Mzimu wa Dr Slaa Waitikisa Tena Chadema...Mambo Mazito Yaelezwa

Wakati baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakihitimisha jana vikao maalum vya kila mwaka kujadili yale waliyofanya katika mwaka, imefahamika kuwa sifa walau tisa anazotakiwa kuwa nazo mrithi wa Dk. Willibrod Slaa, kwa nafasi ya ukatibu mkuu ni miongoni mwa mambo mazito yanayopasua vichwa vya baadhi ya wengi ndani ya chama hicho.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema jana, ilieleza kuwa viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, walikuwa wakiendelea na vikao vyao mjini Moshi, Kilimanjaro hadi jana jioni kwa ajili ya tathmini kuhusu mwaka uliopita na ushiriki wao katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kuangalia mambo gani ya kufanya katika kipindi cha kuanzia sasa hadi uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020Kadhalika, ajenda kuhusu jina la katibu mkuu ilipata nafasi huku jina la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, liking’ara kwa kupendekezwa na wengi ili lipelekwe kwenye vikao vya juu vya uamuzi. 

Sumaye alijiunga rasmi Chadema hivi karibuni akitokea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako jina lake liliondolewa wakati wa mchakato wa kuwania urais ndani ya chama hicho tawala. 
Jitihada za mwandishi kumpata Mbowe jana kuelezea yanayojiri kwenye kikao chao, ikiwamo harakati za uteuzi wa jina la katibu mkuu, zilishindikana kwani hadi jioni, bado kikao chao kilikuwa kikiendelea huku ikielezwa kuwa simu za viongozi wote wa juu (akiwamo yeye) ziliwekwa mbali na wajumbe hao.

“Ni vigumu kumpata Mbowe wala viongozi wengine wa juu kwa sasa kwa sababu wamejifungia kwa ajili ya kikao na simu zao ziko mbali na wao… ila kwa ufupi, jina la Sumaye bado linatawala katika mjadala kuhusu katibu mkuu wa chama,” mmoja wa viongozi wa Chadema alimweleza mwandishi jana kwa sharti la kutoandikwa jina.
Kabla ya kikao cha jana kilichotarajiwa kuhitimisha mfululizo wa vikao vilivyoanza wiki iliyopita, ilielezwa kuwa ajenda kubwa ni tathmini ya mwaka uliopita na pia kujadili watakayofanya mwaka huu.

“Vikao hivyo vinaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa mpango kazi wa mwaka 2010-2015 na kupanga kwa ajili ya 2016-2020 kabla ya kuwasilisha kwenye vikao vya uamuzi kwa mwaka huu, ambavyo vitafanyika kwa mujibu wa utaratibu wa kikatiba,” ilisema sehemu ya taarifa ya Chadema kwa umma kuhusiana na vikao hivyo mjini Moshi.
Wakati mfululizo wa vikao hivyo ukifikia tamati jana, imefahamika kuwa harakati za kumpata mtu mwenye sifa za kuwa katibu mkuu wa chama hicho kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Slaa bado ni kitendawili.
Chanzo kutoka ndani ya Chadema kiliiambia Nipashe kuwa uteuzi wa jina la mtu atakayerithi mikoba ya ukatibu mkuu uliokuwa ukishikiliwa na Slaa, unavuta hisia za wengi kwa kuwa ni nafasi muhimu kwa mustakabali wa chama na kwamba jambo hilo limeongezeka umuhimu sasa kutokana na ukweli kuwa chama kimekuwa kikubwa zaidi na kuungwa mkono na mamilioni ya Watanzania. 
Katika uchaguzi mkuu uliopita, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, aliyekuwa akiungwa mkono pia na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 39.97 ya kura zote halali zilizopigwa huku Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiibuka mshindi kwa kupata asilimia 58.46.

“Sumaye amekuwa akitajwa sana. Lakini kwa ufupi ni kwamba jina la mrithi wa Slaa (Katibu Mkuu) linasubiriwa kwa hamu kubwa. Hii ni nafasi nyeti kwa chama kikubwa kama Chadema, hivyo haishangazi kusikia wengi wakifuatilia ili kujua ni nani atakayekuwa na sifa za kukamata usukani huo,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.

Dk. Slaa aliitumikia Chadema katika nafasi ya ukatibu mkuu kuanzia mwaka 2002 hadi Julai, mwaka jana, wakati uongozi wa juu wa chama hicho uliporidhia kuwa apumzishwe na kisha yeye mwenyewe kutangaza baadaye kuwa amejiuzulu na kustaafu siasa, akipinga uteuzi wa Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho.

Tangu Slaa alipokosekana katika nafasi hiyo, Chadema bado haijatangaza mrithi wake na nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu.
“Hakuna sababu ya kujaza nafasi hiyo (katibu mkuu) haraka… ni lazima uongozi wa juu uwe makini zaidi kwa sababu chama ni kikubwa hivyo changamoto zake ni kubwa pia. Mtu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo ni lazima achunguzwe kwa undani ili kujiridhisha kuwa kweli ana sifa zinazostahili,” chanzo kingine kilisema.
SIFA NANE MUHIMWakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema walitaja sifa takribani nane kuwa ni sehemu ya zile anazopaswa kuwa nazo mwanachama yeyote atakayekuwa katibu mkuu wa chama hicho na kukiwezesha kupiga hatua zaidi katika kipindi hiki chenye ushindani mkubwa wa kisiasa.
Baadhi ya wale walizoungumza na Nipashe na kutaja sifa hizo , kwa mtazamo wao, na ambazo jumla yake ni nane, ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Mwesige Baregu; Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Arumeru, Samweli Nnko na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Vincent Nyerere.
“Chama kina taratibu zake, miongozo yake, kanuni, katiba na sifa…mambo hayo ndiyo hufuatwa katika kumpata kiongozi wa nafasi hiyo (katibu mkuu), “ alisema Prof. Baregu kabla ya kutaja sifa anazoona kuwa zinafaa kuangaliwa kwa mtu anayeshika nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Baregu, sifa mojawapo ni kwa mtu huyo kuwa na uelewa mpana si tu wa mambo ya Chadema, bali na vyama vingine vya siasa nchini. Awe mzoefu wa kutosha kwenye uwanja wa siasa na pia awe mvumilivu kwa kuwa madongo ya kiasiasa yanayotupwa mengi huelekezwa kwa Katibu Mkuu.
Baregu alisema kuwa pili, awe mzuri katika kushirikiana na wengine kwa kuwa anaweza kuwa Katibu Mkuu anayejiamulia mambo peke yake bila kuwashirikisha wengine na hilo halipaswi kutokea kwa sababu mawazo ya wengine yanaweza kuwa mazuri katika kukisaidia chama.
Sifa ya tatu ina uhusiano na ya pili. Kwamba, katibu mkuu ajaye wa Chadema ni lazima awe msikivu na hapaswi kuwa mbishi au anayefikiria anayoamini yeye ndiyo sahihi na si ya wengine. Ni lazima awe na uwezo wa kusikiliza wengine kwani ni kawaida ndani ya vyama kuwa na malumbano na tofauti za hapa na pale, matukio ambayo baadhi ya watu huyatafsiri tofauti na yeye (katibu mkuu) awe wazi kupokea maoni ya watu tofauti na kuyapa nafasi.

Nne, katibu mkuu ajaye Chadema awe na uwezo wa kuunganisha watu wote ndani ya chama kwa kuhakikisha kuwa wanaweka kando tofauti zao kwa maslahi ya chama.
Sifa ya tano kwa katibu mkuu ajaye ni kwamba, awe mtu asiyehodhi mawasiliano bali kueneza. Katibu mkuu ajaye aeneze habari na uelewa ndani ya chama.Sifa nyingine muhimu (ya sita) ni kuwa muumini wa kuzingatia weledi na kutenda haki. Kwamba, maamuzi yanayofanywa na kamati anazosimamia yafanywe kwa weledi na kutoa haki kwa kila upande
Nnko kwa upande wake, anataja sifa nyingine anayoamini kuwa ya lazima kwa katibu mkuu ajaye ni uzoefu wa siasa utakaomwezesha kukuza shughuli za chama
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ajiunge na CCM
    Fyuuuuuuu
    Magufuli bado ana nafasi za ubunge

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad