Wakati hatua ya aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif, ya kujitoa kwenye mazungumzo ya maridhiano yaliyokuwa yakiendelea visiwani Zanzibar ikiwa imeacha mshangao kwa wananchi, Nipashe imebaini siri ya kujiondoa kwake.
Maalim Seif alijiondoa katika mazungumzo ya kutafuta maridhiano ya muafaka katika kamati iliyowajumuisha Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Katika kamati hiyo iliyowahi kukutana mara tisa kwa nyakati tofauti ili kutatua mgogoro huo bila ya kufikiana muafaka, inaelezwa kuwa kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya wastaafu hao na Maalim Seif.
Kutopatikana kwa muafaka wa vikao hivyo, Januari 11, mwaka huu, Maalim Seif alitoa sababu kadhaa za kutotaka uchaguzi huo kurudiwa huku akimwomba Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati mgogoro huo ili kupatikane kwa muafaka wa haraka.
KWA NINI SEIF AMEJITOA
Baada ya kuwapo kwa usiri mkubwa wa vikao vilivyokuwa vinafanyika katika kutafuta muafaka huo, Nipashe katika uchunguzi wake imebaini sababu saba zilizomfanya Maalim Seif kung’atuka kutoka katika kamati hiyo.
TOFAUTI ZA KIITIKADI
Historia iliyokuwapo tangu miaka ya 1950 ya tafauti za kiitikadi na kisiasa, bado zinaendelea kujitokeza hadi miaka ya sasa na kusababisha kurithishana kwa chuki kwa vizazi hadi vizazi.
Hali hiyo imejitokeza katika sherehe za mapinduzi zilizofanyika Januari 12, mwaka huu, pale baadhi ya wanachama wa CCM walipobeba bango lenye maneno “Machotara Hizbu waondoke Zanzibar ni nchi ya Waafrika”
Chuki iliyokuwapo baina ya chama cha ZNP na ASP miaka ya nyuma hadi kufanyika kwa Mapinduzi 1964, baada ya ASP kuungana na Umma Party na kuiangusha ZPPP bado inaendelea kujitokeza sasa baina ya CUF na CCM, huku ubaguzi huo ukijitokeza CUF ikitawala Pemba na baadhi ya maeneo ya Unguja na CCM kutawala Unguja
UHAFIDHINA
Hii mi moja ya sababu zilizofanya kiongozi huyo kujiondoka katika mazungumzo kwa sababu ya dhana ya kuwapo kwa makada ndani ya CCM wasiotaka mabadiliko ndani ya nchi.
Kuwapo kwa wanachama wenye msimamo mkali ndani ya CUF na CCM wasiobadilika kimtazamo, nayo ni sababu ya Maalim Seif kujiengua katika mazungumzo hayo.
Kwa mfano baadhi ya wanachama wa CUF kumtuhumu Maalim Seif kuwasaliti inadhirisha wazi kuwapo kwa misimamo mikali ndani ya vyama hivyo.
Ndani ya CCM kuna baadhi ya wanachama ambao hawako tayari kukabidhi Zanzibar mikononi mwa CUF, wako tayari kuona CCM ikitawala milele. Hiyo nayo huenda ikawa sababu mojawapo ya kiongozi huo wa CUF kujiengua katika kamati ya mazungumzo.
Tangu kuzaliwa kwa chama cha TANU 1954 hadi kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, chama hicho kimekuwa kikishika dola kwa miaka yote tangu kupatikana kwa uhuru 1961 na hata Mapinduzi 1964.
Kwa mujibu wa CUF na kauli zinazotolewa na Maalim Seif ni kuwa kuanzia mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, CUF imekuwa ikishinda kila uchaguzi unapofanyika lakini CCM imekuwa ikiwapora ushindi huo kwa kuchakachua matokeo.
Hata katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana uliofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), CUF wanadai kuwa walishinda uchaguzi huo, hivyo CCM wakatumia mbinu ya kufuta uchaguzi ili wapate mwanya wa kujipanga upya.
