Wadau mbalimbali wakiwamo wananchi, polisi, Jeshi la Wananchi (JWTZ), Wizara ya Mambo ya Ndani wamezungumzia kuongezeka kwa ujambazi katika jiji la Dar es Salaam.
Baadhi wamesema matukio hayo ya ujambazi yamesababishwa na udhaifu wa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na wahalifu wanaotumia silaha kupora fedha kwenye mabenki na maduka makubwa.
Sababu nyingine zinazotajwa ni majambazi hao kuhukumiwa vifungo vya muda mfupi na kutoka gerezani mapema, hali inayorudisha nyuma juhudi za Serikali kupambana na uhalifu.
Kadhalika, umbali wa kituo kimoja cha polisi mpaka kingine, na mara nyingine baadhi kufungwa siku za mwisho wa juma, ni moja ya mambo yanayosababisha kuongezeka kwa uhalifu.
Chanzo kingine kilichotajwa kuchochea ongezeko la uhalifu ni kuhujumiwa kwa Jeshi la Polisi na baadhi ya askari wake ambao ama hutoa silaha kwa wahalifu au kushiriki.
Maoni ya wananchi
Mkazi wa Tandika, Iddi Shomvi alidai jana kuwa majambazi wengi wanaopora fedha kwenye mabenki ni askari wa JWTZ), waliopitia mafunzo ya mgambo, pamoja na polisi. Alisema watu hao ndiyo wenye ujuzi wa kutumia silaha na wanajua zinakopatikana.
“Mwananchi wa kawaida hawezi kutumia silaha za moto wala mabomu. Wanajeshi na polisi ndiyo wanaojua kutumia na wanazo hizo silaha. Nina uhakika kwamba wao ndiyo wanaotupa shida mitaani kwa sababu ya tamaa zao za fedha,” alisema Shomvi.
Alisema ni muhimu Jeshi la Polisi likashirikiana na wananchi kuanzia ngazi za chini ili kuwatambua majambazi na wageni wote walioingia nchini kinyume cha sheria. Alisema baadhi ya wageni nao pia ni chanzo cha kuingia kwa silaha kali nchini.
“Serikali irudishe mfumo wa nyumba kumi ili kila mtu atambulike anafanya nini. Mgeni akija kutoka Burundi, anaweza kuishi na Watanzania bila kufahamika yeye ni nani na anatoka wapi,” alisema.
Mkazi wa Tabata, Severin Lawrence alisema ujambazi unaongezeka kwa sababu utendaji wa polisi ni dhaifu. Alisema inashangaza kuona vituo vinafungwa siku za wikiendi wakati ndiyo zenye matukio mengi.
“Ni jambo la aibu kabisa. Unaona kituo kile cha polisi! Leo kimefungwa. Sasa likitokea tukio la ujambazi hapa tutakimbilia wapi kutoa taarifa?” alihoji kijana huyo huku akionyesha Kituo cha Polisi cha Tabata Relini ambacho kilikuwa kimefungwa.
Lawrence aliitaka Serikali kufunga mfumo wa GPS kwenye pikipiki zote kwa sababu vyombo hivyo vya usafiri ndivyo vimekuwa vikitumika kwenye matukio ya ujambazi. Alisema hilo litasaidia kuwabaini watu wanaojihusisha na ujambazi popote.
Mkazi wa Kitunda, Jumaa Lukindo alisema kitendo cha askari kukaa vituoni kwa muda mrefu kumewafanya wazoeane na wahalifu, jambo linalofanya vita dhidi ya ujambazi jijini kuwa ngumu.
Lukindo alitaka polisi wapewe silaha nzito ili waweze kukabiliana na majambazi ambao nao wanatumia silaha kali.
“Kwenye tukio la ujambazi pale Mbagala, tumesikia kwamba majambazi walitumia pia mabomu ya kutupa kwa mkono. Hao si raia wa kawaida, ni watu wenye ujuzi na mambo ya silaha. Polisi nao wajipange kikamilifu,” alisema.
JWTZ wazungumza
Akizungumzia kuhusika kwa wanajeshi kwenye matukio ya ujambazi, msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema hakuna uthibitisho wowote kwamba wanajeshi walihusika katika matukio ya ujambazi, hususan lile la Mbagala.
Lubinga alisema mahakama ndiyo inayoweza kuthibitisha baada ya watuhumiwa kukamatwa na kesi zao kusikilizwa. “Siwezi kusema nani anaiba, lakini Tanzania kuna ujambazi. Jambazi anaweza kuwa mtu yeyote, anaweza kuwa padri, sheikh au mwananchi wa kawaida. Lakini hatuwezi kumwita jambazi mpaka itakapothibitika,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Charles Kitwanga kuomba msaada ya JWTZ kusaidia vita dhidi ya ujambazi, Lubinga alisema hawajapokea rasmi maombi hayo, lakini watakuwa tayari endapo Serikali itaamua kulitumia katika vita hiyo.
“Serikali ikiamua kuunganisha nguvu, tutakuwa tayari lakini siwezi kusema lini tutaanza operesheni hiyo kwa sababu lazima atangaze Amiri Jeshi Mkuu. Cha msingi majambazi waache kuiba kwa sababu Serikali imechukia na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Kanali Lubinga.
Makamanda wa polisi, Dar
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alisema kuongezeka kwa matukio ya ujambazi Dar es Salaam kunasababishwa na mambo mbalimbali, kama watuhumiwa kuachiwa huru na mahakama mara wanapokamatwa.
Mkondya alitaja sababu nyingine kuwa ni majambazi wanaokutwa na hatia kufungwa kwa muda mfupi, hali inayosababisha kuendelea na ujambazi mara wanaporudi mtaani na kufanya kasi ya ujambazi kuongezeka.
“Tunaomba Mahakama itusaidie, majambazi hawa wakae magerezani kwa muda mrefu ili wasilete shida mitaani. Sisi polisi pia tutajitahidi kujenga ushahidi mzuri ili majambazi wasiachiwe huru wakifikishwa mahakamani,” alisema.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kila wanapowaona au kuwahisi majambazi ili nyendo zao zifuatiliwe. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema hawezi kuzungumzia matukio ya ujambazi kwa sababu za kiintelijensia na kuwa upelelezi wa matukio mbalimbali bado unaendelea.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio la juzi Mbagala,” alisema kamanda huyo na kusisitiza kuwa wananchi wawe watulivu, polisi wanafanya kazi yao.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mkuu mpya wa upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam, Camilius Wambura alisema: “Ndiyo kwanza nimeteuliwa, hata sijaripoti kazini. Nikiripoti, nitayasoma na kuangalia namna gani tutayafanyia kazi.”
Mambo ya Ndani
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema anafahamu kuwa matukio hayo ni makubwa lakini hawezi kusema chochote hadi apate ripoti kamili.
Siri ya Matukio ya Ujambazi Dar es Salaam Yawekwa Bayana
0
February 29, 2016
Tags