Magufuli na Edward Lowassa Wote Kwa Bwana Samatta

Si wanasiasa, si wanamichezo, wasanii na wengine wote walikuwa kitu kimoja wakati walipoungana kutoa salamu za pongezi kwa mshambuliaji nyota wa mpira wa miguu nchini, Mbwana Samatta kwa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika.

Kundi hilo la wapeperusha salamu linaongozwa na Rais John Magufuli ambaye katika salamu zake za pongezi alizomtumia Waziri wa Michezo, Nape Nnauye, alisema; “tuzo hiyo imemjengea heshima Mbwana Samatta mwenyewe, wanasoka hapa nchini na Tanzania kwa ujumla katika medani ya soka la kimataifa”.

Pia, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikuwa miongoni mwa waliotuma salamu za pongeza akisema: “Ushindi wa Samatta ni changamoto kubwa kwa wanasoka wa Tanzania, lakini zaidi kwa Serikali kuwekeza kwenye eneo hilo.”

Samatta, ambaye anatarajiwa kuihama klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kujiunga na FC Genk ya Ubelgiji, alishinda tuzo hiyo ya Mwanasoka Bora wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa Wachezaji wa Barani Afrika juzi kwenye hafla iliyofanyika Lagos, Nigeria.

Mshambuliaji huyo, mwenye umri wa miaka 24, anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kutwaa tuzo hiyo baada ya kuiongoza TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika akiwa amefunga mabao sita.

Pia, ndiye mfungaji tegemeo wa Taifa Stars, akiwa amefunga mabao mawili kwenye raundi mbili za michuano ya awali ya Kombe la Dunia dhidi ya Malawi na Algeria, ingawa Stars ilitolewa kwa jumla ya mabao 7-2 na wababe hao wa Afrika Kaskazini.

Jana ilikuwa siku ya shangwe kwa Watanzania baada ya Samatta kutwaa tuzo hiyo usiku, baadhi wakituma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na wengine taarifa kwenye vyombo vya habari kupongeza.

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa Dk Magufuli amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amfikishie salamu zake kwa nyota huyo.

Katika salamu hizo, Dk Magufuli amewasihi wanasoka wote na wadau kuongeza juhudi za kuundeleza mchezo huo ili upige hatua zaidi za kimaendeleo.

Naye Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema, alisifu juhudi za Samatta.

Huyu kijana kufikia hapo ni kujituma, lakini zaidi ni malezi aliyoyapata katika timu yake ya TP Mazembe... ni lazima tuwe na utaratibu wa kujenga shule za kukuza vipaji vya soka (academy), tutawapata akina Samatta wengi,” alisema Lowassa.

Alisema Serikali isione shida kuchukua ilani ya Chadema iliyoridhiwa na Ukawa ambayo inataka kufutwa kodi kwa vifaa vyote vya michezo.

“Wasione haya kuchukua ilani yetu. Sisi tulitangaza kuwa tutafuta ushuru kwa vifaa vyote vya michezo pamoja na kuanzisha academy ili kuinua vipaji. Tunaamini kwa kufanya hivyo watapatikana akina Samatta wengi tu na si katika soka, bali hata michezo mingine kama riadha na ngumi.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, ambaye ni shabiki maarufu wa klabu ya Yanga, aliandika kwenye ukurasa wake wa Tweeter kumpongeza Samatta akisema ushindi wake umeipa heshima nchi.

Hongera sana, ufanikiwe zaidi ya hapa,” alisema Nchemba katika ujumbe wake.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika naye hakuwa nyuma kumwagia sifa Samatta, akisema mafanikio yake yanadhihirisha pasi na shaka uwepo wa vipaji lukuki hapa nchini ambavyo hupotea bila kufikia ukomo wa juu wa ndoto na uwezo wao.

Tunahitaji mikakati sahihi, utekelezaji na uwekezaji wa kutosha katika soka. Inawezekana! Tuiangalie hii kama fursa ya kuwakwamua vijana wetu kuzalisha ajira na wao kutimiza ndoto na matamanio yao,” alisema Mnyika katika salamu zake.

Kufeli mtihani si kufeli maisha

Nyumbani kwa wazazi wa Samatta na shuleni kwake ilikuwa ni kutafakari safari ya mshambuliaji huyo tangu utotoni.

“Haya ni mafanikio makubwa,” alisema mwalimu wa michezo wa Shule ya Sekondari ya Thaglan ya Mbagala, Mapesi Jamal ambaye hivi sasa amehamishiwa Kisiju wilayani Mkuranga.

Niligombana naye sana nikitaka apende vitu vyote viwili (shule na mpira) kutokana na kutokuwa vizuri darasani, ndiyo maana matokeo yake ya mwisho hayakuwa ya kuridhisha.

“Nakumbuka (baadaye) niliwahi kumwambia ajitahidi sana kupenda mpira na uwe ndiyo chaguo lake la kwanza baada ya kugundua kuwa darasani ameshindwa.

