Utata kuhusiana na uhalali wa tiba zinazotolewa na Dk. Juma Mwaka wa kituo cha tiba mbadala cha Foreplan Clinic kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam unaelekea kuwa ‘pasua kichwa’ kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangalla, baada ya majibu ya uchunguzi wa vyeti vya mganga huyo kushindwa kutolewa kwa umma kama ilivyoahidiwa.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Waziri Kigwangalla aliahidi kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na Dk. Mwaka juzi (Jumatatu). Alieleza hayo baada ya kufanya ziara ya ghafla kwenye kituo cha Dk. Mwaka Desemba 14, 2015 na kutomkuta yeye na baadhi ya watoa huduma wake kabla ya kumtaka (Dk. Mwaka) awasilishe vyeti vyake wizarani kwa ajili ya ukaguzi.
Hata hivyo, licha ya Dk. Mwaka kutekeleza agizo alilopewa Desemba 16 na waziri kukiri kuwa kweli vyeti hivyo vimefikishwa kwao na kuhakikiwa, bado suala lake linaelekea kusumbua kwani hadi kufikia jana, hakukuwa na ufafanuzi zaidi kama ilivyoahidiwa wiki iliyopita huku Dk. Kigwangalla akiutaka umma utulie na kusubiri taarifa ya ukaguzi kwani hivi sasa kuna masuala mengine ya kushughulikia.
“Tutawapa taarifa mara tutakapomaliza kuipitia ripoti hiyo, subirini tu kwa kuwa kuna kazi nyingi za kufanya wizarani,” Dk. Kigwangalla wakati alipoulizwa na mwandishi wa Nipashe jana kuhusiana na matokeo ya ukaguzi wav yeti mwaka kama alivyoahidi wiki iliyopita.
Akieleza zaidi, Dk. Kigwangalla alisema bado anaipitia ripoti hiyo na akishamaliza, atashauriana na viongozi wengine wa wizara yao akiwamo Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, na kisha ndipo ataitisha mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa.
ILIVYOKUWA
Desemba 14 ya wiki iliyopita, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya kustukiza kwenye kituo cha Dk. Mwaka ambaye amekuwa maarufu kutokana na matangazo mbalimbali anayotoa kila mara kuhusiana na tiba anazotoa.
Hata hivyo, baada ya Dk. Kigwangalla kufika kwenye kituo hicho, hakumkuta Dk. Mwaka na wenzake na ndipo (Dk. Kigwangalla) alipotoa amri ya kufungwa kwa muda kituo hicho akimtuhumu Dk. Mwaka na wenzake kumkimbia na kisha akaamuru apeleke vyeti vyake ili vichunguzwe na kuona kama huduma wanazotoa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.
Desemba 20, Kigwangalla aliiambia Nipashe kuwa ameshapokea ripoti yenye maelezo ya vyeti vya Dk. Mwaka na kwamba, angetoa ufafanuzi kwa vyombo vya habari Jumatatu au Jumanne (juzi au jana).
Sakata Dk. Mwaka Lawa Pasua Kichwa kwa Dk. Kigwangalla
0
December 24, 2015
Tags