Askofu Kanisa La Anglikana Atimuliwa kwa Ufisadi wa Mamilioni ya Pesa

KANISA la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) lililopo jijini Mwanza, limemtimua rasmi Askofu kanisa hilo, Boniface Kwangu, kutokana na ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni.

Askofu huyo ni wa pili kutimuliwa na uongozi wa kanisa hilo baada ya mwaka 2007 aliyekuwa Askofu wa dayosisi hiyo, John Changae na yeye kufukuzwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kitendo ambacho kinaonesha taswira mbaya kwenye kanisa hilo.

Pia Askofu Kwangu aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minane, katika uongozi wake alishawahi kutuhumiwa na waumini wake kuwa anajihusisha na dini ya Freemasons huku wengine walikuwa wakimtuhumu kwamba anatumia nguvu za giza.

Askofu Kwangu na wenzake wanne wanatuhumiwa na kanisa hilo kwa ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni pamoja na kuendesha kanisa hilo bila kufuata kanuni na taratibu za kanisa hilo kitendo ambacho kimesababisha kutimuliwa kwake.

Askofu Kwangu, anatuhumiwa na upotevu wa Sh. 500 milioni ya shule ya kimataifa ya Isamilo, kuuza gari la dayosisi hiyo, kufukuza wafanyakazi wa kanisa hilo na kusababisha wadaiwe Sh. 60 milioni, kujipatia kiasi cha zaidi ya Sh. 15 milioni kutoka kwa Mhasibu wa kanisa, Sam Wisa, bila kibali.

Akisoma tamko la kumfukuza kazi, Mwenyekiti wa Nyumba ya Wadumu kutoka DVN, Andrew Kashilimu, amesema askofu huyo ameisababishia hasara kanisa hilo zaidi ya Sh. 600 milioni, kutokana na kufanya kazi bila kufuata kanuni na taratibu.

Amesema kuwa askofu Kwangu amekiuka viapo vya uaskofu, katiba ya jimbo, katiba ya DVN na amekiuka maadili na kanuni, kuendekeza matabaka ndani ya wahudumu na waumini, kutoa ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.

Amesema katika kikao kilichoketi Septemba 1 mwaka jana, kilithibitisha mambo hayo na kukubaliana kwamba Askofu huyo ajiuzulu kwa afya ya kanisa la Mungu lakini alikaidi maagizo hayo mpaka kutoka kwa tamko hilo.

“Askofu (Boniphace Kwangu) ametumia vibaya madaraka yake na alikuwa anatumia vibaya mali na fedha za kanisa, kwa hali hiyo tusingeweza kuwa na kiongozi wa namna hiyo,” amesema Kashilimu.

Mmoja wa waumini ambaye alikumbwa na fagio la Askofu, Kwangu, Edwar Kibiti, amesema kwamba kutimuliwa kwa kiongozi huyo wa kiroho katika kanisa hilo kutasaidia kurudisha matumaini kwa waumini walio wengi.

Kibiti ambaye pia ni Mchungaji amesema kuwa walipokuwa wakijaribu kuhoji sababu za Askofu Kwangu kuuza mali za kanisa ikiwamo gari alilochangiwa na waumini alikuwa akiwafukuza watu waliotaka kufahamu suala hilo.

“Tulipokuwa tunahoji matumizi ya mali za kanisa tulichokuwa tukiambulia ni kwenda polisi na wengine wafukuzwa, huyu (Askofu Boniphace Kwangu) alikuwa anafanya kazi kwa majungu na mpaka anaondoka alishafukuza wachungaji 19,” amesema Kibiti.

Amesema kuwa baada ya askofu huyo kuona wachungaji wazawa wanaanza kumfuatilia alianza kutafuta wachungaji wengine kutoka nchi mbalimbali hususani kutoka Rwanda, ili kuficha maovu yake anayoyafanya.

Mmoja wa Waumini, Joycelyn Juma, amesema kilichomgharimu askofu huyo ni upungufu wa mambo ya kiuongozi ambayo yamechangia kusababisha kuwepo kwa mwanya wa wizi wa mali na fedha za kanisa hilo.

“Kiufupi nimefurahi sana kwa sababu mambo ya ufisadi ama wizi wa fedha haviendani na mambo ya Mungu na nimefurahi kuona suala hili limefikia mwisho na sasa tutakuwa na amani,” amesema Juma.

Sanjali na kufukuzwa kazi ya Uaskofu DVN, pia uongozi wa kanisa hilo limemfungulia kesi Askofu Kwangu na wenzake wanne, Katibu wa Bodi, James Mtaritinya, Mhasibu wa Shule ya Isamilo, Sam Wisa, Samson Maganga na John Magawa.

Kesi iliyofunguli ni Januari 10 mwaka huu, Mw/Rb/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Magufuli akamue majipu mpaka kwenye taasisis za dini,maana kesho utasikia kiongozi huyu aliyefanya kosa akiwa Anglican anapata kibali cha kuanzisha kanisa lingine.Wanahusika na sembe pia viongozi wa dini walio wengi.MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    ReplyDelete
  2. DU KUMBE SIO BAKWATA TU.ENDELEANI KUKAMUA MAJIPU

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad