Rais Kagame Awapa Mbinu Viongozi wa Burundi Kutafuta Suluhu

Rais wa Rwanda Paul Kagame amewashauri raia wa Burundi kumaliza mgogoro unaoendelea nchini humo kwani hakuna mtu wa nje anayeweza kufanya hivyo.

Rais Kagame alisema kuwa, viongozi na nchi hiyo na raia hao wana wajibu wa kushughulika na mambo yao ya ndani kuliko kutegemea msaada wa watu wengine.

“Siyo kweli kwamba Rwanda inafurahia mgogoro wa kisiasa unaoendelea Burundi kwani athari zake zinatugusa hata huku. Wakimbizi wanazidi kuongezeka hivyo ni vyema wakatafuta ufumbuzi haraka iwezekanavyo kuyanusuru maisha ya watu,” alisema.

Kiongozi huyo alikanusha uvumi kwamba nchi yake imekuwa ikisaidia baadhi ya makundi ya wapiganaji yanayopingana na Serikali ya Burundi.

“Hayo ni madai ya yasiyo ya kweli na kama kuna mwenye ushahidi kuhusu hilo athibitishe. Huu siyo wakati wa lawama kwani jambo la muhimu ni suluhu itakayomaliza mgogoro huo,” alisema.



Amuunga mkono Museveni

Katika hatua nyingine, Kagame alionyesha kumuunga mkono Rais wa Uganda Yoweri Museveni anayewania madarakani kwa muhula wa tano.

“Ukiniuliza mtazamo wangu kuhusu Uganda jibu ni kwamba nimefanya kazi vizuri na viongozi waliopo madarakani hivyo nawatakia kila la heri kwenye uchaguzi ujao,” alisema na kuongeza kuwa:

“Naamini waganda ni watu wenye akili timamu na uelewa wa kutosha utakaowawezesha kufanya uchaguzi sahihi bila kuleta machafuko katika nchi yao.”

Kuhusu uamuzi ambao mataifa ya magharibi yanaweza kuchukua kutokana na kufanyika mabadiliko Katiba ya Rwanda, Kagame alisema Warwanda hawawezi kuishi kwa kufuata matakwa ya watu wengine.

“Wanyarwanda wataishi wanavyotaka. Hatuwezi kuwa waoga na watiifu kupita kiasi kwa vile tunategemea misaada kutoka kwa wahisani, binafsi sidhani kama kuna matatizo makubwa yanayoweza kutokea na yakawa zaidi ya yaliyowahi kutukuta,” alisema.


Uamuzi wa bunge

Juzi, Bunge la Burundi lilipinga mpango wa Umoja wa Afrika wa kutaka kutuma kikosi cha kusimamia amani katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa.

Spika wa Bunge hilo, Pascal Nyabenda alisema hakuna dharura ya kutuma kikosi cha umoja huo nchini humo.

Kwa upande wake, Spika wa Baraza la Seneti la Burundi, Reverien Ndikuriyo alisisitiza kuhusu tofauti baina ya mauaji na mauaji ya kimbari.

Wabunge na wawakilishi wa baraza hilo wakiwa katika kikao chao, walikubaliana kwamba Serikali ifanye kila iwezalo kukomesha mauaji yanayohatarisha amani nchini humo.

Ijumaa iliyopita Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika llilipitisha uamuzi wa kupeleka kikosi cha askari 5,000 nchini humo.

Kabla ya hatua hiyo ya Bunge na Baraza la Seneti, Msemaji wa ofisi ya Rais alikuwa ametoa radiamali yake kuhusiana na uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kutaka kutuma kikosi cha kusimamia amani Burundi na kutangaza kuwa, endapo AU itatuma kikosi hicho na kupuuza upinzani wa Serikali kwa hatua hiyo, vikosi hivyo vitahesabiwa kuwa ni majeshi vamizi.

Viongozi wa Serikali wanadai kuwa vitendo vya utumiaji mabavu vya vikosi vya usalama vinafanyika katika fremu ya kurejesha amani na usalama, wapinzani wanasema kuwa, hatua hizo ni za ulipizaji kisasi dhidi yao na lengo lake ni kuwauwa wapinzani wa serikali.

Katika hali ambayo, weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanatahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea vita vya ndani na kuanza mauaji mengine ya kimbari Burundi, Umoja wa Afrika umetangaza kuwa hautaruhusu kuanza vita na kutokea mauaji mengine ya kimbari barani humo.

Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kiyonga ambaye nchi yake ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa Burundi alitangaza hivi karibuni kwamba, njia bora kabisa katika mazingira ya hivi sasa na hali ya usalama inazidi kudorora nchini humo ni kuanza mazungumzo kwa minajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Kiyonga alisema, viongozi wana mambo 10 ambayo wanataka yatiwe katika ajenda ya mazungumzo ya tarehe 28 Desemba.

Miongoni mwa mambo hayo ni utawala wa awamu ya tatu ya uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza, jedwali la uchaguzi, hali ya usalama pamoja na serikali ya umoja wa kitaifa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha, zaidi ya watu 240 wameuawa na zaidi ya 200,000 wakilazimika kuyakimbia makazi yao, kutokana na machafuko hayo tangu Aprili mwaka huu.

Machafuko hayo yalitokea baada ya chama tawala CNDD-FDD kumwidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo.

Wapinzani Burundi walisema, hatua ya Nkurunziza kugombea kiti cha urais katika uchaguzi uliopita ilikuwa kinyume na katiba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad