Waziri wa zamani wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Hawa Ghasia, ameshinda kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa dhidi yake na wanachama wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, kupinga kuchaguliwa kwake kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini.
Ushindi huo unatokana na uamuzi uliotolewa na Jaji Fauz Twaib, baada ya kutupilia mbali maombi ya kupunguziwa gharama za kesi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wanachama hao kutoka chama cha upinzani, Alli Mohamed Lipemba na Bora Abdallah Mkonda.
Jaji Twaib alikubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na wakili wa Ghasia, Samson Mbamba, ambaye aliiambia mahakama kuwa maombi ya kupunguziwa gharama yalikuwa yamewasilishwa nje ya muda unaotakiwa kisheria.
Mbamba alieleza kuwa kwa mujibu wa Sharie ya Uchaguzi, mwombaji anapaswa kuwasilisha maombi ya kupunguziwa gharama ndani ya siku 14 tangu shauri la kupinga matokeo linapofunguliwa mahakamani.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, waombaji walifungua kesi ya uchaguzi Novemba 25, 2015, ambapo siku 14 ziliishia Desemba 9, 2015, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ya kupunguziwa gharama.
Lakini waombaji waliwasilisha maombi yao Desemba 10, 2015.
Kufuatia uamuzi huo wa mahakama, kesi ya uchaguzi nayo imekufa na hivyo kumfanya Mbunge huyo mteule aliyechaguliwa kwa tiketi ya Chama Cha Mapindzi (CCM) kwa kura 24,258 kuendelea kushikila jimbo hilo.
Mpinzani wake kutoka CUF aliambulia kura 22,615 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Wanachama hao wa CUF walidai kuwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi yalighubikwa na dosari nyingi ambazo zilijitokeza tangu wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi na mchakato mzima wa ujumlishaji na hivyo kufanya shughuli nzima kuwa batili.
Walidai kuwa jumla ya kura zilizotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi kumfanya Ghasia mshindi hazikulingana na zile zilizokuwa zimebandikwa kwenye vituo katika jimbo zima.
Kwa mujibu wa wanachama hao, mgombea kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na alitoa taarifa kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu kujitoa kwake.
Lakini cha kushangaza Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo hakuondoa jina la mgombea wa Chadema katika orodha ya wagombea na katika uchaguzi huo alipata kura 793.
Kutokana na dosari hizo na nyinginezo, ziliwafanya wanachama hao wawili wa CUF kukimbilia mahakamani kupinga matokeo hayo ya uchaguzi dhidi ya Ghasia na walalamikiwa wengine wawili, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.