Hakuna Kupanda Ndege Bila Kibali cha Raisi...Hapa Kazi Tu Inaendelea..

Katika kile kinachoonekana kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli haitalegeza kamba linapokuja suala la kusitisha safari holela za nje za watumishi wa umma, Idara ya Uhamiaji imesema bado inakagua uwapo wa barua ya mwajiri na kibali maalum cha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Awali, ili kusafiri nje ya nchi mtumishi wa umma alihitaji pasi ya kusafiria yenye viza na tiketi.

Akizungumza na Nipashe kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile, Msemaji wa Idara hiyo Tabu Burhan, alisema idara hiyo inaendelea kusimamia kikamilifu maelekezo ya Rais.

Katika utekelezaji wa agizo hilo, kila mtumishi wa umma anayesafiri nje ya nchi anatakiwa kuonyesha barua ya mwajiri wake na kibali cha Ikulu, alisema.

Burhani alisema Idara hiyo inafanya ukaguzi huo katika vituo vya usafiri kama viwanja vya ndege na mipakani ili kubaini watu watakaokiuka kwa makusudi agizo la Rais Magufuli.

Burhan alisema ingawa kazi ya kuwadhibiti watumishi wa umma wanaosafiri nje ni ngumu kutokana na hati zao za kusafiria kutoonyesha kazi wanazofanya, lakini wamejipanga vizuri kutumia mbinu mbalimbali kuwabaini.

Tutawabana wakija kugonga mihuri hati za kusafiria, tukigundua ni mfanyakazi wa serikali tutamuomba atupatie barua kutoka kwa mwajiri na kibali cha Ikulu, kama hana tunamrudisha na hataweza kusafiri,” alisema Burhan.

Alisema zamani ilikuwa rahisi kwa kila mtumishi aliyetaka kusafiri nje ya nchi kutambulika kazi yake kwasababu walikuwa wakitakiwa kujaza fomu iitwayo TIF 10 na TIF 12, mfumo ambao ulisitishwa mwaka 2005 baada ya kuanza kutumika hati za kusafiria za kieletroniki.

“Tunawashauri watumishi ambao wanataka kusafiri wajiridhishe wenyewe kwanza, itakuwa usumbufu na hasara endapo tutawarusidisha wakiwa tayari uwanja wa ndege,” aliongeza.

Akizungumzia idadi ya watu waliozuiliwa tangu kuanza kwa utekelezaji wake, msemaji huyo alisema mpaka sasa hakuna mtumishi aliyenaswa mbali na wafanyakazi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ambao tayari wamesimamishwa kazi.

Watumishi hao ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.

Agizo la kuwazuia watumishi kusafiri nje lilitolewa na Rais Magufuli siku moja baada ya kuapishwa kwa lengo la kubana matumizi ya serikali na hadi sasa ameshaokoa mabilioni ya fedha.

Akilihutubia Bunge la 11 na kulizindua mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli aliwataka watanzania na wabunge waunge mkono uamuzi wake wa kupiga marufuku safari za nje ambapo fedha nyingi zitaokolewa na kutumika kwenye huduma za jamii kama barabara, afya na elimu.

Alitoa mfano kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2013 na nusu ya 2014/2015 pekee, safari za vigogo nje ya nchi ziligharimu Sh. bilioni 356.3 fedha ambazo alisema zingeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilomita 400 au kutimiza miradi mbalimbali ya jamii.

Alisema tiketi za ndege pekee ziligharimu Sh. bilioni 183.160, mafunzo ya nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu Sh. bilioni 104.552.

Novemba mwaka jana, Ikulu ilisambaza mwongozo unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kuyatimiza ili wapewe kibali cha kusafiri.

Sharti la kwanza ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na maombi yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda kwa Sefue ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa safari hiyo na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.

Sharti lingine linamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama taasisi apime kama safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kabla ya kuwasilishwa Hazina na aeleze manufaa ambayo nchi itapata kutokana na safari hiyo.

Pia sharti lingine linataka mhusika aeleze umuhimu wa safari hiyo na isipofanyika itaathiri vipi nchi. Mwombaji aanatakiwa aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na taifa; kama imewahi kufanyika huko nyuma ilisaidia nini.

Ofisi za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba 12 mwaka jana ikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake. Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad