1. Utangulizi
Mnamo mwezi Februari mwaka 2015, serikali ya Tanzania ilizindua sera mpya ya Elimu na Mafunzo.
Sera hii imepanua wigo wa elimu ya msingi kwa kuiunganisha na elimu ya sekondari (hii ilikuwa ikitolewa bure na kwa lazima tangu mwaka 2001 baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi {MMEM}).
Sera hii imepanua wigo wa elimu ya msingi kwa kuiunganisha na elimu ya sekondari (hii ilikuwa ikitolewa bure na kwa lazima tangu mwaka 2001 baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi {MMEM}).
Tangu kuchaguliwa kwa Rais John Pombe Magufuli mwezi Octoba mwaka 2015, utekelezaji kikamilifu wa sera hii imekuwa moja ya ahadi kuu za serikali yake.
Rais Magufuli aliwahakikishia wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule za msingi na sekondari katika hotuba yake ya ufunguzi wa bunge la kumi na moja kuwa hawatapaswa kutoa michango yoyote kuanzia mwezi Januari mwaka 2016.
Rais Magufuli pia alibainisha kuwa fedha zote zitakuwa zikipelekwa moja kwa moja shuleni, na kuongeza kuwa “Nina uhakika fedha hizo zitatumika vizuri, ole wao watakao zitumia vibaya.”
Japokuwa dhamira hii ya kutoa elimu bure mpaka kiwango cha sekondari (kidato cha nne) kwa kila mtoto wa Kitanzania ni hatua kubwa katika historia ya nchi, lakini upatikanaji fursa za elimu siyo changamoto pekee inayoukabili mfumo wa elimu nchini Tanzania. Juhudi zote zitakuwa hazina maana kwa wananchi na taifa kwa ujumla iwapo watoto wanaenda shule lakini hawajifunzi.
Hivyo basi ubora wa elimu inayotolewa ni suala muhimu pia. Ripoti ya Uwezo ya mwaka 2014 inaonesha kuwa asilimia 19 pekee ya wanafunzi wa darasa la 3 ndiyo walioweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha darasa la pili 4 .
Tukiangalia ufaulu wa darasa la 7 mwaka 2015, takribani asilimia 68 ya wanafunzi waliofanya mitihani walifaulu 5 . Japokuwa hii ni ongezeko la ufaulu kwa karibu asilimia 11, bado ni idadi kubwa ya wanafunzi wasiofaulu ipasavyo.
Kutokana na umuhimu wa elimu katika maendeleo, na ukizingatia mabadiliko katika sekta ya elimu yanayoendelea nchini hivi sasa, ni vyema kufahamu mitazamo ya wananchi kuhusu mfumo wa elimu ya umma.
Wananchi wana mtazamo gani juu ya hali ya elimu iliyopo hivi sasa? Wana maoni gani juu ya walimu wa shule za umma na ubora wa elimu wanayopatiwa watoto wao? Je wana matarajio yapi kuwa elimu ya bure itaboresha elimu?
Je wazazi wamekuwa wakichangia fedha kiasi gani huko mashuleni, na nini athari za kupigwa marufuku kwa michango yote ya wazazi katika elimu? Na je fedha hizo zimetumikaje?
Muhtasari huu umebeba maoni na uzoefu wa wananchi juu ya utolewaji wa elimu ya msingi ya umma. Tunatumaini matokeo haya yatakuwa mwanzo mzuri wa kupima mafanikio ya utekelezaji wa sera hii mpya kwa siku za usoni.
Takwimu kutoka muhtasari huu zimekusanywa na Twaweza kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi. Sauti za Wananchi ni utafiti unaofanywa kwa njia ya simu za mkononi, wenye uwakilishi wa kitaifa. Utafiti huu unawakilisha Tanzania Bara.
Mambo muhimu kuhusu matokeo haya:
• Asilimia 76 ya wananchi wanaamini kuwa utoaji wa elimu bure utaboresha elimu.
• Asilimia 89 ya wazazi wanasema wanatoa michango ya fedha kugharamia elimu ya watoto wao waliopo shule za umma.
• Asilimia 66 ya michango ya wazazi hulipia ulinzi, asilimia 57 majaribio na asilimia 34 madawati.
• Karibu nusu ya wananchi wanaamini michango inayokusanywa shuleni haitumiki kwenye malengo husika.
• Wananchi 8 kati ya 10 wanaamini kuwa walimu hawapendi taaluma yao.
• Nusu ya wananchi wote wanaona kuwa ubora wa elimu ya msingi umezorota ama kubaki pale pale wakati nusu nyingine wanaona kuwa imeboreshwa. Hii ni ndani ya miaka 10 iliyopita.
2. Mambo sita kuhusu elimu nchini Tanzania
Jambo la 1: Wananchi wana matumaini na ahadi ya elimu bure
Asilimia 97 ya wananchi wanafahamu kuhusu ahadi ya Rais Magufuli ya kutoa elimu bure ya sekondari (kidato nne) kuanzia Januari 2016, kama ilivyoainishwa kwenye sera mpya na ilani ya chama tawala. Vilevile, asilimia 88 wana imani kuwa ahadi hii itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Asilimia 76 ya wananchi wanaamini kuwa utolewaji wa elimu bure utaongeza ubora wa elimu kwa kuboresha mazingira ya kufundishia (asilimia 55).
Pamoja na imani hiyo, asilimia 15 ya wananchi walisema elimu ya bure haitaboresha elimu, kwa kuwa kuongezeka kwa uandikishwaji wa wanafunzi kutatumia rasilimali (fedha) nyingi 8.
Asilimia 49 walisema wanafunzi hawatafanya vizuri kutokana na kukatazwa kwa masomo ya ziada ambayo walimu waliyatumia kuwasaidia wanafunzi wasiofanya vizuri huku wakijipatia kipato cha ziada. Pamoja na hayo asilimia 22 wana hofu na upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya kufundishia 9 .
Jambo la 2: Asilimia 89 ya wazazi huchangia elimu ya umma
Michango imekuwa ni sehemu ya mfumo wa elimu baada ya upanuzi wa Elimu ya Msingi kwa Wote. Asilimia 89 ya wazazi waliohojiwa walikiri kuchangia fedha kwenye shule za umma.
Wazazi walipoulizwa kuhusu kiwango cha fedha walichochangia, asilimia 80 walisema wamechangia TZS 50,000 ama pungufu kwa mwaka, huku asilimia 8 wakichangia zaidi ya TZS 100,000 .
Michango inayotolewa kwenye shule za umma hutumika kugharamia ulinzi (asilimia 66), majaribio (asilimia 57) na madawati (asilimia 34). Kiwango kidogo hutumika kwenye mahafali (asilimia 4) na safari za kishule (asilimia 4).
Utaratibu wa ugawaji wa fedha za ruzuku ni: asilimia 40 vitabu na nyenzo nyingine za kusomea; asilimia 20 kwa ajili ya vifaa vya kuandikia (kalamu, madaftari, penseli n.k.); asilimia 10 kwa shughuli za kiutawala na asilimia 10 kwa ajili ya makaratasi ya mitihani na uchapishaji. Hivyo basi, maamuzi ya kuwa ruzuku itumike vipi yanakuwa changamoto kwa upande wa shule zenyewe, na hata hivyo, inaonekana wazi kuwa michango hulipia vitu vingi zaidi kuliko ruzuku.
Jambo la 3: Asilimia 49 ya wazazi wanaamini michango ya wazazi haitumiki ipasavyo
Japokuwa wazazi wengi wamekuwa wakitoa michango ya ziada, asilimia 49 ya wazazi wanaamini kuwa fedha hizo hazitumiki ipasavyo. Wazazi wa mjini wana mashaka zaidi ambapo asilimia 57 wanasema hivyo ukilinganisha na asilimia 44 ya wazazi wa vijijini.
Vilevile asilimia 58 ya wananchi wanaamini kuwa michango hii haijaidhinishwa na serikali. Asilimia 89 wanaamini kuwa walimu wa shule za umma huchangisha fedha hizo kama chanzo cha kujipatia kipato cha ziada 11 .
Jambo la 4: Wananchi wanahusisha mafanikio ya ujifunzaji na juhudi za mwalimu
Wananchi walipoulizwa kuwa ni nini ambacho wanadhani kinachangia matokeo ya darasa la saba kwenye jamii yao (kuwa mazuri ama mabaya), nusu yao walihusisha matokeo na juhudi za mwalimu 12 . Asilimia 7 pekee ndio waliotaja changamoto zinazohusiana na wazazi au wanafunzi wenyewe 13 .
Cha kushangaza ni kwamba mwananchi 1 kati ya 3 hajui nini kinachangia matokeo ya kujifunza pindi watoto wanapohitimu elimu ya msingi.
Jambo la 5: Wananchi wanaamini kuwa walimu wanaona fahari juu ya taaluma yao lakini hawapendi kazi yao
Asilimia 93 ya wananchi wanaamini kuwa ualimu ni taaluma ambayo ndiyo msingi wa taifa. Japokuwa asilimia 79 ya wananchi wanaamini kuwa walimu wanaona fahari ya kile wanachokifanya, asilimia 80 wanaona kuwa walimu hawapendi kazi zao na hufanya tu kwa ajili ya kujipatia kipato. Je ni kwanini walimu wanaona fahari ya taaluma yao lakini hawapendi kazi yao?
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, ni kutokana na mishahara pamoja na mazingira ya kufanyia kazi. Kwa ujumla asilimia 42 ya wananchi wanaamini kuwa walimu hawalipwi vizuri, na asilimia 34 wanaamini mazingira ya kazi ya walimu hayawapi motisha wa kufundisha.
Haya ni maoni ya wananchi wachache (wananchi wengi wanatoa kauli zinazokinzana), lakini yanaweza kutoa mwanga kwanini wananchi wanadhani walimu hawapendi kazi yao.
Wananchi walipoulizwa kuhusu vitu ambavyo vinaweza kuwaongezea walimu motisha ili kutoa elimu bora kwa wanafunzi, asilimia 56 walisema nyongeza ya mishahara na asilimia 19 walitaja uboreshaji wa mazingira ya kazi.
Jambo la 6: Maoni ya wananchi yanatofautiana juu ya ubora wa elimu ya msingi.
Wananchi walipoulizwa kuhusu ubora wa elimu, nusu yao waliamini kuwa ubora wa elimu ya msingi umezorota ama kubaki vilevile kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, huku nusu nyingine wakisema elimu ya msingi imeboreshwa.
Wananchi walio wengi wanaamini njia kuu ya kuboresha elimu ya msingi ni kwa kuweka mkazo kwa walimu. Ili kuboresha elimu wananchi wametoa ushauri ufuatao kwa serikali: kufuatilia utendaji wa walimu (asilimia 40), kuongeza mishahara ya walimu (asilimia 19), pamoja na kuongeza idadi ya walimu (asilimia 10). Asilimia 7 pekee ndiyo waliotaja ushirikiano kati ya
mwalimu na mzazi kama njia ya kuwawezesha watoto kujifunza.
3. Hitimisho
Serikali mpya imejikita kwenye utoaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari na wananchi wamekuwa na imani kubwa juu ya suala hilo. Wananchi wanaamini kuwa utoaji wa elimu bure utatekelezwa katika muda ulianishwa, na ubora wa elimu utaongezeka.
Wasiwasi wa wananchi unaonekana kwenye uwajibikaji wa walimu katika kufikia kiwango cha juu cha elimu. Walipoulizwa kuhusu namna ya kuboresha elimu ya msingi, wananchi walitilia mkazo kwenye mishahara ya walimu, kuongezeka kwa idadi ya walimu mashuleni na zaidi ya yote uwajibikaji
wa walimu.
Siyo wananchi pekee wanaosisitiza uwajibikaji wa walimu. Kwa mujibu wa Davidson, ukosefu wa motisha kwa walimu ni moja ya sababu kuu inayoathiri ubora wa elimu nchini Tanzania 16 .
Utafiti usio rasmi uliofanywa na Twaweza kwa walimu 272 unaonesha kuwa asilimia 96 ya walimu hao hawaridhishwi na kazi zao.
Pia, mwalimu 1 kati ya walimu watatu alisema asingechagua tena kazi ya ualimu, huku wakitaja mazingira magumu ya kazi (asilimia 34) na mishahara midogo (asilimia 26) kama sababu kuu. Hii inadhihirisha kuwa walimu na wananchi kwa ujumla wana mitazamo inayofanana.
Kwa kuwa uongozi mpya umeweka mkazo suala la elimu, ni vizuri pia ukaanza kutatua matatizo ya walimu na kuboresha mazingira ya ufundishaji Tanzania ili kwenda sambamba na kasi ya utoaji wa elimu.
Wakati utekelezaji wa sera mpya ya Elimu ukiendelea, ni vyema kufuatilia mabadiliko yaliyofanyika na mafanikio yaliyopatikana.
Kumekuwa na kusitasita kuhusu dhana hii ya ‘elimu bure’ ambapo viongozi wa shule wana mashaka na jinsi ambavyo TZS 10,000 kwa kila mwanafunzi mmoja kwa mwaka inaweza kutosha. Mfano mmoja ni kuhusu suala la ulinzi.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, asilimia kubwa ya michango ya wazazi kwa mwaka 2015 imekuwa ikitumika kwenye ulinzi (asilimia 66); wakati ruzuku inayotumwa shuleni haihusishi suala la ulinzi.
Iwapo fedha zote zilizotengwa zitapelekwa shuleni na kuwafikia wahusika kwa kiwango kilichopangwa, je kiwango hicho kitatosha kuhakikisha watoto wanajifunza?
Suala jingine la msingi ni kuhusu utunzwaji wa rasilimali. Ruzuku hapo awali zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja shuleni mpaka mwaka kufikia mwaka 2002 zilipoanza kupelekwa kupitia kwa mamlaka zaHalmashauri za Wilaya na Miji.
Kwa sasa mfumo umebadilika ambapo ruzuku zinapelekwa moja kwa moja shuleni. Tunaamini uamuzi wa kupeleka ruzuku moja kwa moja mashuleniumechangiwa na na kutokuwepo kwa ufanisi katika mfumo uliopita.
Kwa mfano, kati ya 2010 na 2013, kwa wastani ni TZS 2,202 pekee ndizo zilizofika shuleni kwa kila mwanafunzi.
Sera mpya ya kupeleka pesa za ruzuku moja kwa moja mashuleni unaibua maswali kadhaa. Tutahakikisha vipi upelekaji wa pesa moja kwa moja kwenye shule utatupa matokeo tofauti?
Je shule zina uwezo wa kusimamia rasilimali hizo vizuri; kuzuia ubadhirifu na upotevu na kuhakikisha zinaelekezwa kwenye matumizi ya vitu muhimu zaidi? Kuna mfumo gani uliopo kwenye ngazi ya shule, hususani katika kuhakiki maamuzi ya matumizi?
Ili kuhakikisha tunapata thamani halisi ya matumizi katika elimu, utoaji na matumizi ya fedha vinapaswa kuhakikiwa katika ngazi ya shule.
Kwa kumalizia, na la muhimu zaidi, utawala mpya umeonekana kuwa kimya kwenye suala la kuboresha matokeo ya ujifunzaji. Ongezeko la shule za msingi kwa mamilioni ya watoto wa kitanzania ni mafanikio makubwa.
Hata hivyo, baada ya miaka kumi ya sera hii, tunatilia shaka anguko la uandikishaji huo wa maelfu ya watoto pasipo kutoa fedha za kutosha, wala kutilia mkazo suala la ubora. Je kutakuwa na walimu wa kutosha kwa wanafunzi hawa? Tutahakiki vipi kama wanajifunza?
Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita tumeshuhudia ongezeko kubwa la shule za sekondari pamoja na wanafunzi huku ikiambatana na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi wanaofanya vibaya kwenye mitihani yao ya kidato cha nne.
Je uongozi huu umejipanga kufanya nini cha tofauti kuhakikisha kuwa Tanzania haiendelei kutengeneza wahitimu mbumbumbu?
Tutahakikisha vipi mfumo wa elimu unawapa watanzania fursa ya kuishi maisha mazuri na kuchochea maendeleo ya nchi? Pamoja na nia njema na maelezo mazuri ya Rais yanayotilia mkazo kwenye elimu na kutoa matumaini mapya, ni muhimu kuzingatia kuwa ufanisi katika sekta hii muhimu utafikiwa kwa kutumia ushirikiano na wadau wote.
Aidha, panahitaji marekebisho mapana zaidi katika mfumo wa elimu ili kufikia malengo ya elimu bure na bora, na sio bora elimu bure!