Siku 100 Za Rais Magufuli Ikulu, Wapo Waliolia na Wengine Kucheka...

Ni kweli siku hazigandi kwamba Rais John Magufuli aliyeingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, ametimiza siku 100 leo.

Tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, Rais Magufuli  amejitahidi kuishi katika maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.

Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika.

 Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi.

 Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati hawafanyi kazi yoyote.

Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.

Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Rais Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.

Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza.

Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani, Mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji.

Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure.

 Alivyoanza kazi
Mara tu baada ya kuingia ofisini, alimuapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.

Katika siku zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.

Mtindo wake huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa na wengine.

Katika siku zake hizo za mwanzo, Rais Magufuli pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.

Atoa Msimamo wake
Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, alikutana na watumishi wa Serikali ikiwa ni pamoja na manaibu katibu wakuu, manaibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali.

Katika kikao hicho, aliwataka kujiandaa kufanya kazi kwa ufanisi katika Serikali ya awamu ya tano chini yake. huku akiwasisitiza juu ya dhamira yake ya kuendeleza kaulimbiu yake ya “Hapa kazi tu”.

Kikao hicho pia kiliudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali anayoitaka.

Afuta Safari za Nje
Rais Magufuli alitumia kikao hicho kutangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine, na kueleza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi.

Alisema mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.

Badala yake aliwataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi.

Hadi sasa, Rais Magufuli bado hajakwenda safari yoyote ya nje ya nchi zaidi ya kuwatuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda kumwakilisha kwenye shughuli mbili tofauti.

Safari zake  ndani ya nchi
Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam alipokwenda mkoani Dodoma ambako alifungua Bunge la 11.

Katika mkutano wake, Rais Magufuli alijikuta akisusiwa hotuba yake na wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga uteuzi wake na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kama rais halali, baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Januari 12, mwaka huu, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya kukodi kwenda Zanzibar ambako alihudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Januari 21, mwaka huu alifanya ziara ya kwanza mkoani Arusha, ambako alikwenda pia katika Chuo cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) Monduli kutunuku vyeo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuhitimu mafunzo, huku naye akiwa amevalia sare za jeshi hilo.

Februari 5, mwaka huu pia Rais Magufuli alisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Singida kuhudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akataa sherehe ya kifahari Bungeni
Rais alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695.

Afuta gwaride la Uhuru
Novemba 9, mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru na kwamba fedha zitakazookolewa atazipeleka sehemu nyingine.

Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.

Baraza la Mawaziri
Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.

Katika uteuzi wake, aliacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa madai alikuwa akitafuta watu watakaofaa kuteuliwa kuongoza wizara husika.

Wizara ambazo hakuteua mawaziri katika baraza lake la awali alilolitangaza ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Desemba 23, mwaka jana ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli alikamilisha baraza lake kwa kuwataja mawaziri wanne waliokuwa wamebakia.

Uteuzi wa Rais Magufuli umekuwa wa tofauti ambapo viongozi wengi aliowateua kushika nafasi mbalimbali ni wasomi wa ngazi ya uprofesa na udaktari.

Mabalozi Wapigishwa  Kiapo cha Utii
Katika mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi yake, Rais Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao.

Akiwaapisha kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni bora ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi.


Majipu 152  Yatumbuliwa
Ndani ya siku hizi 100  za  uongozi  wa  Rais  Magufuli, watumishi wa umma 152  wamefukuzwa  kazi  kutokana na kasoro mbalimbali za kiutendaji.

Hao ni watumishi waliotimuliwa kwa majina au vyeo vyao, lakini ukijumlisha na wengine waliosimamishwa au kufukuzwa kwa matamko bila kutajwa majina, idadi ni kubwa zaidi.

Watumishi hao wamesimamishwa na baadhi wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, Rais kutoridhishwa na utendaji wao, wizi kwenye taasisi zao, ukwepaji kodi, tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na utovu wa nidhamu.

1.Muhimbili
Hatua za kusimamisha na kutimua zilianza siku nne tu baada ya Rais kuapishwa, ambapo Novemba 9, 2015 Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hussein Kidanto, alihamishwa na bodi iliyokuwa na wajumbe 11 ilivunjwa.

2.TRA
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade Novemba 27.

3.Bodi ya TPA
Desemba 7, mwaka jana, Magufuli alivunja bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadh Massawe.

Pia, aliwasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD). Jumla ya waliotimuliwa TPA na TRA ni watu 47.

4.Takukuru
Akiendelea na kasi yake, Desemba 16, 2015 Rais alitengua uteuzi wa nafasi nyeti ya Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah. Rais alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa Takukuru chini ya mkurugenzi huyo.

Maofisa wengine wa taasisi hiyo walisimamishwa kazi kwa kukiuka maagizo yaliyohusu safari za nje.

Waliosimamishwa kazi ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, wakiwa watumishi waandamizi wa taasisi hiyo.

