Ikulu Yafafanua Magufuli Kumtuma Samia Mkutano wa Marais wa Afrika.

Rais Dk. John Magufuli ameendelea kukacha safari za nje ya nchi, baada ya jana kumtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kumwakilisha katika Mkutano wa wakuu wa Nchi za Afrika unaojadili masuala ya usalama barani Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, aliieleza Nipashe kuwa  kutumwa kwa Makamu kwa Rais ni sawa na uwapo wa Rais katika mkutano huo.

Alisema Rais anapokuwa hayupo nchini, Makamu wa Rais ndiye anayeongoza nchi na kusema kuwa Rais Magufuli ana miaka mitano ya uongozi mbele, hivyo kuna mikutano mingi atakayotakiwa kuhudhuria.

Alisema serikali inawatendaji wengi, hivyo si kila mkutano Rais anatakiwa kwenda.

“Katika serikali kuna Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mabalozi, hivyo si kila mkutano Rais aende. kuna  watendaji wengi,” alisema Msigwa.

Msigwa alisema itakapotokea Rais Magufuli anasafiri kwenda kuhudhuria mkutano wowote nje ya nchi, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu itatoa taarifa kwa umma.

Akiwa nchini humo katika mkutano huo wa masuala ya usalama barani Afrika, Samia alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Li Yong, na kuzungumzia juu ya kuendeleza ushirikiano kwenye maendeleo ya viwanda utakaotolewa na UNIDO kwa serikali ya Tanzania na kuwa moja ya nchi za viwanda kuanzia mwaka 2015/2020
Tangu aingie madarakani Novem,ba 5, mwaka jana, Rais Magufuli  amekuwa akikacha safari za nje ya nchi kuhudhuria mikutano na badala yake amekuwa akiwatuma viongozi wa kiserikali kumwakilisha.

Mojawapo ya safari ambazo hakwenda ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM), uliofanyika visiwa vya Malta Novemba 27, mwaka jana.

Rais John Pombe Magufuli
Katika mkutano huo, Rais alimtuma aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe, kumwakilisha akiwa pamoja na maofisa wengine watatu.

Pia Novemba 29, mwaka jana, Rais Magufuli alitakiwa kuwapo Paris, Ufaransa, katika mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya tabianchi duniani (COP21) ambao takriban wakuu wa nchi 150 kutoka  nchi 195 walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na Xi Jinping wa China.

Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakwenda Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za Afrika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli alisema safari za nje zimeligharimu taifa Sh. bilioni 356.3, ambazo kati yake Sh. bilioni 183.1 zilikuwa kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh. bilioni 68.6 ziligharamikia mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zilikuwa za posho, ambazo zingeweza kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.

UHUSIANO WA TANZANIA NA AU
Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU).

Miongoni mwa viongozi 30 ambao walikuwa waasisi wa OAU ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Pia katika  bara la Afrika, miongoni mwa nchi zinazoheshimika kutokana na mchango wake katika ukombozi wa bara hilo ni Tanzania kwa kusaidia mataifa mengi kupata uhuru na kujitawala.

Aidha, Nyerere kupitia OAU, alipewa heshima ya pekee na kuenziwa kwa kuamua Jengo la Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo kuitwa Julius Nyerere.

Kadhalika, Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa chini ya OAU, makao makuu yake yalikuwa Dar es Salaam na  Katibu Mtendaji wake alikuwa Brigedia Jenerali Hashim Mbita (sasa marehemu) ambaye alikuwa Mtanzania.

Licha ya rekodi ya Rais Magufuli ya kutosafiri kwenda Ulaya na nchi nyingine za nje ya Tanzania hata mara moja tangu aingie madarakani kuwavutia wengi, baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe wamedai  hatua hiyo ni nzuri.

Mkufunzi wa Chuo cha Mlimani kilichoko Mbezi kwa Musuguri jijini Dar es Salaam, Vedasto Malima, alisema Rais Magufuli anafanya jambo la maana na la kuigwa kwa watendaji wengine.

Alisema Rais Magufuli ameonesha nia na dhati ya kuwasaidia Watanzania kuliko kupenda kusafiri nje ya nchi kama watangulizi wake walivyofanya.

Post a Comment

5 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Waswahili hamna shukrani,huyo magu akianza kupiga misele msianze kulalamika

    ReplyDelete
  2. Mda utafika tu nae ataenda

    ReplyDelete
  3. Magufuli anaogopa sana kupanda Ndege hata siku za kampeni alipanda boat kuelekea Zanzibar.

    ReplyDelete
  4. “Katika serikali kuna Rais, Makamu wa Rais,
    Waziri Mkuu na mabalozi, hivyo si kila mkutano
    Rais aende. kuna watendaji wengi,” alisema
    Msigwa.
    Ni kweli lkn tuangalie na uzito wa huo mkutano wenyewe mikutano yote hio iliyo tajwa ilikua ni nafasi yake mh raisi km ni mkuu wa nchi ahudhurie yeye

    ReplyDelete
  5. ushamba nao ni mzigo

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad