Amri hiyo imekuja baada ya mpangishaji wa IMTU ambaye ni Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) kupeleka notisi kupitia kwa kampuni ya mnada ya Fosters Auctioneers & General Traders, ya kuondoka katika ploti namba 2348 iliyopo Mbezi Beach jijini hapa.
Jerome Msemwa, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uwakili ya Msemwa & Advocates inayoiwakilisha NDC, alisema jana kuwa IMTU ilisainiana mkataba wa upangishaji na shirika hilo kwa Sh100 kwa mwaka kuanzia mwaka 1996 kwa miaka 15 hadi Agosti, 2011 na tangu hapo chuo hicho hakikulipa kodi yoyote kwa mpangishaji wake.
“Hadi sasa NDC inadai jumla ya Sh3.06 bilioni kama deni la kodi ya kuanzia Agosti, 2011 hadi Septemba, 2015 kwa kodi ya Sh73 milioni kwa mwezi,” alisema Msemwa akieleza kuwa nakala za notisi hiyo imesambazwa katika taasisi mbalimbali zikiwemo Ikulu na vyombo vya habari.
Agizo hilo ni pigo jingine kwa uongozi wa IMTU ambao utalazimika kutafuta eneo mbadala kuendeleza masomo kwa wanafunzi wa chuo hicho, ambao tangu Julai mwaka jana wamejikuta wakisoma katika mazingira magumu.
Itakumbukwa kuwa Serikali iliwahi kuifungia hospitali ya chuo hicho Julai, 2015 kutokana na kutotimiza masharti na taratibu za uendeshaji.
Sakata hilo ilikuwa ni sehemu ya mfululizo wa balaa zilizokuwa zikiikumba IMTU, baada ya viungo vya binadamu ambavyo hutumika kufundishia madaktari kukutwa vimetupwa eneo la katika msitu uliopo Bunju wakati huo.
Notisi hiyo ilisema kuwa IMTU tangu Septemba 2012 ilikuwa ikipeleka mashauri mahakamani ya kupinga kuondolewa katika eneo hilo, lakini Septemba 2014 Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotoa amri ya mpangaji huyo kuondoka, ambaye hata hivyo hakutekeleza.
“Unatakiwa kuondoka katika eneo hilo linalomilikiwa na NDC na kulipa madeni yote haraka iwezekanavyo.
“Zingatia kuwa ukishindwa kuhama ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya notisi hii, tumepatiwa maagizo ya kukuondoa kwa nguvu bila taarifa yoyote na kushikilia mali zako zote ili kuweza kulipia madeni hayo,” ilisomeka notisi hiyo.
Mkurugenzi wa hospitali ya IMTU, Profesa Yassin Mgonda alisema hajapata notisi hiyo na kueleza kuwa huenda imeufikia uongozi wa juu hasa mmliki na mwenyekiti wa chuo hicho, Katuri Subbarao.
“Siwezi kusema nimejiandaeje kuondolewa wakati sina taarifa yoyote na mtu aliyeachiwa madaraka yupo likizo. Ila nafahamu kuwa kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa masuala ya kulipana na mambo yalikuwa hayajakaa vizuri,” alisema Profesa Mgonda.