MUSTAKABALI WA MUUNGANO
Dhana ya kuwapo kuvunjika kwa Muungano kwa wananchama wa CCM endapo CUF itaongoza Zanzibar ni mojawapo ya sababu inayofanya CCM Zanzibar kutokukubali kuikabidhi nchi kwa upinzani.
Dhana hiyo pia ni sababu ya uchaguzi Zanzibar kufutwa na kutakiwa kurudiwaa, kwa dhana kuwa CUF inasimamia kuwapo kwa serikali tatu na mamlaka kamili, hivyo Muungano huenda ukavunjika.
Uwapo wa dhana hiyo na kufanyika kwa vikao mara tisa vilivyowajumuisha marais wastaafu kwa ajili ya kutafuta muafaka pasipo kuwapo kwa kiongozi mwingine zaidi ya Maalim Seif, huenda ndiyo sababu pia ya kujitoa kwake katika mazungumzo.
HAKUNA KIONGOZI WA KUKEMEA
Kutokuwapo kwa kiongozi mwenye uwezo wa kukemea mambo mabaya na maovu ambayo yanaweza kuitumbukiza nchi katika machafuko nako kumesababisha Maalim Seif kujitoa katika mazungumzo hayo.
Wakati wa uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi tangu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ulifanyika mwaka 1995 ambapo CCM ilipata asilimia 50.2 na CUF asilimia 49.8, mivutano ya kisiasa ilijitokeza.
Katika sokomoko hilo, CUF ilikataa kuyatambua matokeo hayo na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa wakati huo, Dk. Salmin Amour Juma.
Mivutano ya kisiasa ilijitokeza wazi wazi baina ya vyama hivyo- CUF na CCM, ambapo uhasama na chuzi za kisiasa zilishika kasi. Watu walikuwa hawashiriki hata katika masuala ya kijamii. Kama mtu amefariki dunia kwa mfano, iwapo ni wa CUF basi CCM hawatamzika na vivyo hivyo kwa CCM, CUF hawamziki.
Hatua hiyo ilimfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuingilia kati na kuagiza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). kukosekana kiongozi kama Nyerere kukemea na kutoa uamuzi kumechangia Maalim Seif kujitoa katika mazungumzo hayo.
KAULI ZA CCM NA CUF
Katika kile kilichoonekana ni kuvurugika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa visiwani Zanzibar, na kusababisha Maalim Seif kujitoa ni kauli za baadhi ya viongozi wakiwemo wakuu wa CUF, CCM na serikali za Zanzibar.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika hotuba yake aliyoitoa Januari 12, mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, aliwataka wafuasi wa CCM kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio utakaotangazwa na ZEC .
Kutolewa kwa kauli hiyo na kiongozi huyo ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya kusaka muafaka, huenda imechangia kumvunja imani Maalim Seif kuendelea kuhudhuria vikao vya kamati hiyo na kuamua kujiengua.
Kadhalika, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliwahi kuwaeleza wanachama wa CCM kujiandaa na marudio ya uchaguzi wakati kamati ikiwa bado inaendelea kutafuta muafaka.
Pia aliwataka wana CCM Zanzibar kujiandaa na uchaguzi wa marudio na kuepukana na propaganda zinazotolewa na wapinzani kwamba hakuna uchaguzi mwingine, huku akieleza kuwa kwa upande wao wako katika maandalizi ya uchaguzi mwingine ikiwemo kutayarisha mawakala watakaosimamia.
Vilevile, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jusa Ladhu, aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema uchaguzi Zanzibar hauwezi kurudiwa.
Maalim Seif naye amewahi kueleza msimamo wa CUF wa kutotaka uchaguzi urudiwe bali kuendelea kwa kazi ya kuhesabu kura.
MUUNDO WA KAMATI
Hii pia ni sababu nyingine iliyomfanya Maalim Seif kujiweka kando katika kamati ya kutafuta muafaka visiwani humo, hivyo kusababisha sintofahamu na mustakabali wa siasa za Zanzibar.
Jopo la wanakamati wanaounda kamati hiyo ni wanachama wa CCM hata mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Ali Mohammed Shein ni mmoja wa wagombea urais.
Kuwapo kwa Maalim Seif peke yake na kutokuwapo kwa wajumbe wengine kutoka vyama vingine vya upinziani, kumesababisha Maalim Seif kuitwa ‘msaliti’ na wanachama wenzake wa CUF.
Maalim Seif amekuwa akihudhuria vikao vyote tisa peke yake kutoka CUF wakati CCM imekuwa ikiwakilishwa na Dk. Shein, Mwinyi, Mkapa. Dk. Salmin, Karume na Balozi Iddi.
KUTOAMINIKA ZEC
Tangu Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi Oktoba 28, mwaka jana, siku tatu baada ya kumalizika kupiga kura kwa kile kilichoelezwa ni uchaguzi kuwa na kasoro, wanachama wa CUF walikosa imani na ZEC kwa kudai kuwa mwenyekiti huyo hakunukuu kifungu chochote cha katiba au sheria kilichompa mamlaka ya kufuta uchaguzi huo.
Toka kufutwa kwa uchaguzi huo, CUF wamekuwa wakimtaka Mwenyekiti
Jecha kujiuzulu na kuvunjwa kwa tume hiyo na kuundwa mpya.
Vilevile kuwapo kwa madai ya muda mrefu ya kuhitaji kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi na CUF ni mojao ya sababu za chama hicho kutokuwa na imani na ZEC na Maalim Seif kujiondoka katika mazungumzo.
MAZUNGUMZA YA MUAFAKA ZANZIBAR
Mazungumzo ya kwanza ya kusaka muafaka wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokana na utata wa matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 1995, yaliyosimamiwa na Jumuiya ya Madola chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Chifu Emeka Anyaoku, aliyewakilishwa na mjumbe wake, Dk. Moses Anafu.
Licha ya makubaliano hayo yaliyotiwa saini na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin na Maalim Seif katika Ikulu ya Zanzibar Juni 1999, utekelezaji wake ulikwama kutokana na sababu ambazo hazikujulikana.
Mazungumzo ya pili ya kusaka mgogoro ulioibuka mwaka 2001 baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000 na kusababisha mauaji ya zaidi ya wafuasi 30 wa CUF, wakati wakiandamana Unguja na Pemba kupinga matokeo hayo, yalianza Machi, 2001 chini ya makatibu wakuu wa vyama hivyo, Philip Mangula (CCM) na Maalim Seif (CUF).
Muafaka ulifikiwa na makubaliano na kutiwa saini katika Ikulu ya Zanzibar na makatibu wakuu hao mbele ya wenyeviti wa vyama hivyo, Benjamin Mkapa (CCM) na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF pamoja na mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Ikulu ya Zanzibar Oktoba, 2001.
Kama ilivyokuwa katika mazungumzo ya kwanza, utekelezaji wa makubaliano hayo ulikwama kutekelezwa, ikiwamo waathirika wa matukio ya mauaji yaliyofanywa na polisi kulipwa fidia kama ilivyopendekezwa na Tume ya Hashim Mbita, iliyochunguza tukio hilo.
Mgogoro uliozuka wakati na baaada ya wa uchaguzi wa mwaka 2005, ulisababisha Rais Jakaya Kikwete wakati wa kulizindua Bunge la tisa Desemba 30, 2005 kuwaelekeza makatibu wakuu wa CCM na CUF, kufufua mazungumzo ya kusaka muafaka mwingine.
Mazungumzo hayo yaliyoanza mapema mwaka 2006 kwa kusimamiwa na Yussuf Makamba (CCM) na Maalim Seif, yalikoma mwaka 2008 muda mfupi kabla ya vyama hivyo kutoa taarifa ya pamoja juu ya waliyokubaliana. Hatua hiyo ilitokana na kitendo cha Baraza Kuu la uongozi la CUF kutangaza baadhi ya makubaliano hayo kwa waandishi wa habari ikiwamo kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Baada ya mkwamo huo, mwaka 2009, Rais Karume na Maalim Seif walikutana binafsi Ikulu, Zanzibar, na kukubaliana vyama hivyo kumaliza uhasama ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Makubaliano hayo yalitekelezwa kisheria kwa kuifanyia Katiba ya Zanzibar marekebisho mwaka 2010 ikiwamo kuruhusu kura ya maoni, ambayo ilifanyika mwaka huo na wananchi wengi kukubali kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Kuundwa kwa serikali hiyo, baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 uliompa ushindi mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kulisababisha mgawanyo wa madaraka baada ya Maalim Seif kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na nafasi ya Makamu wa pili wa Rais kwenda kwa Balozi Seif Ali Iddi huku vyama hivyo vikigawana nafasi za Baraza la Mawaziri.
Serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo iliyoifanya Zanzibar kuwa na utulivu wa kisiasa kabla ya kuibuka kwa mgogoro wa sasa uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
WANASHERIA, WANASIASA Z'BAR WANENA
Baadhi ya wanasheria na wanasiasa, wamesema muafaka wa kuleta suluhu ya mkwamo wa uchaguzi mkubwa Zanzibar, unakwamishwa na kukosekana kwa ukweli na nia njema miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mazungumzo hayo.
Walikuwa wakizungumzia uamuzi wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif kujiondoa katika mazungumzo ya kutafuta muafaka huo.
Mazungumzo hayo yanaongozwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na wajumbe wake akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Marais wastaafu akiwamo Dk. Salmin Amour, Dk. Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
NASSOR MOYO
Mwanasiasa mkongwe Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, alisema baadhi ya viongozi ndani ya CCM, hawana ukweli katika kutafuta muafaka wa kumaliza mgogoro huo.
“Tatizo letu viongozi wetu CCM hasa Zanzibar, waliopumzika kazi na wale wamo serikalini na nje, baadhi yao hawana ukweli na bila ya ukweli jambo lolote haliwezi kukamilika na kuleta tija kwa wananchi wake,” alisema Moyo Waziri wa kwanza wa Katiba na Sheria baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Alisema kabla ya mazungumzo hayo kuanza kufanyika, viongozi walitakiwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na kuacha itikadi na utashi wa kisiasa wa vyama vyao, jambo ambalo halikufanyika.
Alisema Kamati ya Maridhiano ya kutafuta muafaka wa mpasuko wa kisiasa mwaka 2009, ilipata mafanikio na kuzaliwa serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya wajumbe wake sita kutoka CCM na CUF kufanya kazi bila kujali maslahi ya vyama vyao.
Moyo alisema siasa za Muungano si kikwazo kwa Zanzibar kumaliza matatizo yake ya kisiasa, isipokuwa kuna watu wamekuwa wakipandikiza siasa zisizofaa dhidi ya uhai wa Muungano kama kutatokea mabadiliko ya kiutawala na Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar.
“Hakuna mwanasiasa anayetafuta mabadiliko ya kiutawala Zanzibar kwa madhumuni ya kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mawazo hayo hayafai," alisema Moyo.
Moyo alisema kuwa hakuna mwanasiasa mwenye ubavu wa kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hata kama kutatokea mabadiliko ya kiutawala Zanzibar kutokana na uimara wa misingi ya Muungano.
Alisema misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyowekwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Karume, ipo imara katika Jamhuri ya Muungano.
Alisema wanasiasa Zanzibar lazima wakubali kubadilika kimawazo na kifkira na kuwa tayari kukubali misingi ya demokrasia ya kushinda na kushindwa katika uchaguzi.
“Tumekubali mfumo wa vyama vingi, lazima tuwe tayari pia kukubali matokeo pale unaposhinda au kushindwa hiyo ndiyo demokrasia,” alisisitiza Moyo.
RAIS WA ZLS
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, alisema wakati umefika kwa Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema mazungumzo hayo yatafanikiwa kama watashirikishwa watu huru badala ya kuendelea na viongozi kutoka pande mbili zinazovutana.
Awadh, ambaye ni Wakili mkongwe wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, alisema mkwamo wa uchaguzi mkuu Zanzibar, unahusu Katiba na sheria na hauwezi kupata ufumbuzi kwa njia za kisiasa kutokana na kila upande kutetea maslahi yake.
Alisema Rais Magufuli kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama, bado ana jukumu kubwa la kumaliza mgogoro huo katika kuimarisha amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa zamani Zanzibar, Hamid Mbwezereni, alisema mahakama pekee ndiyo ina uwezo wa kutafsiri Katiba na kuangalia kama Mwenyekiti wa Zec alikuwa na mamlaka ya Kikatiba na sheria kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema kama kuna watu wanapinga maamuzi ya Mwenyekiti, wanatakiwa kwenda mahakamani badala ya kuendelea kulalamika nje ya mfumo wa sheria.
NAIBU KATIBU MKUU CCM Z'BAR
Naibu Katibu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hawezi kutoa msimamo wa Chama baada ya Maalim Seif kujiengua katika mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi kabla ya kutolewa rasmi taarifa na kamati ya Mazungumzo hayo.
Hata hivyo, alisema CCM bado inaamini mazungumzo ndiyo muafaka katika kumaliza matatizo ya migogoro ikiwamo ya kisiasa.
“NAIBU KATIBU MKUU CUF
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu CUF Tanzania Bara, alisema kujitoa kwa Maalim Seif katika mazungumzo hayo, kutafanya watu wengine waingilie kati hali itakayofanya Zanzibar isiwe salama.
Alisema kwa uelewa wake, madhumuni ya vile vikao ilikuwa ni kutoa matunda mazuri.
“Habari ya Zanzibar kila mtu anajua ukweli ukoje hata CCM wenyewe, kilichofanyika sasa hivi ni makusudi kupindisha ukweli, Maalim Seif alikubali kuingia kwenye vikao vya maridhiano akijua wenzake watakaa wafikirie mbele ili kutoa kitu chenye manufaa kwa Wazanzibar,” alisema Sakaya.
Alifafanua kuwa Maalim Seif kwenda katika vikao hivyo peke yake, ilikuwa ni tatizo, lakini katika vikao vya chama tangu mwaka jana walitoa msimamo wao kama chama.
Naye Mhadhiri kutoka UDSM Idara ya Sayansi ya Siasa, Dk. Rasul Ahmed, alisema kujitoa kwa Maalim Seif kunaweza kuongeza au kuchochea mgogoro zaidi.
Alisema Maalim Seif angepaswa kuwa mvumilivu au kutafuta njia nyingine nzuri ya kuboresha mazungumzo hayo kuliko uamuzi aliouchukua kwa kuwa athari zake zinaweza kuwa mbaya mbele.
Hata hivyo, Profesa Mohamed Bakari, kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa UDSM, alieleza kuwa hatua ya Maalim Seif kujitoa kunamaanisha matumaini ya kupatikana kwa suluhu yamepungua.
Alisema athari za mgogoro huo endapo hautapatiwa ufumbuzi, kiwango cha misaada itapungua kutoka kwa wafadhilri, akitolea mfano Tanzania ilivyokosa fedha za MCC.
CHANZO: NIPASHE
Udaku Special Blog
Siri Kuvunjika Mazungumzo ya Mwafaka Zanzibar Zavuja
0
January 21, 2016
Tags