Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.
“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
“Nataka kujua nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.
Tuhuma nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa maabara.
Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015
Tumbua majipu sasa ihamie na mikoani
ReplyDelete