Waziri Mkuu Acharuka.....Asema Wabadhirifu Watang'olewa Mara Moja,Asisitiza Wasomi Wako Wengi wanaotafuta Ajira

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya watendaji wa halmashauri nchini kwamba atakayebainika ametumia vibaya fedha za Serikali atang’olewa kazini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano haina mchezo na mtu.
 
Alitoa kauli hiyo jana mchana (Jumapili, Desemba 20, 2015)  wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo Lindi mjini.
 
“Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu,  ole wake. Yeyote atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng’oa. Wako wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira.”
 
“Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza kujali wananchi.  Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, ” alisema huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa pili. (Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza).
 
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Lindi Jana, aliwaeleza wakazi hao kwamba amekuja kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi kwamba hatawaangusha Rais John Pombe Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika ngazi ya Uwaziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Jordan Rugimbana ya kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi yake ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini.
“Uwanja huu lazima uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya Amri Rangers.  Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. Kwa hiyo timu aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi lakini pia iwajumuishe Meya na mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya Lindi, ” alisema.

Akielezea kuhusu mipango ya Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu alisema hivi karibuni mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi baada ya kampuni ya BG kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la Kikwetu ili wajenge mitambo ya kusafisha gesi.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili ifikapo Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki maonyesho ya NaneNane kitaifa mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad