ABIRIA 269 waliokuwa wakisafiri kutoka Mwanza kuelekea wilayani Bukoba, wamenusurika kufa baada ya meli ya Mv Serengeti waliokuwa wakisafiria kupata hitilafu ya injini katika ziwa Victoria.
Meli ya Mv Serengeti ambayo muda sio mrefu ilitoka katika matengenezo, katikati ya mwaka jana ilipata hitilafu kama hiyo ikiwa ziwa Victoria na abiria kitendo ambacho kinaelezwa kuwapa wasiwasi watumiaji wa chombo hicho.
Meli hiyo iliyokuwa na abiria 269, tani 64 za mizigo pamoja na gari ndogo, ilipata hitilafu kwenye mfumo wa shafti na majembe ya upande wa kulia (Starboard side) ambayo yalisababisha meli hiyo kuchelewa kutia nanga katika Bandari ya Bukoba.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimu Meneja wa Kampuni ya Usafirishaji Majini, Kapteni Winton Mwassa, amesema meli hiyo iliondoka juzi kutoka Mwanza saa 12 : 40 jioni na kutia nanga jana saa 6: 05 mchana na kwamba ilipata hitalafu majira ya saa 6:20 usiku.
Amesema kuwa mpaka sasa chanzo cha meli hiyo kuchelewa kutia nanga bado hakijafahamika na kwamba walipata taarifa kutoka kwa Nahodha wa Meli hiyo, Bembele Ng’wita kwamba mfumo wa shafti na majembe ya kulia ya upande wa kulia yamepata hitilafu.
“Kwa mujibu wa taarifa ni kwamba saa 6:20 usiku mfumo huo ulipata hitilafu iliyopelekea injini kuwa nzito na kusababisha meli kutetemeka na joto la injini kupanda na kupelekea injini hiyo kuzimwa kwa usalama zaidi,” amesema Mwassa.
Hata hivyo amesema baada ya hali hiyo meli iliiendelea na safari yake kwa kutumia injini moja na kwamba imewasili salama katika Bandari ya Bukoba saa 6: 05, abiria wote na mali zao wapo salama.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo, kampuni imemtuma mpiga mbizi (Diver) kwa usafiri wa ndege ili akakague mfumo huo na kuweza kubaini tatizo na chanzo cha kusababisha hitilafu hiyo na kwamba kwa mujibu wa Nahodha huenda meli ilinasa katika nyavu za wavuvi.
Mwassa aliwataka watanzania kutokuwa na wasiwasi na usafiri huo na kuwataka kuondoa zana potofu kwamba watumishi wa meli hiyo wanauhujumu usafiri wa meli zinazomilikiwa na Serikali kitendo ambacho alikikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo hakupatikana ofisini kwake na kwamba yupo nje ya ofisi.
Meli ya MV Serengeti Majanga Matupu....Abiria 269 Wanusurika Kifo Ziwa Victoria...
0
January 06, 2016
Tags