“Tangu ajiunge kidato cha kwanza alikuwa tayari ameanza kujifunza soka kwenye kituo cha Jamal Kisongo alikokuwa akichezea timu ya vijana ya klabu ya Mbagala Market.”

Mwalimu Mkuu wa Thlagan, Juma Nyenga ambaye kwa sasa ni mlezi na mshauri wa shule hiyo, alimwelezea Samatta kuwa ni kijana mpole ambaye hakukatishwa tamaa na matokeo mabaya ya kidato cha nne.

Alionyesha njia nyingine ya kupata mafanikio ambayo ni soka,” alisema Nyenga.

Nyange aliiambia Mwananchi kuwa wamefurahishwa na mafanikio ya Samatta kwa kuwa yanamtangaza yeye, shule na nchi yake.

Alisema kuna kipindi aliingia kwenye matatizo ya kitaaluma na walilazimika kumuita baba yake shuleni.

“Mzee Samatta ni muelewa pia, alituambia mfumo wa mwanaye na kutuomba tumsaidie jinsi ya kuendesha maisha yake kwa kuwa tayari ameonyesha kuwa alikuwa anapenda soka kuliko shule. Ingawa hata sisi tulitaka apende vitu vyote kwa pamoja, nililazimika kumpa adhabu ya kumchapa viboko vinne mbele ya mzazi wake,” alisema.

Nyenga anasema tangu siku hiyo alirudisha mapenzi ya kuhudhuria vipindi.

Walimu hao wanaona Samatta bado hajachelewa kujiendeleza kielimu.

Tunaposema arudi darasani si kwenda kusoma masomo yote upya, kwa vile amekuwa ni wa kimataifa na matokeo yake hayakuwa ya kuridhisha, anatakiwa kujiendeleza kwa kusoma lugha ya Kiingereza,” alisema

“Pia kama ameweza kufuata miiko ya soka, basi anatakiwa aendelee hivyohivyo maana hiyo pekee ndiyo itampa mafanikio zaidi huko mbele. Awe na nidhamu si uwanjani pekee, hata nje ya uwanja kama alivyo sasa, awekeze kwani mpira una muda wake,” alisema Mapesi.

Baba amwaga machozi

Baba yake mzazi, Ally Samatta alisema aliangua kilio mara baada ya mwanaye kutangazwa mshindi.

Nilifuatilia kuanzia mwanzo hadi mwisho. Walipotangaza sikuamini, nilijikuta naangua kilio mpaka majirani walishtuka,” alisema mzazi huyo.

Nimefurahi na ninampongeza sana kwa hilo, pia nawashukuru Watanzania wote waliowezesha hili kwa njia moja au nyingine.

“Nilimpa maneno ya siri alipokuwa anakwenda huko na hata atakaporudi nitamwambia. Nashukuru huwa anazingatia. Samatta amekuwa mchezaji bora kama nilivyokuwa mimi mwaka 1964 nilipotwaa tuzo hiyo kwa Tanganyika ila yeye kanifunika kabisa.”

Mama mlezi wa Samatta, Khadija Abdallah naye alikuwa na furaha.

Mimi nilijikuta presha inapanda huku kichwa kikiniuma sana, hatujalala kabisa kwani bado hatuamini kwa kweli. Tumelala saa 11 alfajiri na tumeamka saa moja asubuhi,” alisema.

Mzee Samatta alitoa ahadi kwa mwanaye kuwa akitwaa tuzo hiyo basi watamfanyia sherehe kubwa.

Wazazi hao wameeleza kuwa mtoto wao anapokuwa likizo huwa anapendelea kufanya mambo kadhaa, hasa usafi wa nyumba, kuangalia televisheni, kucheza game, kusikiliza redio pamoja na kuchati.

Wazazi wake walisema Samatta alikuwa anamiliki nyumba saba, lakini moja ambayo ipo Saku, Maji Matitu ameibomoa na ana mpango wa kujenga msikiti, nyingine iliyokuwa Mbande aliiuza kwa sababu ilijengwa chini ya kiwango hivyo amebaki na nyumba tano.

Mbali na nyumba hizo anamiliki viwanja zaidi ya 10 pamoja na mashamba zaidi ya matatu na magari ya kifahari.


Source:Mwananchi

Udaku Special Blog

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Anastahili sifa kutoka kwa kila mtanzania mpenda soka.Nidhamu,kujituma ndio silaha kubwa ambayo unatakiwa kuwa nayo siku zote za maisha yako.Ulipokewa na wakongo ukiwa mgeni lakini ukaona hao ndio ndugu zako na ukaishi nao vizuri,
    Samata namsifu kwa kuwa anaweza kuiga yaliyo mema na anaweza kuishi na watu.Hajalewa sifa japokuwa mafanikio kaanza muda mrefu.
    Wengine igeni mfano.Niyonzima atafakari na kuiga hii ya Samata,nae alipokewa kama mfalme lakini kashalewa sifa,kila siku yeye ni wa kukosea,na si kwamba hawezi kujirekebisha bali ni makusudi kwamba aone watamfanya nini,lol!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad