TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa na upotoshwaji kuhusu zoezi la ufuatiliaji wa matumizi ya misamaha ya kodi inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa wafanyabiashara, wawekezaji, Taasisi za Dini na Taasisi zisizo za kiserikali kwa maelezo kwamba TRA inazilenga baadhi ya Taasisi.Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania inaipa Mamlaka ya kusimamia, kukagua na kuhakiki mapato ya Serikali pamoja na kuzuia ukwepaji wa kodi wa aina yoyote ile ikiwemo matumizi mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa mujibu wa Sheria.
Kifungu cha 5 (3) cha Sheria ya TRA kinatoa mamlaka kwa TRA kufanya jambo lolote lenye tija na manufaa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kisheria.
Kwa vile misamaha ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamiwa na TRA, ni wajibu wa Mamlaka kuhakiki kama bidhaa au huduma zilizosamehewa zinatumiwa na watu au Taasisi zinazostahiki misamaha hiyo au kwa miradi iliyokusudiwa.
Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za upotoshaji kwamba TRA imeilenga Taasisi moja ya kidini kwa kuiandikia barua ya kuomba vielelezo na ufafanuzi juu ya misamaha ya magari iliyopewa awali na kuonekana kana kwamba ni utaratibu mpya wa utoaji wa misamaha.
Tungependa kufafanua kwamba TRA haibagui wala kulenga Taasisi yoyote bali inatekeleza wajibu wake wa kufuatilia misamaha iliyotolewa
Katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2015 TRA iliwaandikia walipakodi 65 kupata vielelezo juu ya matumizi ya misamaha ya kodi walioipata na katika hao zimo Taasisi za kidini 39.
Ukaguzi huu huisadia TRA kupata taarifa muhimu ili kuishauri Serikali namna bora ya kutoa misamaha kwa ajili ya kuleta tija na ufanisi uliokusudiwa ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii na kupunguza umaskini.
Aidha taarifa za misamaha ya kodi zinaisadia TRA kubaini matumizi bora ya misamaha pamoja na mianya ya upotevu wa mapato kupitia misamaha hiyo ili TRA ichukue hatua zinazostahili pale inapobainika kuwa kuna ukwepaji na kuziba mianya hiyo.
Zoezi hili ni endelevu hivyo tunaziomba Taasisi zote za kidini na mashirika yote yanayonufaika na misamaha ya kodi kuchukulia zoezi la ukaguzi wa misamaha hiyo kuwa ni utekelezaji wa sheria na wahusika wote watoe ushirikiano kwa TRA pale wanapohitajika ili zoezi hilo lifanyike kwa ufasaha na kwa manufaa kwa wote.
"Pamoja Tunajenga Taifa Letu"
A. J. Kidata
KAIMU KAMISHNA MKUU.