Mbunge Chadema Achaniwa Suti Mbili na Polisi

DODOMA: KALI ya mwaka. Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijuakali wa Chadema, amechaniwa suti mbili katika matukio mawili tofauti na Jeshi la Polisi ndani ya wiki moja, Risasi Jumamosi linakutaarifu.

Katika tukio la kwanza, mbunge huyo alitolewa nje kwa nguvu kutoka Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, baada ya kukaidi agizo la mwenyekiti wa kikao, Yahaya Nania la kumtaka asishiriki katika zoezi la kuapishwa kwa madiwani wateule na kumchagua mwenyekiti na makamu wa halmashauri hiyo kwa kili kilichodaiwa kuwa hakuwa mjumbe halali wa baraza hilo.

Katika purukushani hizo, zilizotokea Januari 24 mwaka huu, ambazo yeye aligoma kutoka akidai ni mwakilishi halali wa wananchi wa jimbo lake, mbunge huyo alichaniwa suti yake katika vuta nikuvute ya polisi.

Katika tukio la pili, Januari 27, mwaka huu, lililosababisha suti yake nyingine kuchanwa na polisi, Lijualikali alikuwa mmoja wa wabunge wa upinzani waliotolewa nje kwa nguvu, baada ya kukaidi amri wa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ya kukaa chini na kutulia.

Wabunge hao walichukuliwa hatua hiyo baada ya kupinga kujadiliwa kwa hotuba ya rais, aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge Novemba mwaka jana, wakitaka kwanza kupata ufafanuzi wa serikali kwa kitendo chake cha kulizuia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kurusha vipindi vyote vya vikao vya Bunge moja kwa moja (live).

Kana kwamba haitoshi, wabunge wa upinzani kwa mara nyingine walitoka nje ya Bunge katika kikao chake cha asubuhi, Alhamisi iliyopita baada ya Naibu Spika, Tulia Akson kukataa kusikiliza mwongozo uliokuwa ukiombwa na wapinzani, baada ya Naibu huyo kuzuia kujibiwa kwa swali la mmoja wao kuhusu elimu ya bure.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad