“Usione vyaelea vimeundwa”, huo ni msemo wa wahenga ukimaanisha kila mafanikio yana maandalizi.
Msemo huo unaendana na kilichotokea katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne yaliyotangazwa wiki iliyopita, ambapo katika shule 10 zilizofanya vizuri hakuna hata moja yenye maandalizi hafifu. Shule nyingi kati ya hizo ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi tisa kwa mwaka.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa shule hizo zote ni zenye majengo mazuri, walimu wazuri na wenye motisha, maabara zilizokamilika sehemu nzuri za kulala na zinazotoza ada zaidi ya Sh2.5 milioni, mbali ya gharama nyingine za chakula, malazi na vitabu.
Shule 10 zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilizoshika nafasi za kwanza ni Kaizirege ya mkoani Kagera, Alliance Girls ya Mwanza, St. Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys ya Mwanza, Canossa (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Alliance Rock Army (Mwanza), Feza Girls na Feza Boys (Dar es Salaam) pamoja na Uru Seminary (Kilimanjaro) ambayo ada yake imetajwa kati Sh1.5 milioni au Sh1.6 milioni kwa mwaka .
Uchunguzi huo umebaini shule tano kati ya 10, zilizoongoza ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi tisa kwa mwaka.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kaizirege iliyoshika nafasi ya kwanza, kila mmoja analipa Sh2.5 milioni za ada. Malipo yote hayo kwa shule zote 10 ni tofauti na gharama za malazi, chakula na vitabu ambavyo malipo yake yanajitegemea.
Kwa makadirio ya ada pekee, mwanafunzi atakayesoma shule hii kwa miaka minne endapo ada hiyo haitaongezeka, atapata elimu hiyo bora katika mazingira mazuri ya kufundishia, lakini lazima awe na Sh10 milioni.
Meneja wa shule hiyo, Eulogius Katiti alisema wanafunzi wanasoma katika mazingira bora, sehemu nzuri ya kulala, chakula bora, vifaa vyote vya kufundishia na hakuna somo linalosomwa kwa nadharia, yote husomwa kwa vitendo kama inahitajika kufanya hivyo.
“Angalia kwenye mtandao, utaona ubora wa mazingira ya shule, mabweni, jumlisha na matokeo ya mwisho ndiyo utaona ni kwa jinsi gani fedha yao inafanya kazi na kuwapa kilicho bora,” alisema Katiti.
Shule ya wasichana ya St. Francis iliyopo mkoani Mbeya, iliyoshika namba tatu, ili mwanafunzi ajiunge na shule hiyo, anatakiwa alipe ada ya Sh2.2 milioni kwa mwaka, huku akitakiwa kulipa katika mikupuo minne.
Mwanafunzi anayesoma katika shule hiyo, anatakiwa kulipa kiasi cha Sh8.8 milioni kwa miaka minne (endapo ada itabaki palepale) mbali ya kulipia bweni, vitabu, chakula na malazi.
Katika Shule ya Sekondari ya wasichana Canossa ya Dar es Salaam, mzazi anahitaji kuwa na Sh3 milioni, ili mwanaye asome mwaka mmoja shuleni hapo, zikiwamo gharama za malazi, chakula, vifaa vya kusomea na ada.
Kwa maana hiyo kwa miaka minne anatakiwa kuwa na kiasi cha Sh12 milioni ili aweze kusoma shule ya Canossa.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Feza Boys ada ni Sh2.9 milioni, lakini ikijumlishwa na gharama za chakula, malazi na vifaa vya masomo, jumla inafika Sh8 milioni na ushehe, ikiwa ni chini kidogo ya Sekondari ya Feza Girls ambazo gharama yake inafikia Sh9 milioni kwa mwaka.
Mkuu wa taaluma wa shule hiyo, Zakia Irembe alitetea gharama hizo, akisema zinaendana na kiwango cha elimu anachopata mwanafunzi na utulivu anaokuwa nao awapo shuleni hapo.
Alisema hakuna kitu kigumu katika masomo kama kusoma huku mwanafunzi anawaza atakula nini, hana uhakika wa kulala, lakini kwao chakula bora, malazi ya kuvutia, uhakika wa kufanya vizuri kutokana na weledi wa walimu katika kufundisha ndiyo siri pekee ya mafanikio yao.
Irembe alisema katika mlo wa wanafunzi kila wakati lazima kuwe na matunda, huku wanafunzi hao wakiwa hawali ugali na kufua nguo ni uamuzi wa mwanafunzi ama atumie mikono au mashine, uhakika wa umeme, kamera za CCTV kwa ajili ya usalama na kila bweni lina eneo la kupumzikia kutizama taarifa ya habari.
“Mzazi analipa fedha anabaki anatudai elimu, jukumu la kusimamia chakula, malazi ni letu, ndiyo maana vitu vyote kwetu ni bora ili kupata elimu bora pia. Elimu inahitaji uwekezaji mkubwa, kusoma siyo kila mtu anaweza, kunahitajika vitu vya ziada kuhakikisha akili ya msomaji inawaza masomo pekee,” alisema Irembe.
Mwanafunzi aliyeshika namba moja katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, Butogwa Shija aliyekuwa akisoma katika Shule ya Wasichana Canossa, alisema kuwa licha ya kupenda kusoma, mazingira mazuri ya kusomea, uhakika wa kupata kila anachotaka katika kujifunza ndiyo chachu ya mafanikio yake.
Mzazi wa mwanafunzi Innocent Lawrence aliyeshika nafasi ya tatu katika mtihani huo kutoka Feza Boys, Lawrence Nyakabunda alisema kuwa ada anayolipa katika shule hiyo inalingana na elimu anayopata mwanaye.
Alisema anakubaliana na ada kuwa kubwa, lakini anaridhishwa na kiwango cha elimu kijana wake anachopata.
Wakati wenye shule na wazazi wakisema hayo, Msomi wa masuala ya elimu, Profesa Kitila Mkumbo alisema sababu kubwa ya shule hizo kufanya vizuri ni aina ya wanafunzi wanaochukua, wanakuwa wamechujwa hadi wanapofika katika mtihani wa mwisho wote wanakuwa bora.
Alisema shule hizo pia zina walimu wa kutosha, wenye weledi wa ufundishaji, huku wakipewa motisha ya kufanya kazi hiyo.
Wataweka maelezo mengi lakini uchunguzi zaidi ukifanyika na independent investigator utabaini hizi gharama wanazolipisha wazazi ni kubwa mno!
ReplyDeleteKama ni hivyo basi serikali iangalie uwezekano wa wanafunzi wanaotoka kwenye hizi shule wajilipie wenyewe chuo kikuu! Na pia iweje mzazi aweze kulipa milioni 3 hadi 9 kwa mtoto wa sekondari lakini ikifika chuo kikuu waanze kuilalamikia serikali?
Pili hapa mbele hizo shule zitakosa pesa kwa sababu tunajua kwamba wengi wa wanaolipa hizo pesa hawakuwa na kipato halali cha kuwawezesha kulipa kiwango hicho. `Sasa hivi na hiki kibano cha Magu lazima pesa zipotee.