Serikali imesema itahakikisha makaa ya mawe yanakua chanzo kingine kikubwa cha uzalishaji wa umeme nchini ili kupunguza gharama za umeme zilizopo hivi sasa.
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ameyasema hayo alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na kuongeza kuwa serikali itahakikisha inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na mgodi huo ili kuimarisha uchumi wa taifa kupitia makaa ya mawe.
“Nimeelezwa makaa ya Ngaka yana ubora na kiwango cha hali ya juu na nimeelezwa kwamba kuna baadhi ya viwanda vimeingia mkataba na Ngaka lakini badala yake wananunua makaa kutoka nje. Hilo halikubaliki ikiwa makaa ya ndani ya nchi yana ubora lazima tutumie bidhaa za nyumbani,”amesisitiza Prof. Muhongo.
Kutokana na malalamiko ya Mgodi kuhusu hali ya Mkataba ya kuuziana makaa kutoafikiana, Waziri Muhongo ameutaka mgodi huo,Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),EWURA, Kampuni za Saruji za Dangote, Tanga Cement na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kukutana Makao Makuu ya Wizara tarehe 14 Januari,2016, ili kujadili kuhusu suala hilo na pia kujadiliana juu ya gharama za kuuziana umeme na TANESCO pindi mgodi huo utakapoanza kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Masoko wa mgodi wa Ngaka, Christopher Temba, mgodi huo unazalisha tani za makaa ya mawe laki tano kwa mwaka na tayari makaa hayo yanasafirishwa katika nchi za Kenya, Zambia, Malawi na vilevile katika viwanda kadhaa hapa nchini vikiwemo vya Saruji, Mohamed Enterprises na viwanda vingine.