Vigogo watatu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), akiwemo Mtendaji Mkuu wa mradi huo, Asteria Mlambo, wamepandishwa kizimbani, kwa tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5.
Mbali na Asteria, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ya uhujumu uchumi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale, Mwanasheria Mkuu wa mradi huo, Francis Kugesha na Mkurugenzi wa kampuni ya Yukan, Yuda Mwakatobe.
Walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashitaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Walisomewa mashitaka na wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jackline Nyantori akisaidiwa na Estazia Wilson na Stellah Mafuru.
Nyantori alidai kati ya Septemba Mosi na Oktoba Mosi 2013, Kinondoni Dar es Salaam, Asteria, Katale na Kugesha wakiwa wafanyakazi wa mradi huo, walishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5.
Katika mashitaka yanayomkabili Mwakatobe, inadaiwa Juni 29, 2005 katika ofisi za kodi Ilala, Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), wakati akiwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka 2004 na ya 2005 ya kampuni yake ya Yukan Business, jambo lililosababisha alipe kodi ndogo.
Awali, Wakili Nyantole alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha hati ya kuruhusu mahakama hiyo, kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi hivyo washitakiwa wataruhusiwa kujibu mashitaka yao.
Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Takukuru ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia hawana pingamizi ya dhamana kwa washitakiwa.
Hakimu Mwijage alisema Asteria, Katale na Kugesha watapata dhamana endapo kila mmoja atakuwa na mdhamini mmoja anayefanyakazi serikalini au kwenye taasisi inayofahamika, atakayesaini hati ya Sh milioni 15. Pia kila mshitakiwa awasilishe Sh milioni 15 au hati isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 15.
Kwa upande wa Mwakatobe, dhamana yake ipo wazi endapo atapata mdhamini mmoja mwenye barua kutoka taasisi inayofahamika, asaini hati ya Sh milioni tano.
Wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti. Asteria na Katale wametakiwa kuwasilisha hati hizo Machi 3 mwaka huu. Kesi itatajwa tena Machi 9 mwaka huu.