Polisi Sita Mbaroni kwa Tuhuma za Mauaji ya Washukiwa Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia askari polisi sita, wawili wakiwa askari wa kawaida na wanne wa Idara ya Wanyamapori kwa tuhuma za kusababisha vifo vya watu wawili wanaodaiwa kujihusisha na ujangili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,  Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliwataja askari hao wa kawaida kuwa ni Bonny Mbange ambaye ni mkaguzi wa polisi E.909D/SGT na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Filbert.

Kwa upande wa Askari wa Wanyamapori aliwataja kuwa ni Emmanuel Mbaga, Deogratias Mwageni, Joseph Jimmy na Asubile Mwakyusa.

Kamishna Kova aliwataja watuhumiwa waliofariki kuwa ni Yasin Rashidi (46) na Samson Michael (46) mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam.

Aidha, Kamishna Kova alisema awali waliwakamata askari saba walioshiriki katika mauaji hayo, lakini wakati wanahojiwa mmoja kati yao aitwaye Issa Kazimoto mwenye namba F.5371D/C alifanikiwa kutoroka.

Alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa askari hao na wenzao wa Idara ya Wanyamapori kutoka kikosi maalum cha kuzuia ujangili walikuwa wanafuatilia watu wawili kwa tuhuma za ujangili.

Alisema Desemba 9, mwaka huu, zilitolewa taarifa Kituo cha Polisi Magomeni kutoka kwa askari waliokuwa katika operesheni maeneo ya Sinza kuwa watuhumiwa waliokuwa wanawafuatilia wamefariki dunia katika harakati za kuwakamata.

Alisema uchunguzi wa awali wa tukio hilo unaonyesha kuna utata tangu wakati wa ukamatwaji hadi vifo vya marehemu hao wawili na ndiyo sababu askari hao  wanashikiliwa ili kupata ukweli wa vifo hivyo na uhalali wa nguvu iliyotumika.

Aliongeza kuwa ukaguzi wa miili ya marehemu hao unaonyesha kuwa walipata majeraha ya risasi, hivyo uchunguzi wa kisayansi utafanyika ikiwa ni pamoja na kuwahusisha  madaktari bingwa wa uchunguzi wa miili.

Aidha, Kamishna Kova aliwataka wananchi wenye taarifa zaidi kuhusu tukio hilo walisaidie Jeshi la Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad