Mtu mmoja anayetuhumiwa kuuza tiketi za ulanguzi kwenye Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT), jana alitumia kinyesi cha binadamu kujilinda dhidi ya polisi waliokuwa wakitaka kumkamata baada ya kubaini alikuwa akifanya biashara hiyo haramu.
Pamoja na kutumia mbinu hiyo ya kipekee, mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Nuhu Matumla (26), alikamatwa na askari hao ambao jana waliweka kambi UBT ambako ulanguzi wa tiketi za mabasi yaendayo mikoani umepamba moto wakati huu wa kuelekea siku kuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Tukio hilo lililovuta hisia za watu na kusababisha msongamano wa magari, lilitokea saa 1.30 asubuhi nje ya kituo hicho wakati wa operesheni hiyo ya kukamata walanguzi wa tiketi na matapeli.
Askari wapatao wanne waliokuwa na silaha walikuwa wakimfukuza Matumla na walipomkaribia, alivua suruali yake iliyokuwa na kinyesi na kisha na kukichota kwa mkono na kuwarushia.
Wakati akirusha alikuwa akisema “niachieni, nitawapaka kinyesi”, lakini juhudi zake hazikufua dafu.
“Kamata huyo hakuna kumwachia, unarusha kinyesi unafikiri sisi tunaogopa,” alisema mmoja wa askari hao.
Kinyesi alichokuwa akirusha kilichafua sare za askari hao na magari madogo yaliyokuwa yameegeshwa katika eneo hilo.
Wananchi walioshuhudia tukio hilo tangu asubuhi, walidai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na zaidi ya tiketi 20 ambazo alianza kuziuza kwa watu waliokuwa wakitaka kusafiri.
“Sisi tulikuwa tumekaa hapa tukamuona huyo jamaa (Matumla) akiuza tiketi, hatukujua kama ni za ulanguzi. Baada ya muda tukaona askari wanakuja wakamkamata.” alisema Hassan Issa.
Juma Idd, aliyekuwapo eneo la tukio, aliwamwagia sifa askari kwa kumkamata.
“Tunawasifu hawa askari. kitendo cha kumkamata huyu jamaa aliyekuwa akiwarushia kinyesi ni cha kishujaa,” alisema.
“Kwanza kinyesi chenyewe kilikuwa kinatoa harufu kali ambacho kwa mtu wa kawaida huwezi hata kumsogelea.”
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mohamed Mpinga alisema mpaka sasa watu wawili wamekamatwa kwa kuuza tiketi za ulanguzi huku wengine 20 wakikamatwa kwa makosa ya kutapeli na kusumbua abiria.
“Tumefanikiwa katika hilo japo ulanguzi wa tiketi unafanyika kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Alisema wote waliokamatwa watafikishwa mahakamani na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.