WAKATI wapinzani wakipinga uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, waziri huyo amewasihi wananchi kumvumilia kidogo, ili baada ya muda mfupi atoe mpango wa maendeleo ya wizara hiyo, ambao pamoja na mambo mengine, utaelezea bei ya nishati hiyo itakavyoshuka.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Profesa Muhongo alisema mbali na mkakati wa kushusha bei ya umeme, kasi ya kusambaza umeme vijijini kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itarejea palepale.
“Nimepokea uteuzi huo, kinachofuata ni kuwatumikia wananchi, niwaombe tu wanivumilie kidogo nitawapa mpango wangu wa maendeleo wa muda mfupi na mrefu, lakini nisisitize tu nishati sio siasa, ni suala la utaalamu, liachwe lifanywe kitaalamu,” alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia bei ya umeme na upatikanaji wake, Profesa Muhongo alisema kupunguza bei hiyo ni ajenda muhimu itakayozingatiwa na kusema ili umeme uwe wa uhakika, ni lazima kuwe na mipango ya kuwa na nishati hiyo ya uhakika ifikapo mwaka 2025.
“Umeme wa uhakika utapatikana na matarajio yetu ni Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo tunatarajia uzalishaji wa nishati hiyo ufike Megawati 10,000 hadi 15,000,”alisema Profesa Muhongo.
Alisisitiza kwamba wizara yake haitategemea chanzo kimoja cha nishati bali wataangalia vyanzo vingine ikiwemo nishati jadidifu, upepo, gesi, makaa ya mawe, maji huku akisema vyanzo hivyo vikitumika kuzalisha nishati, ni wazi bei ya umeme itashuka na kushusha gharama nyingine za maisha na za uwekezaji.
Aliongeza katika kuendeleza sekta ya nishati suala la uwekezaji ni muhimu hivyo wizara yake inakaribisha wawekezaji wenye sifa, watakaowekeza kwenye sekta hiyo ili kuja na matokeo bora zaidi, wananchi wanufaike na rasilimali za nchi yao.
Pamoja na nia yake hiyo kwa wananchi, Profesa Muhongo anakabiliwa na pingamizi kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Lissu na Profesa Lipumba, wamekaririwa wakikosoa uteuzi wa Profesa Muhongo kwa madai kuwa wizara aliyopewa kuiongoza, ilikumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakati wa uongozi wake, ikasababisha ajiuzulu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba na Lissu katika kukosoa huko, hawakutaka kutumia kumbukumbu zilizo wazi kuwa uchunguzi dhidi ya Profesa Muhongo, ulibaini kuwa hakukiuka maadili yoyote katika sakata la utoaji wa karibu Sh bilioni 300 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
Matokeo ya uchunguzi huo yalitangazwa Mei mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambapo alisema Tume ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ndiyo ilifanya uchunguzi kama Profesa Muhongo alistahili kwenda kwenye Baraza la Maadili kujibu mashitaka, lakini hawakuona tatizo lake na kufunga shauri lake.
Balozi Sefue aliweka wazi kuwa Profesa Muhongo alijiuzulu kwa sababu za kisiasa, lakini kimaadili hakuhusika kwa namna yoyote, kutokana na uchunguzi wa Sekretarieti ndiyo sababu hakufikishwa katika Baraza la Maadili.
Kitu kingine ambacho Lissu na Profesa Lipumba, hawakutaka kuzungumzia ni utendaji wa Profesa Muhongo alipokuwa katika wizara wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa katika miaka miwili ya uongozi wake katika Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Muhongo alisimamia kwa umahiri usambazaji wa umeme vijijini.
Kabla ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo, Watanzania asilimia 14 tu ndio waliokuwa wakitumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12 walikuwa watumiaji wa mijini na asilimia mbili ndio walikuwa watumiaji wa vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, kati ya mwaka 2007 na mwaka 2010, kulikuwa na ongezeko la asilimia nne la watumiaji wa umeme, hali iliyoonesha kuwa ongezeko la Watanzania waliokuwa wakipata umeme, lilikuwa asilimia moja kwa mwaka.
Lakini baada ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo katika nafasi hiyo, katika muda mfupi wa uongozi wake, idadi ya Watanzania wanaotumia umeme iliongezeka na kufikia asilimia 36 katikati ya mwaka jana.
Kwa hatua hiyo, uongozi wa Profesa Muhongo ulivuka malengo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ndio msingi wa utekelezaji wa malengo ya Serikali, iliyotaka Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata umeme.
Katika kutimiza malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010, uongozi wa Profesa Muhongo, ulitangaza punguzo la gharama za kuunganisha umeme majumbani kutoka Sh 177,000 za awali hadi Sh 27,000 vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam limeanzia na limepita, lakini baada ya muda gharama hizo zilishushwa kwa vijiji vyote nchi nzima.
Profesa Muhongo mwenyewe alikaririwa akisema gharama hizo zitahusu miradi inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), katika kipindi ambacho makandarasi watakuwa wakiendelea na awamu ya pili ya miradi iliyoanza Machi mwaka huu na kutarajiwa kukamilika katikati ya mwakani.
makombo ya jk
ReplyDeleteTumpatie muda wa kufanya kazi. Ni msomi mzuri kama kuna makosa aliyafanya, ataweza kuyarekebisha. Tufanye kazi muda wa majungu umekwisha.
ReplyDeleteJames B.Kalugira.
hata mm ni mwathirika hapa. kipindi prof yupo madarakani kijijin kwetu kulikuja mchakato wa umeme lkn ghafla baada ya prof kuachia ngazi tumebaki tunaangalia nguzo tu zilizosimamishwa had leo hakuna kinachoendelea. labda amerud madarakani na sie tutakumbukwa sasa. Mungu ibariki Tanzania. nina imani na uteuzi wa Rais Magufuli
ReplyDeletekweli kabisa nchi ni masikini wahitaji ni wengi na katika huhitaji wao wanataka wapewe na yeyote awe mwizi au muuaji wao wanaangalia kile wanachotaka, nchi ikiwa masikini na wanaoikaa huwa masikini na mawazo yao huwa ya kimasikisikini.
DeleteALIYEMTEUA NDIYE ATAKAYELAUMIWA KWANI KAAMINI KAZI YAKE ATAMSIMAMIA TU, ONDOA SHAKA KWAO
ReplyDelete