mengine, ndugu zangu tuna amani ambayo tunapaswa kuilinda kwa nguvu zetu zote.
“Wapo wengi wangetamani tuchinjane hapa nchini, wana wivu na chuki na nchi yetu na pengine wanaweza hata kutumia viongozi mbalimbali kupenyeza mambo yao, ili tuchukiane sisi kwa sisi, tuwakemee watu wanaodharau hii amani iliyopo,” alisema Askofu Sangu.
Alisema Tanzania hata bomu likilipuka, watu wanakimbia kwenda kutazama, lakini kwa nchi zenye machafuko, likilipuka bomu hakuna anayekwenda pale kwa kuhofia kifo na hiyo ni dalili tosha kuwa kuna amani.
Askofu Sangu aliwataka Watanzania kusherehekea sikukuu kwa upendo hususani katika ngazi ya familia na kuhamasisha watu kuishi kwa kupendana na kuepuka vitendo vya kupeana ujumbe wa kujengeana chuki, kwani ndiyo chanzo cha vurugu katika jamii na taifa kwa ujumla.
Dar na mabadiliko ya kweli
Mkoani Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alisema mabadiliko ya kweli yanaletwa na watu ambao wako tayari kufanya kazi kwa dhati usiku na mchana na si matajiri.
Akitoa mahubiri yake kwa waumini wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph lililoko Posta jijini Dar es Salaam, katika Ibada ya usiku wa Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, alisema katika fikra za mabadiliko, watu wa kawaida waliaminishwa kwamba hawana mchango wanaoweza kuutoa katika mabadiliko.
“Mara nyingi sisi watu wa kawaida tulisadikishwa kwamba hakuna mchango tunaoweza kuutoa ili kuleta mabadiliko katika jumuia yetu, tulisadikishwa kwamba watu wanaokuwa na fedha na mali nyingi hao ndio wanaoweza kuleta mabadiliko katika jumuiya yetu,” alisema Pengo.
Alisema sasa mawazo hayo yamekwishatambuliwa kuwa hayakuwa sahihi, kwani watu wenye mali si wanaoweza kuleta mabadiliko yanayotakiwa katika jumuiya ya watu.
“Watakaoleta mabadiliko ni wale ambao haidhuru nafasi yao ni ipi katika jumuiya, lakini wako tayari kufanya kazi usiku na mchana, ili kuhakikisha kwamba hali ya kibinadamu inakuwa nzuri zaidi na huo ndio ujumbe unaopaswa kupokelewa kutoka kwa malaika aliowaendea wachungaji na kuwaambia msiogope,” alisema Pengo.
Askofu Pengo alisema na kupitia ujumbe huo wa malaika, Tanzania inaambiwa usiogope, kwani unayo habari njema, ambayo ni kuwa tayari kufanya kila linalokuwa ndani ya uwezo wake ili hiyo habari njema iifikie.
Aliwataka Watanzania wamuombe Mungu awajaalie neema ya kutambua kila mmoja anaweza kuwa chimbuko la habari njema na mabadiliko, si tu katika mazingira ya imani ya kidini, lakini katika mazingira hata ya kiuchumi na kisiasa.
Alisema watu hawapaswi kuogopa, bali kulinda makundi yao wakisubiri habari njema na habari hiyo si kwa ajili ya matajiri wanaoishi katika majumba ya kifahari, bali kwa ajili ya wote, habari ambayo ni ya furaha ambayo ni chimbuko la heri kwa wanadamu wote.
“Habari hii siyo kwa ajili ya matajiri, siyo kwa ajili ya wale wanaoishi katika majumba ya kifalme ni habari ya furaha ambayo itakuwa chimbuko la furaha na heri kwa wanadamu wote, Mwenyezi Mungu atujaaliye hilo katika Taifa letu,” alisema Pengo.
Magufuli asisitiza kazi
Wakati viongozi wa dini wakihamasisha Watanzania kumuombea, Rais Magufuli mwenyewe alihudhuria ibada ya Sikukuu ya Krismasi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro, lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika ibada hiyo, alipewa nafasi ya kutoa salamu, ambapo aliwatakiwa Watanzania wote sikukuu njema ya Krismasi na Mwaka Mpya na kuwataka washerehekee kwa amani wakikumbuka kufanya kazi baada ya shamrashamra za sikukuu.
Rais Magufuli alisema watu wakumbuke kwamba ustawi wa nchi unatokana na watu kufanya kazi ndio maana anasimamia kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu.
“Tunaposherehekea sikukuu hizi, tukumbuke ya kwamba baada ya shamrashamra ni kufanya kazi kwa bidii kwa ujenzi wa Taifa letu,” alisema Rais Magufuli.
Magufuli Awakuna Viongozi Wa Dini.....Maaskofu Wahimiza Aombewe Ili Aendelee Kutumbua Majipu
1
December 26, 2015
Tags
Long live JPJM
ReplyDelete