5.Rahco
Rais JPM alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), Benhadard Tito, Desemba 23, 2015 kwa kile kilichoelezwa ni “ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ununuzi” katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

Pia alivunja bodi ya Rahco yenye wajumbe wanane na bodi ya TRL yenye wajumbe wanane pia.

6. Katibu Tawala Mwanza 
Akiendelea na kasi hiyo, Januari 15, alitengua uteuzi na kumfukuza kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Faisal Issa kutokana na “utovu mkubwa wa nidhamu” aliounyesha katika kikao cha cha kamati ya ulinzi kilichofanyika mjini Mwanza.

7.Idara ya Uhamiaji 
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia utawala na fedha, Piniel Mgonja Januari 21 ili kupisha uchunguzi baada ya kubaini dosari kadhaa kwenye ofisi hiyo.

8.NIDA
Januari 25, Dk Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya Sh179 bilioni.

Wengine waliosimamishwa Nida ni Joseph Makani ambaye ni mkurugenzi wa Tehama, Rahel Mapande (ofisa ugavi mkuu), Sabrina Nyoni (mkurugenzi wa sheria) na George Ntalima, ofisa usafirishaji.

Pia, aliwarudisha nyumbani mabalozi wawili, Dk Batilda Buriani aliyekuwa Japan, Dk James Msekela (Roma, Italia). Pia, Peter Kallaghe (Uingereza) na kurejeshwa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano, Kikanda na Kimataifa.

                          Dunia nzima Yamkubali
Kutokana na kasi yake ya mabadiliko ya kweli ya uongozi wake, hasa kudhibiti matumizi na kuelekeza fedha katika huduma za kijamii, Rais Magufuli amekuwa gumzo kwenye anga za kimataifa.

Uongozi wake umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo anayoyafanya, yanagusa ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya safari yoyote ya nje ya nchi kama wanavyofanya viongozi wengine.

Tangu aingie madakarani, amedhibiti mabilioni ya fedha na kuzielekeza katika kuboresha huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), ruzuku ya shule na miundombinu ya barabara.


                        Changamoto: Sakata  la  Zanzibar
Pamoja na yote, suala la kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar limekuwa likiitesa Serikali ya Rais Magufuli.

Wakati Chama Cha Mapinduzi kikitaka uchaguzi huo urudiwe, Chama cha Wananchi (CUF) kimeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakitakubali marudio ya uchaguzi huo na hakitashiriki.

CUF wanaamini Rais Magufuli pekee ndiye anayeweza kumaliza mzozo huo ulioibuka visiwani humo, lakini kiongozi huyo hajazungumza lolote hadi hivi sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alipotangaza kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Kuendelea kuwako kwa mgogoro huo, ni wazi kwamba kunaitia doa Serikali ya Dk. Magufuli nje ya nchi.  

Post a Comment

12 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Zanzibar it's our motto
    We don't care how much he did
    Zanzibar it's part of Tanzania

    ReplyDelete
    Replies
    1. Vipi,issue ya mafuta yaliyogunduliwa Zanzibar nayo atakuwa na maamuzi nayo?

      Delete
    2. Nenda kaisome vizuri katiba ya nchi yako ya Zanzibar kwanza.
      Kuna wakati Pinda alitoa kauli kuwa Zanzibar sio nchi,hawa wazee wa kanzu wakataka kumtoa roho kwa maneno makali..

      Delete
    3. Zanzibar wamalizane wenyewe.
      Magufuli hatakiwi kuingia kwenye hili,soma katiba.

      Delete
    4. Whatever,let us be honest,Iam sure you are proud with JPJM.Meza tu.
      Magufuli ni mwambaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa.

      Delete
  2. HAHUSIKI NA UCHAGUZI WA ZANZIBAR HATA JAJI MKUU NA LUBUVA WALISHATOA UFAFANUZI

    ReplyDelete
  3. Wacha UKIWA wajinyonge Jembe ni Jembe tuuuuuuuu

    ReplyDelete
  4. Anahusika sana mbona anapeleka majeshi km hahusiki?

    ReplyDelete
    Replies
    1. ACHA UJINGA WAKO AHUSIKE KATIKA LIPI? WACHE WAMALIZANE WENYEWE SI WANA SERIKALI YAO??????? NA TUME SI YAOOOOOOO

      Delete
    2. Majeshi ni ya jamhuri ya Muungano, na yemepekwa Zanzibar kwa maombi ya serikali ya Zanzibar. Lkn maswala ya uchaguzi kila sehemu inaendesha kivyake. Zanzibar wana ZEC na bara kuna NEC.
      na kwa mujibu wa katiba Zanzibar mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ndie mwenye kauli ya mwisho ktk issues za uchaguzi, haingiliwi na mtu yoyote...upo hapo

      Delete
    3. Zanzibar kwa ujinga wao na viongozi wao vibaraka WA waarabu acha wauane,...ila jeshi lipo na kazi itafanyika kama hali itahitaji hivyo

      Delete
  5. Mr Presidaaa ishi miaka mingi baba, ili uzidi tumbua vipele, vijipu uchungu na mijipu.
    Magufuli oyeeeee

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad