Mtandao wa Uhalifu Bandarini Uanikwe..Kuna Uhalifu wa Kitaasisi na si Wanjanja Wachache Kama Inavyodhwaniwa

Jumatano Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea tena Bandari ya Dar es Salaam kufuatilia utendaji kwenye eneo hilo muhimu katika kuendesha nchi.

Kwa mara nyingine, Waziri Mkuu alishuhudia mambo yanavyoendesha kwa jinsi ambayo inatia shaka baada ya kukuta bomba lililojengwa kutoka bandarini hadi eneo la kampuni ya Tipper, ambayo inafanya shughuli za uagizaji mafuta.

Eneo ambalo bomba hilo linaelekeza mafuta, limezungushiwa uzio na hivyo haliwezi kufikiwa na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na hivyo usimamizi wa kinachoendelea humo ndani ni mgumu hata kama kuna wizi mkubwa wa mafuta.

Waziri Mkuu hakuweza kupata maelezo ya kutosha kuhusu bomba hilo na kuagiza uongozi wa Tipper, kampuni inayoendeshwa kwa ubia baina ya Serikali na Oryx Energy na uzio unaozuinguka eneo la Tipper uvunjwe ili Mamlaka ya Bandari iweze kuratibu uingizaji mafuta.

Tukio hilo limetokea wakati Waziri Majaliwa akiibua kashfa za ufisadi bandarini, zikiwamo za ukwepaji kodi kwa kupitisha makontena kinyemela na kutolipa ushuru. Imebainika kuwa zaidi ya makontena 11,000 yalipitishwa kinyemelea bila ya kulipiwa ushuru na hayo ndiyo maisha ya bandarini kwa miaka mingi sasa.

Tukio hilo la Jumatano limeibua maswali mengi kuhusu usimamizi wa bidhaa zinazoingia bandarini, na hasa mafuta ambayo kwa sasa ndiyo yanayotegemewa sana kuendesha uchumi kutokana na kutegemewa na sekta zote. Haiingii akilini kwamba bomba linalochepusha mafuta linajengwa mchana bila ya viongozi wahusika kuhoji sababu za ujenzi huo na linaanza kutumika bila ya wahusika kuhoji.

Haiingii akilini kwamba ujenzi wa bomba hilo pia ulihusisha ujenzi wa mabomba mengine ya kuchepusha mafuta na yakaanza kufanya kazi kwa muda wote bila ya wahusika kuhoji.

Kwa maana nyingine kama wizi huo uchunguzi utabaini wizi huo, ni dhahiri kuwa utakuwa ni uhalifu wa kitaasisi na si wa wajanja wachache kama inavyotokea kwenye maeneo mengine, kitu ambacho ni hatari. Wakati hayo yakitokea, Wakala wa Vipimo (WMA) nao waliamua kuzima mita za kupima mafuta na badala yake kufanya kazi hiyo kwa kutumia miti, uamuzi ambao pia unatia shaka kuhusu usimamizi wa mali za umma.

Katika hali inayotia shaka, mita iliwashwa saa chache kabla ya Waziri Mkuu kutembelea na alipouliza sababu za kuwasha mita siku hiyo, aliambiwa ni maagizo kutoka kwa kigogo.

Kuhusu mita kuzimwa, Waziri Mkuu aliambiwa kuwa hilo lilifanyika kwa hisia kuwa wafanyabiashara walikuwa wanapunjwa ndiyo maana mita zikazimwa. Hivi bidhaa nyeti kwa uchumi kama hiyo inafanyiwa maamuzi kwa hisia?

Ni lazima kuna uhalifu wa kitaasisi unafanyika katika uingizaji mafuta na ndiyo maana mambo ambayo yalikuwa yakifanyika kweupe, lakini yakafumbiwa macho na viongozi.

Tunashauri kuwa uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini mtandao wote wa uhalifu huo kwenye nishati hiyo nyeti kwa uchumi wa Taifa.

Uchunguzi huo uwe wa kina ambao utalenga kubaini watu wote walioko kwenye mtandao huo unaojihusisha na vitendo vya upitishaji bidhaa bila ya kulipia ushuru na kodi husika kwa kuwa ndio wanaopunguza uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi wake.

Na kwa kuwa bandarini kunaonekana kuwa kumekithiri kwa vitendo vya wizi na hujuma, Serikali iendelee kuweka jicho kali eneo hilo ili kukomesha wizi unaotesa wananchi huku ukinufaisha kikundi cha wachache wanaoishi maisha ya kifahari kwenye nchi maskini.

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Haya mafisiemu, uwanja wenu. Anzeni kutetea kwa nguvu zote. Maana ni kawaida yenu kwa vile nyinyi ni misukule tu!!!!

    ReplyDelete
  2. Jamani tusichoke kuwaombeA hawa watumbua majipu uzima maana hicho Ni kitu muhmu kwao .amiin

    ReplyDelete
  3. magufuli fukuza kwanza waisadizi wako kwani hawa ndo watoa siri za safari zako za ghafla majipu yapo mengi tunayo jinsi gani ya kukupata hatujui kwani wasaidizi wako hatuwaamini 10000000000% hutoa siri
    Pro MUHONGOOOOOOOO

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad