TRA Yavuka Lengo .......Yakusanya Trilioni 1.4 Kwa Mwezi

Jumla ya shilingi trilioni 1.4 imekusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha mwezi Desemba mwaka uliopita wa 2015.

Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la wastani wa shilingi  bilioni 490 kwa mwezi ukulinganisha na wastani wa makusanyo ya kuanzia Julai hadi Novemba ambapo ,TRA ilikuwa inakusanya wastani wa shilingi bilioni 900 kwa mwezi.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Kamishna Mamlaka ya Mapato  Tanzania (TRA) Alphayo Kidata wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kutoa taarifa kwa umma juu ya ukusanyaji wa kodi nchini.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi kufikia Desemba mwaka huo TRA ilikuwa imekusanya wastani wa shilingi trilioni 6.4 ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya trilioni 6.5 katika kipindi hicho.

Kaimu Kamishna huyo ametaja sababu za kuongeza kwa makusanyo ya kodi kuwa ni pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuweka mifumo mizuri ya ufuatiliaji ili kumrahisishia mlipa kodi kulipa kodi anayostahili bila usumbufu.

Kidata amesema kuwa katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya tano ya kuongeza mapato Mamlaka hiyo itasimamia kwa ukaribu ukusanyaji wa mapato na kuwabana wote wenye nia ya kukwepa na hatimaye kuwafikisha katika vyombo vya sheria watakaobainika wamekwepa kodi.

Katika hatua nyingine Kaimu Kamishina Mkuu wa TRA huyo amesema jumla ya shillingi billioni 11.8n zimekusanywa kutoka kwa wafanyabiashara walioondosha makasha katika Bandari Kavu kinyume na taratibu za forodha.

Amesema kuwa makusanyo hayo yanajumuisha shilingi bilioni 5.3 kuoka kwa Kampuni na wafanyabiashara 19 ambao wamemaliza kulipa kodi za makasha yao na wengine 19 ambao wamelipa sehemu ya kodi ya makasha yao

Na Raymond Mushumbusi-MAELEZO
Dar es Salaam
6.1.2016
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad