Nilikuwa Tukuyu, Mbeya kwa siku kadhaa. Njiani kwenda, safari yangu ilianzia Iringa, nikasimama na kuongea na Watanzania wa Kinyanambo, Mafinga Mjini, Kinegembasi, Makambako, Igawa, Uyole mpaka nikafika Tukuyu. Na kurudi nikasimama maeneo kadhaa pia.
Niseme tu, humo mote nilimopita, jina la John Magufuli limo midomoni mwa watu wengi. Watanzania wanaonekana kumkubali sana Magufuli, bila kujali tofauti zao za kivyama. Kuna hata niliowasikia wakitamka kuwa Magufuli atawale tu bila hata hao Mawaziri!
Ni dhahiri, wenye kutamka hayo wanaonyesha kuhamasika na utendaji wa Magufuli na sasa wanadhani hata hao Mawaziri watakuja kuharibu tu. Hata hivyo, ukweli wa kisayansi ni kwamba; Jahmuri inaweza kwenda kwa kipindi fulani bila uwepo wa mawaziri, lakini Jamhuri haiwezi kwenda kwa muda wote bila uwepo wa Mawaziri.
Lakini ni nini tafsiri haswa ya wanachokizungumza Watanzania juu ya Magufuli?
Ndugu zangu,
Mimi ni muumini wa mifumo. George Washington alipata kuwa Rais wa Marekani aliyependwa sana baada ya Abraham Lincoln.
George Washington kimsingi angeweza kuitawala Marekani mpaka pale alipohitaji mwenyewe kuondoka. Ndiye Rais, katika wakati wake, aliyejenga mifumo mipya na kuimarisha uchumi wa Marekani kwa kiwango kikubwa.
Lakini, kinachomfanya George Washington aendelee kuheshimika mpaka leo ni ule ujasiri wake wake wa kuyapa mgongo mazoea ya kale. George Washington aliamua kuitumia hali ya umaaarufu na kukubalika kwake na Wamarekani kwa kuhakikisha anabadilisha mifumo, hata ile iliyopelekea yeye kuingia madarakani.
Aliongoza kwa mihula miwili, na katika wakati wake mambo mengi ya kimfumo yalibadilishwa kuifanya Marekani kuwa bora zaidi kwenye masuala ya utawala.
John Magufuli ana kila nafasi sasa ya kuandika historia kwa kutumia umaarufu na kukubalika kwake, kuhakikisha anabadilisha mifumo hata iliyopelekea kumuingiza madarakani.
Kama Magufuli akitaka, Tanzania ya leo inaweza kuwa tofauti sana na ya jana, na ya kesho ikawashangaza hata watu wa dunia. Ni kuhakikisha kuwa anajenga mfumo ambao, hata kama yeye hatakuwepo madarakani, bado Tanzania na Watanzania watafuata na kuheshimu mifumo mipya itakayowekwa. Mifumo ambao, hata yeye Magufuli akigeuka kesho na kuturudisha tulikotoka, au kufanya maovu, bado mifumo itakayokuwepo iwe na uwezo wa kumshughulikia Magufuli.
Ni kwa maono ya kama watu wa aina ya George Washington, ndio maana Marekani imeweza hata kutawaliwa na Rais aliyeanzia kuwa mtangazaji wa vipindi vya michezo redioni na baadae akawa mcheza sinema, ni Ronald Reagan. Wamarekani hawakuwa na wasiwasi wa kuwa na Rais mcheza sinema kwa vile waliamini, kuwa akifanya madudu mfumo utamshughulikia.
Kwa nchi kama ya kwetu, lililo muhimu kwenye mifumo ni kwa wenye kukiuka sheria, kanuni na taratibu zitakazowekwa kuadhibiwa, na kwenye makosa ya ufisadi na uhujumu wa uchumi wa nchi, wenye kukutwa na hatia wasiadhibiwe kwa hukumu za kwenda jela, au ...sijui kulipa faini, bali kwenda jela na, ... kazi ngumu.
Kwa kuweka mifumo mipya, yenye kutanguliza maslahi ya nchi na si ya vyama, ni imani ya wengi, kuwa itakuwa ni amira ya chenga itakayopelekea uchumi wa nchi, kwa kasi ya ajabu, kuumuka mpaka mifuniko kuanguka.
Maggid,
Iringa.
Tafsiri ya Niliyoyasikia njiani nilimopita kumhusu Magufuli
1
December 03, 2015
Tags
TUMUOMBEE MUNGU AMTANGULIE KWA KILA ANACHOKIFANYA
ReplyDelete