WATU 24 wameuawa na wengine kujeruhiwa kwenye mgahawa mmoja mjini Baidoa, Kusini mwa Somalia wakati wakitazama mechi ya soka baina ya Manchester United na Arsenal baada ya shambulizi lililotekelezwa na Al-Shabab jana jioni.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa milipuko miwili mikubwa ilitokea, katika mgahawa huo uliokuwa umejaa mashabiki wa mechi kati ya Manchester United na Arsenal.
Miongoni mwa wale waliouawa ni pamoja na afisa wa serikali ya jiji hilo.
Mji wa Baidoa ulitekwa na wapiganaji wa Kiislamu wa Al-Shabaab mwaka wa 2008, lakini walitimuliwa mwaka 2012.
Mji huo ulioko takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu Mogadishu ni mji wa hivi punde zaidi kushambuliwa na wanamgambo hao wa kiislamu.
Shambulizi la kwanza lilitokea katika mgahawa maarufu unaopendwa na wageni na viongozi wa kisiasa ambao ulishambuliwa kwa gari lililokuwa limetegwa bomu.
Walionusurika waliokolewa na wanajeshi wa muungano wa Afrika AMISOM.
Shambulizi hili limetokea muda mchache tu baada ya kukamilika kwa warsha ya viongozi wa mataifa yanayochangia wanajeshi wake katika jeshi la muungano wa Afrika AMISOM.
Siku ya Ijumaa watu wengine zaidi ya 20 waliuawa katika mgahawa mwengine kufuatia shambulizi la Al Shabaab.