Profesa Muhongo Aiagiza Tanesco ishushe Bei ya Umeme

Bei ya umeme inatarajia kushuka wakati wowote kuanzia sasa baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuliagiza Shirika la Umeme (Tanesco), kushusha gharama za nishati hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amefuta likizo za wafanyakazi wa shirika hilo ili washughulikie tatizo la umeme nchini huku akisisitiza kuwa hataki kusikia kukatika katika kwa umeme.

Profesa Muhongo alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta Gas Plant, ambapo alikwenda kwa ajili ya kukagua mitambo hiyo ili kuona kama yote inafanyakazi.

Akitoa maelezo ya mtambo huo, Meneja Mohamed Kisiwa alisema wana mitambo mitano na wana uwezo wa kuzalisha Megawati 42 kila saa.

Alisema gharama ya uzalishaji umeme kwa uniti moja ni Sh. 90 na wamekuwa wakiuza kwa Sh. 180 hadi 187.

Profesa Muhungo alisema kwa maelezo ya meneja huyo, inaonyesha umeme wanaozalisha wanapata faida mara mbili hivyo alisema kuna uwezekano mkubwa wa kushusha gharama za umeme.

Aliagiza maofisa wa wizara yake na wa shirika la Tanesco wakutane leo ili wajue umeme huo utashushwa kwa kiwango gani.

?Utauzaje umeme mara mbili ya gharama za uzalishaji, tunataka kuwapunguzia wananchi bei ya umeme na kwenye mkutano wetu wa kesho (leo) tutajadili kupunguza bei ya umeme..haya mahesabu hayajakaa sawa maana unazalisha uniti moja kwa Sh. 90 na kuuza kwa Sh. 180 tutajadiliana mpunguze,? alisema.

CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad