Mara baada ya kuachiwa huru, Sheikh Ponda alisema pamoja na uamuzi huo wa mahakama, amekaa mahabusu kwa muda mrefu kutokana na dhamana yake kuzuiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hivyo haki yake imechelewa kutolewa.
Alisema ipo haja ya Katiba kufanyiwa marekebisho kwa kupunguza mamlaka ya DPP, yakiwamo ya kuzuia dhamana kwa kuwa yeye alikaa mahabusu ilhali hakuwa hana hatia.
Vilio vya furaha vilisikika kutoka kwa wafuasi wa Sheikh Ponda wakiwamo wanawake baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Mary Moyo kumuachia huru.
Kiongozi huyo wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu aliachiwa huru chini ya kifungu namba 235, cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 marejeo ya mwaka 2002.
Hakimu Moyo alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kwa namna gani maneno aliyoyatoa Sheikh Ponda, yameumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.
Wakili Abubakar Salimu ambaye alikuwa akimtetea Sheikh Ponda pia alisema mahakama imechelewa kutoa haki kwa mteja wake, na kwamba muda alioupoteza mahabusu hakuna mtu anayeweza kuulipa.
“Sheikh Ponda amekaa mahabusu kwa miaka miwili na miezi mitatu na katika kipindi hicho amefiwa na mama yake mzazi pamoja na baba mkwe wake, na hivyo kushindwa kuhudhuria mazishi, pia alitenganishwa na familia yake, ifahamike kuwa haki inayocheleweshwa ni sawa na haki inayonyimwa” alisema Wakili Salimu.
Mawakili wa Serikali, Sunday Hyera na George Mbalasa wao walisema kwa nyakati tofauti kuwa hawana cha kuzungumza, kwani tayari kesi imemalizika na mahakama imetoa maamuzi.
Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 2:30 asubuhi, akisindikizwa na polisi na askari wa kikosi maalumu cha Magereza waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Kiongozi huyo alionekana akijiamini na aliposhuka kwenye gari alikuwa mwenye furaha na baadaye alianza kusoma gazeti.
Wafuasi wachache wa Ponda waliruhusiwa kuingia ndani ya mahakama hiyo, huku wengine wakizuiwa nje ya uzio kutokana na sababu zilizoelezwa kuwa ni za kiusalama na kuifanya mahakama iwe katika utulivu.
Mashtaka
Awali, ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Agosti 10, 2013 saa 12.45 jioni Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege mkoani Morogoro, Sheikh Ponda alikaidi amri halali ya mahakama, kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa. Mashtaka ambayo aliyakana.
Hata hivyo, shtaka la kwanza na kutotii amri ya mahakama liliondolewa mahakamani hapo, baada ya Sheikh Ponda kushinda rufaa na hivyo kubaki na mashtaka mawili.
Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi tisa pamoja na vielelezo saba, ikiwamo kamera ambayo ilimrekodi Sheikh Ponda alipokuwa akitenda makosa hayo wakati upande wa utetezi ulikuwa na shahidi mmoja.