Benard Membe |
Membe alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika mapema wiki hii kuhusu, mambo mbalimbali yanayoendelea tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.
Mwanadiplomasia huyo alisema hatua ambazo Rais Magufuli amekuwa akichukua kuwabana wakwepa kodi ni za msingi, lakini lazima alifanye kwa uangalifu mkubwa ili asiwafukuze wawekezaji ambao kimsingi ndiyo wabia wa maendeleo ya taifa.
“Wafanyabiashara ni watu wa ‘kuwahandle’ vizuri na kwa uangalifu mkubwa kwa sababu wao ndiyo gurudumu la maendeleo ya nchi yoyote duniani,” alisema Membe.
“Tunapozungumzia ajira, tunazungumzia wafanyabiashara ambao ndiyo wawekezaji. Sasa ombi langu ni kwamba Serikali isicheze nao.”
Akitumia ishara ya mkono wake wa kulia, Membe alisema: “(Mfanyabiashara) Ni kama ndege ambaye ili uendelee kuwa naye, ni lazima umshikilie hivi, lakini ukiachia vidole ataruka na kwenda kutaga mahali kwingine.”