Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amewavisha kitanzi watendaji wa elimu walioamua mambo mbalimbali kwa shinikizo la kisiasa, kwa kuwapa muda wa kuyapitia upya ili kuyarekebisha yafuate weledi na taaluma.
Tangu mwaka 2013, wadau wa elimu wamekuwa wakilalamikia masuala ya kisiasa kuingizwa katika elimu na kusababisha kushushwa kwa viwango vya ufaulu na kuanzishwa kwa shule na vyuo visivyo na sifa.
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Prof. Ndalichako alisema taasisi zote zimeanzishwa kwa sheria na hakuna mahali popote panapowataka viongozi wake kutumia maoni ya wanasiasa kufanya uamuzi.
“Taasisi zote zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Sitaruhusu siasa iingie kwenye taaluma kwa namna yoyote ile na kwa nafasi yangu kama wazirimkazi yangu si kutoa maagizo fanya hivi, anya vile’.
“Naamini hizi taasisi zina wataalamu wenye weledi, kazi yao ni kufanya vitu vyenye masilahi kwa taifa. Labda niseme kwa nafasi yangu sitaruhusu mtu afanye uamuzi kwa msukumo wa kisiasa, kwanza siasa anaipata kwa nani?
“Wakati mwingine tunasingizia kuwa watu wanatuingiia. Atakuingilia vipi wakati wewe ndiwe una utalamu na isitoshe hizi taasisi zote zimeanzishwa kwa sheria na zina taratibu zinazoziongoza kufanya uamuzi. Hakuna sehemu inasema uchukue maoni ya wanasiasa kufanya uamuzi wako.
“Lakini kama mtu ameamua kufuata siasa ni hiari yake. Sheria inataka weledi ufuatwe na siasa kwenye elimu haiwezi kuwa na nafasi. Kama changamoto zipo, zije tuzifanyie kazi, tusikimbie tatizo kwa sababu itakuwa haisaidii.
“Mimi nawapa changamoto wenyewe (watendaji wa elimu), kama walikuwa wamefanya uamuzi kwa shinikizo la kisiasa, sasa warudi waangalie weledi, wajitathimini na kuangalia taaluma zao. Kama ni madaktari waangalie ili mtu awe daktari viwango vyake ni vipi, mainjinia (wahandisi) bora wanatakiwa waweje na vitu kama hivyo.
“Nataka kuwarudishia wao wenyewe na nimewaambia wajitizame upya. Hata TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) niliwaambia waangalie upya vigezo vyao. Sasa kama kulikuwa na siasa nimewapa fursa ya kujirekebisha,” alisema Prof. Ndalichako.
Aliongeza kwamba: “Nimeaambia tukisema ni hapa wote tusimame hapa hakuna kuyumba na tutaelimisha Watanzania kwa nini tunafanya hivyo na najua tutakuwa na vigezo vinavyoeleweka.”
Aliwataka wananchi pia kutoingilia mambo yanayohusu taaluma zingine kwa kuwa kwa baadhi ya maeneo, kelele zao zinafanya baadhi ya wataalamu kufanya uamuzi usio sahihi.
MADARAJA YA UFAULU
Kuhusu madaraja na uhalali wake, Prof. Ndalichako alisema maelezo yaliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk, Charles Msonde), alipotembelea wiki iliyopita hakuyaelewa na kuona si lazima mtu aseme mezani kila kitu.
“Watakapoleta maelezo yao Alhamisi (keshikutwa) ndipo nitaona kama ni kitu kizuri au kibaya na kama unaona pale niliwataka wasitetereke kwenye utendaji.
“Tukipata sababu zao tutaangalia kulingana na sababu zilizotolewa nini kitafanyanyika. Mpaka sasa hatujajua, maelezo yao ndiyo yatatuambia,” alisema.
Mbali na mambo hayo, alisema licha upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa kuangalia wastani wa alama (GPA), ambao wananchi wanaulalamikia, Necta imefanya vizuri kwenye maeneo mengi ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utungaji mitihani, kuboresha mifumo ya utendaji kazi ya kielektroniki na kuanza kutoa vyeti mbadala kwa wahitimu ambao vyeti vyao vina picha pale vinavyopotea.
“Na kwa wale vyeti visivyokuwa na picha, bado wameendelea kutotoa vyeti mbadala. Badala yake wanatoa ‘statement of results’ (karatasi maalumu ya matokeo) kwa sababu kwenye mambo ya vyeti kuna ‘umafia’ sana. Watu wanabadilishana vyeti na mambo kibao yapo huku,” alisema.
VURUMAI KWENYE ELIMU
Vurumai kwenye mfumo wa elimu ilianza baada ya matokeo ya kitado cha nne ya mwaka 2012 kufutwa kutokana na ripoti ya Tume ya Profesa Sifuni Mchome, ambaye baada ya ripoti yake, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya kabla ya kuhamishwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Sheria na Katiba, baada ya kumteua Prof. Ndalichako kuongoza wizara hiyo.
Matokeo ya awali mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2012, yalionyesha kuwa watahiniwa waliopata kati ya daraja kwanza mpaka la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4, daraja la nne watahiniwa 103,327 (asilimia 28.1) huku waliopata sifuri wakiwa 240,909 (asilimia 65.5).
Baada ya ripoti ya Prof Mchome kutaka matokeo hayo yafutwe na kupangwa upya, waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 35,349 (asilimia 9.54), daraja la nne 124,260 (asilimia 33.54) na waliopata sifuri wakawa 210,846 sawa na asilimia 56.92.
Wizara pia ilibadilisha utunuku wa ufaulu na kuanza kutumia GPA, badala ya jumla ya alama (division) iliyokuwa imezoeleka.
Mbali na uamuzi huo, wizara pia ilishusha alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita ambapo sasa A inaanzia 75 hadi 100, B+ (60 hadi 74) B (50 hadi 59), C (40 hadi 49), D (30-hadi 39), E (20 hadi 29) na F ni kuanzia 0 mpaka 19.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali kwa kidato cha nne ni A (80 hadi 100), B (65 hadi 79) C (50 hadi 64), D (39 hadi 49) na F kutoka 0 hadi 34 huku kidato cha sita ikiwa A (80 hadi 100), B (75 hadi 79), C (65 hadi 74), D (55 hadi 64) E (45 hadi 54), S (40 hado 44) na F kutoka 0 hadi 39.
KUONDOA 0 KUJA NA DIVISION V
Mwaka 2013, serikali ilitangaza kuwa kiwango cha pointi za kupanga madaraja kimebadilika na kwamba daraja la kwanza litaanzia pointi 7 hadi 17, daraja la pili (18 hadi 24), daraja la tatu (25 hadi 31), daraja la nne (32 hadi 47 na daraja tano (48 hadi 49).
Madaraja ya miaka ya nyuma yalikuwa pointi saba hadi 17 kwa daraja la kwanza, 18 hadi 21 daraja la pili, 22 hadi 25 daraja la tatu, 26 hadi 33 daraja la nne na 34 hadi 35 daraja la sifuri.
Sambamba na mfumo huo, serikali ilifuta mfumo wa zamani wa utunuku wa matokeo ambao ulikuwa wa jumla ya pointi (division) na kuleta wa wastani (GPA).
UHALISIA
Wakati serikali ikitumia nguvu nyingi kuficha uhalisia, matokeo ya mwaka 2012 yalikuwa hayana tofauti sana na yale ya mwaka 2011 ambapo asilimia 90 ya wanafunzi wa walipata madaraja ya nne na sifuri.
Pia kwa mwaka 2012, asilimia 93.6 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo, walipata madaraja ya nne na sifuri.
“Niikukumbushe serikali kwamba Baraza la Mitihani lilibadilisha pia viwango vya ufaulu kwa kidato cha sita ambapo sasa kiwango cha chini cha ufaulu ni alama 40 hadi 44.
“Ni vizuri sasa serikali isisubiri matokeo yatoke ndipo ishtuke. Nashauri iwaamuru Necta watumie kiwango cha zamani cha ufaulu ili kuepuka usumbufu kama ulivyojitokeza kwa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012,” alisema Prof. Ndalichako.
Tanzania ilijiwekea historia
Kutokana na uamuzi ambao wadau wa elimu wanaamini ni wa kisiasa wa kushusha alama za ufaulu, Tanzania ilijiweka kwenye nchi zenyewe viwango vya chini zaidi duniani vya ufaulu.
Kabla ya kufutwa kwa matokeo ya mwaka 2012 na serikali kuja na kushusha alama za ufaulu, ilikuwa mwanafunzi akiopata 34 kushuka chini, inahesabika amefeli.
Kiwango hicho bado kilikuwa cha chini kulinganisha na mataifa mengine duniani ambayo mwanafunzi akipata alama 40 kushuka chini, anahesabika amefeli.
Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Sudan, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Gambia, Liberia, Sierra Leone na Uganda.
“Kwa hiyo utaona kwamba ni sisi peke yetu katika ukanda huu wa Afrika tuliokuwa tunatumia kiwango cha ufaulu cha alama 21, ambacho kwa kweli ni kidogo mno na ni udanganyifu ukilinganisha na nchi zingine za Afrika tunazofanana nazo,” alisema.