KIMENUKA Kwa Sumaye Wananchi Wavamia Shamba Lake na Kujimilikisha na Kufanya Haya

Wananchi zaidi ya 100, wakiwemo waliobomolewa maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wamevamia shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33, lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande na kujikatia viwanja.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano kati ya mwaka 1995 hadi 2005, amekiri wananchi kuvamia shamba hilo lakini alisema hana wasiwasi kwasababu ana hati za umiliki.
Aidha alisema atafuata mkondo wa sheria kuhakikisha wavamizi hao wanaondoka kwenye shamba lake.
Juzi Nipashe ilishuhudia wananchi kadhaa wakiendelea kujenga nyumba za miti na wengine za matofali baada ya kujigawia kila mmoja eneo lake kwenye shamba hilo.

Musa Juma, aliyekutwa kwenye shamba hilo akijenga nyumba, alisema yeye ni miongoni mwa waathirika wa bomoa bomoa iliyofanyika Kinondoni Mkwajuni na kwamba amefika hapo baada ya mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Ema kuwaeleza kuwa kuna pori la Sumaye alilolitelekeza.
“Mwenzetu Ema alikuja kule bondeni tulikobomolewa na kutupa habari hiyo hivyo watu kama 100 tukaamua kuja na tukawakuta wengine tuliliona shamba hili likiwa ni pori kubwa ndipo tukaanza kujigawia vipande vipande,” alisema.

“Tumefanya kazi kubwa ya kulifyeka mpaka unaliona lipo katika hali hii, kazi haikuwa ndogo dada yangu, tumekutana na nyoka wakubwa, ukishuka kule bondeni kwenye kingo za shamba utajionea mwenyewe jinsi pori hili lilivyokuwa.” 
Juma alisema walivamia shamba hilo mwezi Oktoba mwaka jana, na wengine walikuja baadaye baada ya kupata taarifa kuwa kuna shamba la bure ambalo limetelekezwa akiongeza kuwa wako pia watumishi wa serikali waliovamia shamba hilo.

“Aliwahi kuja mwanamke mmoja ambaye hatumfahamu akidai kuwa yeye ni mke wa kiongozi huyo na kutueleza kuwa tunapaswa kuondoka eneo hili eti ni mali yao lakini juzi kaja mwenyewe Sumaye; akatusalimia na kuondoka bila kusema lolote,” alisema.
“Mwamamke yule alikuja na watu wengine akiwemo mtu ambaye alikuwa akipiga picha na baadaye aliondoka hadi Alhamisi ya wiki hii walivyokuja wote na Sumaye mwenyewe ingawa hakusema lolote mpaka anaondoka hapa.

“Sumaye alikuja kwa sababu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, aliitisha mkutano na wananchi wa hapa, lakini tukiwa tumekusanyika tukimsubiria Makonda ghafla alifika Sumaye, ambaye hakushuka kwenye gari lake, alitusalimia kwa kutunyooshea mikono na kuondoka kwasababu Makonda hakuja siku hiyo.”
Alipoulizwa sababu za kuvamia shamba hilo, alisema walimsikia Rais John Magufuli kwenye kampeni akisema kuwa mashamba yote ambayo hayajaendelezwa yarudishwe serikalini na wapewe watu wenye uwezo wa kuyaendeleza.
Juma alisema wamejigawia shamba hilo na sasa wanasubiri serikali ije kuidhinisha kwa kuwamilikisha wao.

“Mtu anahodhi shamba kubwa kama hili halafu halijapimwa, tumetafuta alama za mipaka hakuna, wakati mashamba yote yaliyolizunguka shamba hili yamepimwa,” alisema.
Sumaye alisema anamiliki shamba hilo kihalali na ana hati zote na kwamba upo utaratibu wa kuchukua mashamba yaliyotelekezwa lakini sio huo walioutumia wananchi hao.
“Shamba hatujalitelekeza kama wanavyodai hao wananchi, tuna hati na ni letu kihalali, wanasema halina alama za mipaka je, waulize hati nilipataje? Shamba lina alama labda kama wamezing’oa kwa sababu ya jeuri.” 

Sumaye alisema juhudi za kuhakikisha shamba hilo linarudishwa mikononi mwake zimeanza kufanyika na mamlaka husika na kusisitiza kuwa hatatumia nguvu kuwaondoa zaidi ya kufuata sheria.
Kuhusu kuonekana eneo hilo siku ya Alhamisi, Sumaye alisema alienda huko kwa sababu Makonda aliitisha mkutano na wananchi ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo lakini hakufika baada ya kupata udhuru.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Jastine Chiganga, alisema alipigiwa simu na Makonda akimweleza kuhusu mkutano huo lakini hakuweka bayana sababu za kuuitisha, ingawa aliuahirisha baada ya kupata dharura.

Makonda alilipoulizwa kuhusu lengo la mkutano aliouitisha na baadaye kuuairisha, alisema lilitokana na ofisi yake kupokea malalamiko ya uvamizi wa mashamba unaofanywa na wananchi eneo hilo.
Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo aliomba kukutana na viongozi wa mitaa husika, wananchi, watu wa ardhi na wamiliki wa mashamba hayo ili kujua ukweli kuhusu mgogoro huo.
“Hilo shamba linalodaiwa kuwa ni la Sumaye, sijawahi kupokea malalamiko kutoka kwake dhidi ya uvamizi huo ila niliwahi kupigiwa simu na mmoja wa Makamanda wa Polisi Mkoa ambaye alinieleza kuhusu uvamizi huo,” alisema.

Aidha, Makonda alisema mbali ya shamba hilo la Sumaye yapo mengine likiwemo la Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), marehemu Daudi Ballali ambalo nalo limevamiwa.
Alisema mkutano wake aliouitisha ulilenga kwenda kupata taarifa kamili ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Makonda alitoa wito kwa watu wanaodai ni wamiliki halali wa mashamba yaliyovamiwa wajitokeze katika mkutano atakaouitisha wiki ijayo eneo hilo ili ufumbuzi uweze kupatikana.
Tags

Post a Comment

7 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. yeye si aliwaiba wananchi?

    ReplyDelete
  2. MKUKI KWA NGURUWE KWA BINAADAMxxxxx

    ReplyDelete
  3. Haiwezekani mtu 1 amiliki eneo kubwa wakati wengine hawana pa kukaa

    ReplyDelete
  4. Sasa hilo ni shamba au pori?? Kama ni shamba lilikuwa na mazao gani?? Wanafuga vichaka vya kujifichia wezi na majambazi tu.

    ReplyDelete
  5. HIVI HUYO SUMAYE HANA HATA AIBU ANGALAU KIDOGO, KAJIPENDELEA ENEO KUBWA HALAFU HANA KAZI NALO. KULE MOROGORO NAKO KAFUGA PORI JINGINE, UKISIKIA 'MABEPARI' NDIO HUYO SUMAYE NA GROUP LAKE WANAOFUGA MAPORI BILA KUYAENDELEZA....

    ReplyDelete
  6. Na sio yeye tu(Sumaye)mwenye ardhi/shamba lenye hekari kubwa namna hiyo ni karibu viongozi wote wameishajikatia hekari kubwa kubwa tu wengine wanawauzia wananchi kwa bei double kupitia madalali ili wao wasijulikane huwa nashangaaga sana mnaposema eti Tanzania ni nchi ya demokrasia(mnaeelewa neno"DEMOCRACY" hilo lina maana gani?)bado safari ndefu sana kuifikia demokrasia mnayoisema hiyo nchi ipo chini ya mabepari wachache wanaowagandamiza bila ya huruma Watanzania wenzao ambao ni wengi waendelee kuishi maisha ya chini na ya dhiki kutokana na mifano mibaya iliyoonyeshwa na viongozi waliotangulia kabla ya kujilimbikizia mali kama hawana akili nzuri sasa imekuwa ni kama imeishahalalishwa kisheria kuwa pindi utapatapo wadhifa wowote ule ndio lazima uwe fisadi inasikitisha na kutia uchungu sana kuna siku hiyo amani tunayoilingia kila siku itakwisha kwani itakuja kuwa enough is enough kwa watu wa chini kugandamizwa na wachache katika nchi yao wenyewe

    ReplyDelete
  7. Safi sana!Sumaye nae bwana,si alikuwa mstari wa mbele kutaka mabadiliko kupitia UKAWA?ndio kama mngeshinda ni dhahiri wananchi tungenyonywa.Iwe kila kwenye eneo ambalo kiongozi kashika bila kulimwa linapaswa wapewe wananchi.kila mtu ale matunda ya nchi hii sio mabwanyenye tu.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad