Steven Wasira Amkunja Shati Mwandishi Baada Ya Kesi Yake Kupinga Ushindi wa Ester Bulaya Kutupiliwa Mbali Na Mahakama

Mwanasiasa mkongwe nchini, Steven Wasira jana alimvamia mpigapicha wa gazeti la Mwananchi aliyekuwa akichukua picha zake wakati akitoka mahakamani, lakini akashindwa kutimiza azima yake ya kufuta picha.

Wasira, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wa Serikali ya Awamu ya Nne (SA4), alifanya kitendo hicho akitoka kwenye jengo la Mahakama ya Biashara ambako maombi yake ya kukata rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge, jimbo la Bunda yalitupwa na Mahakama Kuu.

Katika kinyang’anyiro hicho cha ubunge, Wasira, ambaye amekuwa mbunge wa Mwibara tangu mwaka 1970 na baadaye mbunge wa Bunda hadi mwaka 2015, aliangushwa na Ester Bulaya wa Chadema katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana. Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari akiwamo walishuhudia tukio hilo.

“Wasira alimkimbiza Jamson akitaka kumnyang’anya kamera, lakini hakuweza,” alisema Nyange,mwandishi  wa  gazeti  la  Mtanzania.

“Baadaye alitaka kumgonga kwa gari lake wakati akiondoka lakini ikashindikana.”

Akisimulia tukio hilo, Jamson alisema Wasira, ambaye amefanya kazi na serikali za awamu zote tangu katikati ya miaka ya 70, alichukizwa na kitendo chake cha kumpiga picha.

“Wasira alinifuata na kuniuliza sababu za kumfuatilia kila mara. Aliniuliza picha nazopiga nazipeleka wapi,” alisema Jamson.

“Njoo, njoo hapa wewe kijana. Nakuambia futa hizo picha kwa usalama wako.Hivi mnatafuta nini maana mnanifuatilia tangu nikiwa kule Mahakama Kuu hadi huku Mahakama ya biashara,” alisema Wasira

Jitihada za Wasira kumnasa Jamson ziliendelea hadi nje ya eneo la mahakama ambako alimfuata kwa kutumia gari aina ya Toyota Land Cruiser (namba tunazihifadhi).

Katika kumfuatilia, gari la Wasira nusura limgonge mpigapicha huyo, lakini waandishi wenzake walimnusuru kwa kumsukumia pembezoni mwa barabara.

Juhudi za kumpata Wasira kuzungumzia sababu za kutaka kumshambulia mpiga picha huyo kwa kuchukua picha za tukio hilo, hazikuzaa matunda.

Awali, Jaji Sirilius Matupa alitupilia mbali maombi ya ruhusa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kufuta shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa Bunda baada ya kubaini waliowasilisha maombi hayo, Magambo Masato na wenzake wanne, hawakufuata sheria.

Uamuzi huo ulisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Eugenia Rujwahuka kwa niaba ya Jaji Matupa.

Katika maombi yao ya msingi, Magambo Masato na wenzake waliiomba mahakama kutengua matokeo yaliyompa ushindi Bulaya wakidai licha ya Wasira kunyimwa haki kuhakiki na kuhesabu upya kura, mchakato wa uchaguzi huo pia uligubikwa na vitendo vya rushwa.

Akisoma maamuzi hayo kwa niaba ya Jaji Sirilius Matupa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Eugenia Rujwahuka alisema maombi hayo yamewasilishwa kwa kutumia kifungu cha sheria kisichohusika.

“Badala ya kuwasilisha maombi yao kwa kutumia kifungu cha 15 (c) cha Sheria ya Uchaguzi Sura namba 141, waleta maombi wametumia kifungu cha 15 (a) (b),” alisema Rujwahuka akimnukuu Jaji Matupa.

Wakati huohuo, shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Nyamagana, iliyofunguliwa Ezekiah Wenje, imesikilizwa jana na kuahirishwa hadi Februari 29, mwaka huu.

Akiahirisha shauri hiyo iliyoahirishwa mara mbili mfululizo Jumatatu na Jumanne iliyopita, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo aliziagiza pande zinazohusika kuhakikisha zinakamilisha taratibu zote za kisheria ili shauri hilo lianze kusikilizwa mfululizo.
Tags

Post a Comment

5 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mzee pumzika umechoka achia vijana nao wafanye acha Kiki zako za kizee

    ReplyDelete
  2. Huyo ndio TYSON bana, hapana chezeiya

    ReplyDelete
  3. No, Mhe Wasira Stephen huwa hana shida kabisa ila huyo mwandishi alichokuwa anafanya si kizuri. Tunafahamu kuwa ni sehemu ya majukumu yao kupata taarifa na picha lakini si tu kila wakati unafuata mtu. Hata hivyo picha za wasira ziko library nyingi sana kuna haoja gani kuanza kuaibishana kihivyo

    Mwandishi ajifunze ustarabu kidogo

    ReplyDelete
  4. HII ILIKUA KALI,ULIKUA NI UVUNJIFU WA AMANI,LILIKUA NI KOSA LA JINAI,LILIKUA NI JARIBIO LA KUUA TENA KWA MAKUSUDI, WANANCHI TUNASUBIRI KWA HAMU KUONA JINSI SERIKALI YETU ITAKAVYOUTUMIA UWEZO NA UKWELI WAKE KWA HILI.NI TUKIO BAYA,LA KUHUZUNISHA,LINATISHA NA WASSIRA ANAPASWA KUCHUKULIWA HATUA SASA.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad