Moyo wa Chuma wa Mbwana Samatta na Kilichowashinda Boban na Henry Joseph Kucheza Mpira wa Kulipwa Ulaya
1
February 13, 2016
Wahenga wana usemi wao ati ‘mvumilivu hula mbivu’ usemi huu kwa tafsiri ya kawaida kabisa humaanisha jinsi ambavyo binadamu anaweza kula matunda mazuri endapo tu atavumilia shida na jua wakati wa utafutaji wa tunda hilo.
Kwa utamaduni wetu wa Kiswahili hakuna kitu kigumu kama kuishi kwa ndugu, mbali na nyumbani kwenu. Ni rahisi sana kutafuta vijisababu ati unateswa na shangazi yako ama shemeji ili tu urudi ukajitanue nyumbani kwenu.
Mwaka 2013 niliposafiri kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya mashindano ya Guinness Football Challenge niliamini kuwa hakuna kitu kigumu kama kwa Mtanzania wa kawaida kuishi umangani, hali ya hewa (baridi kali), chakula (hakuna chipsi mayai) na mambo mengine mengi ya Kiswahili tuliyoyazoea, kupiga soga na marafiki na mambo kama hayo, inahitaji kujitolea sana kuishi.
Ukisoma historia ya safari ya Yaya Toure kutoka Abdjan hadi sasa anakula maisha Etihad, akihama kutoka nchi ya joto Cote d’Ivory hadi Moscow sehemu yenye baridi kali, kubaguliwa rangi na matatizo ya lugha, lakini alikomaa hadi sasa sio tu siye waafrika wenzake bali wazungu wanamtukuza, kweli mvumilivu hula mbivu.
Haruna Moshi Boban alipata fursa ya kucheza ligi kuu ya nchini Sweden, tukafurahi kwamba sasa Tanzania inaanza kupata wachezaji wa kimataifa, lakini kilichomfanya Boban arudi Dar es Salaam, bila shaka tumekielewa kidogo mara baada ya kusoma hapo juu, nchi nyingi za wenzetu, zina mazingira magumu sana kwa mtu kupata bangi na mambo mengine kama hayo, la! kwa gharama kubwa, ni ngumu sana kwa uswahili wetu huu.
Unakijua alichoshauriwa ndugu yangu Mrisho Ngassa asiende Sudan, na kuamua kubakia zake ligi ya Bongo? Je, nini kilimshinda Henry Joseph Shindika hata arudi nyumbani akishindwa maisha ya Norway? Inahitaji moyo wa chuma wa Yaya Toure, kufikia kilele.
Wiki hii nikiwa natazama mahojiano maalumu kati ya watangazaji wa Sports Bar ya Clouds Tv na mshambuliaji wa Tanzania anayekipiga Genk Ubelgiji, nilikumbwa na hisia kubwa na kumwomba Mungu wangu azidi kumtia nguvu na kumfanyia wepesi Mbwana Samatta afikie kilele cha matarajio yake.
Maisha ya Mbwana Samatta ni magumu mno kwa wachezaji ama yeyote mwenye moyo wa karatasi na mtu asiye mvumilivu.
Ingawa ni mapema bado sana, lakini kwa Mbwana Aly Samatta, ni ngumu sana kukubali yaishe huko umangani ili arudi kuandikwa na magazeti yetu hapa ya sports, tumuombee.
Safari hii ya Mbwana Aly Samatta ni zaidi ya funzo kwa wanamichezo wote nchini pamoja na yeyote yule mwenye kutaka kuziishi ndoto zake. Juhudi na uvumilivu wa Samatta utampeleka sehemu ambayo hakuna mtu yeyote amewahi kufikiria kuna siku Tanzania itakua na mwakilishi wake, kila la kheri Mbwana Ali Samatta.
By Na Simon Chimbo
Tags
Ndugu mwandishi,mbwana hayupo umangani yupo uzunguni
ReplyDelete