Wabunge Wa CCM Waungana Na Upinzani Kuibana Serikali Kuhusu Ujenzi Wa Reli, Kuhamiashia Hela BoT Na Shirika la Ndege ATCL

Bungeni
Bila kujali itikadi za vyama vyao, wabunge wameukosoa mwongozo wa kuandaa mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17, wakihoji suala la ujenzi wa reli ya kati kwa viwango vya kimataifa pamoja na mambo mbalimbali.

Pia, wamepinga mpango wa Serikali wa kutaka mapato yote ya halmashauri, taasisi na mashirika ya umma kuwekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na kuitaka itafute vyanzo vipya vya mapato.

Katika kuonyesha msimamo wa pamoja, wabunge wote wanaotokea mikoa ambayo Reli ya Kati inapita wameunda umoja kuhakikisha Serikali katika mpango wake wa bajeti ya 2016/17, inakuja na mwelekeo wa ujenzi wa reli ili nchi ipate maendeleo ya kweli, si ya kwenye makabrasha.

Umoja huo uko chini ya uenyekiti wa Ezekiel Maige, mbunge wa Msalala (CCM), wakati Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), anakuwa katibu wa wabunge hao walio katika mikoa inayoanzia Dar es Salaam kupitia Tabora hadi Mwanza na kutokea Tabora hadi Kigoma.

Mikoa mingine inayounganishwa na reli hiyo kongwe ni Shinyanga, Morogoro na Dodoma.

Akichangia mjadala kuhusu mwongozo huo, Zitto alitahadharisha dhidi ya siasa za kikanda.

“Tunapaswa kuwa makini sana kwenye siasa za kikanda. Tusikubali maslahi ya nchi nyingine yafunike maslahi ya nchi yetu. Ni lazima tuhakikishe mtandao wa reli ambao utaisaidia nchi yetu,” alisema kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo.

“Juzi nilisikia kwamba tuna tatizo la fedha. Mwaka jana Bunge lilipitisha sheria ya Kodi ya Maendeleo ya Reli ambayo inataka kila mzigo unaoingia nchini, utozwe asilimia 1.5 kwa ajili ya reli. Tunacho chanzo cha uhakika cha fedha na tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba chanzo hiki kinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

“Tupewe tafsiri ya Reli ya Kati. Kwetu sisi Reli ya Kati ni ile inayotoka Dar es Salaam, Tabora, Uvinza (kwenda msongati Burundi). Kutoka Kaliua kwenda Mpanda mpaka Kalema kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Kalema. Kutoka Isaka kwenda Keza Ngara kwa ajili ya madini ya Nikel yaliyogundulika huko ili kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.”

Mvutano kuhusu reli ulianza tangu wiki iliyopita katika mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli wakati mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliposema atawashawishi wenzake kuigomea bajeti ya 2016/17, iwapo Serikali haitatoa mwelekeo wa ujenzi wa reli hiyo ya kati.

Kuhusu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Zitto alisema badala ya Serikali kukimbilia kununua ndege mbili, inapaswa kulifanyia shirika hilo marekebisho kwa kuzifanya taasisi za utalii kuwa na hisa ATCL.

“Kutokana na wingi wa watalii wanaoingia nchini, Tanapa na Ngorongoro wanapata mapato. Turuhusu wawe na hisa ATCL ili shirika hili lijiendeshe kibiashara,” alisema Zitto.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliungana na Zitto kumtaka Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango aeleze Reli ya Kati itajengwa kuanzia wapi kwenda wapi wakati atakapokuwa akiwasilisha mpango huo.

Alisema bila kuwa na reli ya uhakika ni ndoto nchi kupata maendeleo inayoyatarajia.

Serukamba alisema kuna taasisi zilizoanzishwa kwa sheria hivyo kuzitaka zianze kupeleka fedha katika mfuko mkuu wa Serikali, italazimika sheria kubadilishwa.

Mbunge huyo alihusisha suala hilo na uvivu wa watendaji wa hazina kutopenda kufikiria vyanzo vipya vya mapato.

“Mtazifanya halmashauri zishindwe kujiendesha jamani mbona hamfikirii suala hili. Waziri hii kitu si sawa kabisa iondoeni,” alisema.

“Viwango vya kodi mnavyoviweka ni vikubwa sana. Hivi (Mamlaka ya Mapato) TRA haijifunzi kwa nchi kama Mauritius ambayo viwango vyake vya kodi ni vidogo lakini inakusanya fedha nyingi?” alihoji.

Naye mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile alisisitiza umuhimu wa kuwa na reli.

“Tukitaka kupaisha uchumi, lazima tuwe na Reli ya Kati ya kiwango cha kisasa. Ni lazima serikali mje na mpango wa kueleweka,” alisema akizungumzia reli hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 1905 wakati nchi ikiwa chini ya wakoloni wa Kijerumani.

Mbunge wa viti maalum (CCM), Mwanne Nchemba alisema suala la reli ya kati si la mzaha kwa maelezo kuwa wapigakura wengi wanaitegemea reli hiyo, pia ni njia nzuri ya kusafirisha mizigo, hivyo lazima Serikali ihakikishe inaijenga kwa kiwango cha kisasa.

Kwa upande wake mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwako alisema sera ya uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kufanikiwa vyema bila nchi kuwa na reli ya uhakika.

“Mizigo lazima ipite katika reli ili kuokoa barabara zetu. Msipokuja na mkakati hatutawaelewa katika bunge hili. Haiwezekani miaka 20 sasa tunazungumzie reli tu,” alisema huku akisisitiza kuwa uwepo wa reli utaongeza kasi ya mapato bandarini.

Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul naye aliungana na Serukamba kuhoji uamuzi huo wa Serikali kuweka fedha zote za mapato kwenye mfuko wa Serikali, akisema utaua halmashauri.

“Tukumbuke historia ya ugatuaji wa madaraka, kumbukeni jinsi Mwalimu (Julius)Nyerere alivyourudisha baada ya kuona faida zake. Serikali za mitaa zina mamlaka ya kukusanya mapato na kutumia, sasa hayo mamlaka mnayaondoa mnategemea nini,” alisema.

“Mkipitisha suala hili, haya mapato hayatakusanywa ipasavyo na pia mtatengeneza mianya mingine ya ajabu ajabu.Tumekuwa tukiona jinsi ambavyo Serikali inashindwa kutoa fedha za maendeleo, sasa mnapotaka fedha zote zipelekwe katika mfuko mkuu wa Serikali, je zitatoka zote wakati zitakapohitajika?” alihoji.

Gekul alisema kama tatizo ni sheria za halmashauri na taasisi, ni vyema zinakabadilishwa ila si kuziondolea mapato.

Mbunge wa Nsimbo (CCM), Richard Mbogo alizungumzia Shirika la Ndege (ATCL) akitaka lipunguze wafanyakazi wake ili kuweza kujiendesha kibiashara.

Alisema kwa sasa shirika hilo linasuasua kutokana na kutokuwa na mapato ya kutosha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad