Serikali Yaamuru Waliovamia na Kujigawia Maeneo Shamba la Sumaye Waondoke

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki amewataka waliovamia na kujigawia maeneo ya watu wengine likiwamo la Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Ritha Mlaki waondoke mara moja kwa kuwa wamevunja sheria.

Alisema zaidi ya watu 2,000 wakiwamo waliobomolewa nyumba katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam wamevamia na kujigawia mashamba hayo yaliyopo Tegeta na Goba kinyume cha sheria.

“Kisa wamevunjiwa nyumba zao walizojenga kinyume cha sheria ndiyo wameamua kuvamia maeneo yasiyo yao, hili ni kosa kama makosa mengine, nawataka waondoke haraka vinginevyo tutawachukulia hatua kali za kisheria,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Alisisitiza kuwa agizo la Rais John Magufuli lilikuwa ni maeneo yaliyoachwa wazi kuainishwa kwa ajili ya kupangiwa matumizi mengine na siyo kuruhusu watu kuvamia bila taratibu.

Sadiki alisema hakuna viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi waliokumbwa na bomoabomoa katika maeneo ya mabondeni.

Zaidi ya nyumba 8,000 zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, fukwe za bahari na kando ya mito zimeanza kubomolewa kabla ya kusitishwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sadiki alisema wananchi waliobomolewa nyumba zao na ambao watakumbwa na operesheni hiyo wasitarajie kupatiwa viwanja vya kujenga nyumba zao.

Bomoabomoa hiyo inaendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ikiwalenga waliojenga kinyume cha sheria.

“Serikali haina viwanja vinavyotosha kuzigawia familia zaidi ya 8,000 zitakazobomolewa, niwashauri tu wasiendelee kupoteza muda wao kwa kuwasikiliza wanasiasa, watafute makazi mengine waende. Kama walivyovamia na kujenga ndivyo wanatakiwa kutafuta maeneo mengine wahamie,” alisema Sadick.

Alisema viwanja 1,007 vya Mabwepande vilitolewa kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko mwaka 2011 ambao waliwekwa kwenye kambi baada ya kukosa makazi,lakini cha kushangaza baadhi  yao waliviuza viwanja hivyo kwa bei ya chini na kurudi tena kwenye maeneo hatarishi.

Alisema kaya zote zilizokosa makazi kutokana na mafuriko hayo zilipatiwa maeneo. Waathirika 580 walitokea Ilala, Kinondoni 349 na Temeke 81.

“Kuna upotoshaji unaendelea kwamba yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuwapatia wanaobomolewa sasa, jambo hili halina ukweli, ikumbukwe tuligawa viwanja vya Mabwepande baada ya Rais (Jakaya Kikwete) kuagiza tufanye hivyo ili kuwasaidia wale tu, waliokumbwa na mafuriko mwaka 2011,” alisema.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. kama walipewa wakauza waendelee kuisoma namba kama walivyokuwa wanaimba kipindi cha kampeni ni ile ile ileeee. mtakoma kuringa na kura mliwapigia na mliwapenda wenyeweeee, chaguo lenu wenyeweeee.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad