TAARIFA KWA UMMA
MGOGORO WA CHUO KIKUU CHA MT. YOSEFU TANZANIA(SJUIT) KAMPASI YA ARUSHA
1. Tunapenda kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) Kampasi ya Arusha ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambacho kilianza kudahili wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka wa masomo 2013/2014.
2. Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.
3. Tume inatambua kuwa kwa nyakati tofauti kumekuwapo na matukio ya migogoro baina ya uongozi wa Chuo Arusha na wanafunzi.
Tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu chimbuko la migogoro hiyo na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa chuo kurekebisha kasoro zinazosababisha migogoro chuoni hapo.
Katika kutekeleza azma hiyo, hivi karibuni Tume iliunda jopo la wataalam kufanya ukaguzi wa kina katika Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania Kampasi ya Arusha. Ripoti ya ukaguzi huo iliwasilishwa tarehe 22/02/2016.
4. Kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kisheria, ripoti hii inatakiwa kuwasilishwa na kujadiliwa na Kamati ya Ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu, ambayo itatoa mapendekezo kwa Tume kuhusu hatua stahiki za maamuzi. Kamati hii itakutana katika kikao cha dharura tarehe 25/02/2016 saa 3:00 asubuhi, na taarifa ya Kamati hiyo itawasilishwa kwenye Mkutano wa dharura wa Tume tarehe hiyohiyo saa 9:00 alasiri.
5. Kwa mantiki hiyo, taarifa rasmi kuhusu maamuzi yaliyofikiwa juu ya hatma ya Kampasi hiyo ya Arusha ya Chuo cha Mt. Yosefu itatolewa siku ya Ijumaa tarehe 26/02/2016.
6. Kwa taarifa hii, Tume inawaomba wanafunzi wote wa Chuo cha Mt. Yosefu Kampasi ya Arusha kuwa watulivu wakati huu ambapo suala lao linashughulikiwa.
7. Tume inapenda kutumia fursa hii pia kuwaarifu wanafunzi wote wa vilivyokuwa Vyuo Vikuu Vishiriki vya Sayansi za Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Teknolojia ya Habari (SJUCIT), kuwa orodha ya majina yao na vyuo walivyopangiwa inapatikana katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu. Hivyo wanashauriwa kuondoka Chuoni mara moja na kujiandaa kwa ajili ya kuripoti katika vyuo walivyopangiwa katika muhula wa pili.
Imetolewa na
PROF. YUNUS D. MGAYA
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
24 Februari 2016