Watu tisa wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutungua helikopta iliyokuwa ikifanya doria kwenye Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu, Simiyu na na kumuua rubani wake.
Mbali na kutungua chopa na kumuua rubani wake, Rogers Gower, raia wa Uingereza, watu hao pia wameshtakiwa kwa kukutwa na nyara za Serikali, kuuza na kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Mkoa wa Simiyu jana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku umati wa wananchi wakifurika na kusababisha hekaheka mahakamani hapo.
Yamiko Mlekano, ambaye ni wakili mwandamizi wa Serikali, alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi tatu; uhujumu uchumi, mauaji na umiliki wa silaha bila ya kibali.
Katika kesi namba mbili ya mauaji, Wakili Yamiko alidai kuwa Shija Mjika (38), Njile Gunga (28), Dotto Pangali (42) na Moses Mandagu walitungua helikopta hiyo Januari 29 kwenye Hifadhi ya Mwiba iliyoko Kijiji cha Makao wilayani Meatu na kumuua rubani Gower.
Mlekano alidai kuwa katika kesi ya uhujumu, mshtakiwa namba moja Iddy Mashaka (49) anadaiwa kujihusisha na kuratibu tukio la uhujumu uchumi kinyume na sheria.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, John Nkwabi, wakili huyo alida kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 6 na Februari Mosi wilayani Meatu kwa kumshauri mshtakiwa namba mbili, Shija Mjika (38) kuua wanyama wasioruhusiwa.
Katika shtaka la pili, watu saba; Njile Gunga (28), Dotto Pangali (42), Moses Mandagu (48), Dotto Huya (45), Mwigulu Kanga (40), Mapolu Njige (50) na Mange Barumu (47) pia wanashtakiwa kwa kuhujumu uchumi.
Aliieleza mahakama kuwa kati ya Januari 21 na 29 katika wilayani Meatu, washtakiwa walipanga na kuratibu tukio la kuwinda wanyama aina ya tembo bila ya kibali cha Serikali.
Wakili Mlekano alidai kuwa shtaka la tatu la uwindaji wanyama wasioruhusiwa linawakabili mshtakiwa wa pili hadi tisa na wanadaiwa kutenda Januari 26 na 29 kwenye Hifadhi ya Mwiba Kijiji cha Makao wilayani Meatu wa kumuua tembo mwenye thamani ya Sh32,891,100 bila ya kibali.
Katika shtaka la nne, mshtakiwa namba mbili na tisa wanatuhumiwa kumiliki nyara za Serikali kinyume na sheria.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 29 na Februari Mosi wilayani Meatu ambako walikamatwa na meno ya tembo yenye uzito wa kilo 31 na thamani ya Sh32,891,100.
Katika shtaka namba tano, Mashaka na Mjika wanashtakiwa kwa kuuzaji nyara za Serikali kinyume na sheria na kwamba walitenda kosa hilo kati ya Januari 6 na Februari Mosi wilayani Meatu.
Hakimu Nkwabi alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na aliahirisha hadi Februari 24 zitakapotajwa tena.
Katika kesi ya tatu ambayo ni kukutwa na silaha kinyume cha sheria iliyosomwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Mary Mrio, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matano.
Washtakiwa hao ni Buluma, Mjika, Pangani, Ngunga, Mandagu, Huya na Kanga ambao baadhi yao walikiri kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria akiwamo Njile anayedaiwa kutungua helikopta hiyo.
Washtakiwa hao walikiri mashtaka mawili ambayo ni kukutwa na bunduki aina ya Riffle 303, wakati Ngunga na Mandagu walikiri shtaka la tatu, nne na tano la kukutwa na silaha na risasi bila ya kibali.
Hata hivyo, Hakimu Mrio alishindwa kutoa hukumu kwa washtakiwa waliokiri kosa kutokana na kutokuwapo kwa vielelezo mahakamani hapo, hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi leo.
Muonekano wao haufanani na biashara ya meno ya tembo choka mbaya
ReplyDeleteHii tabia ya mahakimu kutotoa hukumu wakati ushahidi upo inauzi sana. Au mahakimu ndio mambo ya rushwa
ReplyDeleteNi kweli kimwonekano hawafanani na biashara hiyo ya meno ya tembo tunayosikia kuwa ina hela nyingi,inawezekana wahusika wakubwa wa biashara hii bado hawajakamatwa
ReplyDeletewamkamate na kinana ndie jangili kuu la wanyama poli
ReplyDeleteKuna mtu mwengine nyuma Yao lazima awajibike
ReplyDelete