Madudu 14 Yabainika Vitabu vya Darasa la Kwanza...Watendaji Watatu Wasimamishwa Kazi

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebaini kasoro 14 katika uchapaji wa vitabu 2,807,600 vya darasa la kwanza.

Kutokana na ‘madudu’ hayo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maimuna Tarishi jana alitangaza kuwasimamisha kazi watendaji watatu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuhusishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Tarishi alivitaja vitabu hivyo kuwa ni pamoja na cha Najifunza kusoma, kitabu cha kwanza na Najifunza kusoma, kitabu cha pili.

Tarishi alisema kasoro hizo zimesababisha wanafunzi wa darasa la kwanza wa mwaka 2016 kukosa vitabu kwa kuwa haviwezi kutumika.

Waliosimamishwa kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter Bandio, Mwanasheria wa taasisi hiyo, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela.

Kasoro zilizomo

Katika vitabu hivyo imebainika kuna mwingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha ya aina moja kuwa na rangi tofauti katika vitabu, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya vitabu kufungwa kwa pini moja, vingine kukosa pini kabisa na baadhi kufungwa ubavuni.

Kasoro nyingine ni kuchakaa kabla ya matumizi hasa kitabu cha ‘Najifunza kusoma’ kitabu cha pili, mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi, picha na baadhi ya vitabu maandishi kufutika.

“Tumebaini baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo, majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu vimerudufiwa ‘fotokopi’,” alisema.

Alipoulizwa ni vitabu gani vitatumika badala yake, Tarishi alisema vitaendelea kutumika vitabu teule vilivyochapishwa na kampuni binafsi pamoja na vile vya Kiongozi cha Mwalimu.

Alisema Kampuni ya Yukos iliyochapisha vitabu hivyo, pia haikuzingatia vigezo vilivyowekwa, kwa maana nyingine imekiuka makubaliano yaliyo katika mkataba iliyoingia na TET.

Tarish aliitka iondoe vitabu vyote ilivyochapisha kwenye ghala la Serikali ifikapo kesho.

Ilivyotokea

Ili kutekeleza mtalaa mpya wa darasa la kwanza na la pili, Aprili 3 mwaka jana, TET ilitangaza zabuni ya kuchapa vitabu vya kiada vya darasa la kwanza, wachapishaji watatu walishinda zabuni hiyo ambao ni Jamana Printers Limited, Tanzania Printing Services na Yukos Enterprises Ltd.

“Kampuni ya Yukos Enterprises Ltd ilishinda zabuni ya kuchapa vitabu hivyo. Ufuatiliaji uliofanywa na wizara katika bohari ambayo ilikuwa ikipokea vitabu hivyo, ulibaini kuwa vitabu vilivyowasilishwa vilikuwa na kasoro 14,” alisema Tarishi.

Alisema Januari 22, mwaka huu, uongozi wa taasisi ya elimu ulishauriwa usitishe uchapaji wa vitabu uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Yukos ili Serikali isiendelee kupokea vitabu vyenye kasoro.

“Hata hivyo TET haikusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo na badala yake kampuni hiyo ilichapa vitabu vyote ilivyopangiwa,” alisema.

Hasara iliyopatikana

Tarishi alisema, “Serikali haijaingia hasara yoyote kwa sababu aliyepewa zabuni alilipwa asilimia 20 ya zaidi ya Sh2 bilioni na makubaliano yalikuwa kama akishindwa kutimiza masharti ya mkataba, pesa aliyolipwa atairejesha.”


Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. JPJM.. I CAN SEE A NEW LEADERSHIP ERA.. PERFORMANCE DRIVEN and QUALITY CONSCIOUS.. endelea hata ndiyo mabadiliko ya mwelekeo Na. Ukwamuzi..... We learn along the way and paving for next generation.. Hata mwalimu hakuifikia hii... Nakukubabi Na hii speed.. As the ..

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad