Mkuu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo jana, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alielezea kushangazwa kwake na kile alichokiita “jeshi kuingizwa ndani ya Ukumbi wa Bunge la Jamhuri mjini Dodoma”.
Alisema hayo mjini hapa alipokuwa akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuingizwa kazini kushika wadhifa huo atakaoutumikia kwa miaka minne.
Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, anachukua nafasi ya Askofu Dk Alex Malasusa ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.
Hafla hiyo ambayo Majaliwa alikuwa mgeni rasmi, ilihudhuriwa pia na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na maaskofu zaidi ya 28.
Akizungumza kwa hisia, Askofu Dk Shoo alionekana kuguswa na mambo matano yaliyojitokeza katika Taifa.
Polisi bungeni
Alieleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa Bunge, akisisitiza kuwa ni lazima mihimili mitatu ya dola ijiendeshe kwa uhuru.
“Iachiwe ifanye kazi yake kwa uhuru na kila mhimili utunze heshima hiyo. Tunasikitishwa sana na hali inayoendelea katika Bunge letu na nashukuru nimewaona baadhi ya wabunge humu,” alisema.
Wabunge waliokuwapo ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema Anthony Komu wa Moshi Vijijini, James Mbatia wa Vunjo na Lazaro Nyalandu wa Singida Kaskazini.
“Hili ni lenu na Spika wenu (akiwageukia wabunge). Bunge ndiyo nyumba ya demokrasia kama kweli Tanzania tunataka kujenga jamii ya kweli ya inayoheshimu misingi ya kidemokrasia. Sisi tunatarajia kuona na kusikia hoja zikijadiliwa kwa uwazi na katika hali ya kistaarabu. Kwa kuchezeachezea heshima hii ya Bunge sasa tunaona juzijuzi tu jeshi linaingia bungeni. Nyumba ya demokrasia haiingizwi majeshi. Kwa hiyo wabunge tunzeni heshima yenu,” alisema na waumini wa kanisa hilo kumshangilia.
Utumbuaji majipu
Askofu huyo wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alimpongeza Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Majaliwa na timu yao kwa namna walivyoanza vizuri katika utawala wa awamu ya tano.
“Rais ameshaweka wazi kwa wananchi nia yake ya kufufua uchumi na kupambana na ufisadi. Katika muda mfupi huu wa uongozi wake, mmekwishakuanza (Waziri Mkuu) kutumbua majipu makubwa ya ufisadi,” alisema na kuongeza:
“Tunamwomba sana Rais na timu yake aendelee kutumbua majipu hayo kwa ujasiri mkubwa na miji ya majipu hayo ioshwe na kukamuliwa ili yasirudie.”
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa utumbuaji huo unatakiwa ufanyike kwa hekima na misingi ya uwazi, ili wasio na nia njema wasitumie kuwakomoa wasio na hatia.
“Yale majipu ambayo ni hasa, hayo yasiachwe kutumbuliwa na msiwe na hofu yoyote kutoka kwa watu watakaowapinga, najua kuna watu wanajipanga kuwapinga, msiwe na hofu yoyote,” alisema Askofu Shoo.
Mkwamo Zanzibar
Akizungumzia mkwamo wa kisiasa visiwani baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi na kutangaza tarehe ya kuurudia, Askofu Shoo alisema yanayoendelea huko yanalitia doa Taifa.
“Tunamuomba pia Mungu awape hekima na ujasiri wa kushughulikia suala la Zanzibar ili maridhiano na haki itendeke na nchi yetu iendelee kuwa na utulivu na amani. Mambo yanayoendelea kule Zanzibar yasipodhibitiwa vizuri yataweza kutia doa Awamu ya Tano ya uongozi.”
Katiba mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Askofu Shoo alisema hayo ndiyo matarajio makubwa ya Watanzania ambao wanataka kuona Serikali ya Awamu ya Tano ikiwatimizia ndoto hiyo.
“Tunazidi kumuomba Mungu. Matarajio ya Watanzania ni uwapo wa Katiba Mpya inayoheshimu matakwa ya wengi na inayosisitiza utawala wa sheria na haki za kibinadamu,” alisema na kuongeza:
“Ninashauri mchakato wa Katiba Mpya ufikiriwe kwa upya na utumike kama njia ya kuganga madhaifu na majeraha yaliyotokea au ambayo yapo katika awamu zote zilizotangulia.”
Ada elekezi
Akizungumzia ada elekezi kwa shule za binafsi, Askofu Shoo alitaka suala hilo litizamwe upya tena kwa kuwashirikisha wadau wa elimu nchini.
“Nina imani Serikali ikiboresha shule zake hakutakuwa na haja ya kuweka ada elekezi. Tunachohitaji katika ubora wa elimu ni kuanzisha mamlaka inayojitegemea ya ithibati na udhibiti. Kuwa na mamlaka hiyo na ikijitegemea naamini kutaleta mafanikio katika ubora wa elimu.”
Waziri Mkuu
Akihutubia kwa niaba ya Rais, Majaliwa alisema wabunge wanapaswa kuwa kioo cha jamii.
“Ulipozungumzia hili ulizungumzia Bunge na mimi nashukuru umelieleza hilo la wabunge wenzangu. Jambo hilo ni letu, tutahakikisha suala la demokrasia linaimarishwa ndani ya Bunge,” alisema.
“Lakini pia nataka nieleze Bunge ni eneo ambalo linaweza kuijenga jamii hii mpya. Wabunge ni kioo, ni watu wa kuigwa. Hivyo ni vyema tukalitumia Bunge kwa lugha sahihi na tabia nzuri. Tutaendelea kusimamia lugha nzuri ndani ya Bunge ili wanaoona waweze kuiga. Niwahakikishie Watanzania tutaendelea kuzungumza na wabunge ili bungeni pawe mahali panapojenga tabia njema,” alisema.
Kuhusu Katiba Mpya, alisema hoja ya Askofu Shoo ifanyiwe kazi na akadokeza kuwa amekuwa akizungumza na wabunge juu ya suala hilo.
“Suala la ada elekezi kwa shule binafsi litazungumzwa na wadau wote ili kutoa mwelekeo sahihi. Nataka nikuahidi Baba Askofu, tutaziboresha shule zote za umma ili ziweze kutoa elimu bora,” alisema.
Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Issac Aman alisema kama kuna jipu linalopaswa kutumbuliwa, basi ni la Watanzania kukosa moyo wa uzalendo.
Askofu huyo alisema ufisadi na ubinafsi unaofanywa na baadhi ya Watanzania ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo na uadilifu.
Huyu ni askofu au mwanasiasa?
ReplyDeleteMapolisi wa bongo wote hawana nidhamu kwa ajili ya bangi nyingi
ReplyDeleteaskofu fanya kazi ya Yesu ya nchi magu anatosha,. pia nakuomba ukemee ukabila kaskazini wana chama chao hao.
ReplyDelete