WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye ametengua uteuzi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania Henry Lihaya baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wake.
Mhe. Nnauye ametengua uteuzi huo katika ziara yake aliyoifanya leo mapema katika ofisi za BMT kuona miundo mbinu ya ofisi hizo na kujua changamoto walizonazo.
“Baraza likirekebishwa vyama vya michezo navyo vitakuwa mguu sawa na kuleta chachu na maendeleo katika michezo,”alisema Mhe. Nnauye.
Aliongeza kwa kusema kuwa, miaka saba ambayo Lihaya amekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza imetosha kwani hakuna mabadiliko yoyote aliyoyafanya katika sekta ya michezo tangu alipoteuliwa mwaka 2009.
Kutokana na utenguzi huo Mhe. Nnauye amemtaka Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi kupendekeza jina la Katibu Mtendaji mpya wa BMT ambaye anampendekeza kwa mujibu wa sheria ya BMT kifungu cha 5(1) baada ya kupata idhini ya waziri mwenye dhamana.
Vilevile, Mhe. Nnauye amemtaka mwenyekiti kuteua Katibu Mtendaji ambaye atakuwa ni mchapa kazi na mwenye mipango ambayo itaibadilisha BMT na kuleta chachu katika michezo nchini.
Aidha, Mhe. Nnauye amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara ya habari, utamaduni sanaa na michezo kumpangia Lihaya kazi nyingine wizarani.
Waziri Nape Nnauye Atengua Uteuzi Wa Katibu Mtendaji Baraza La Michezo Tanzania ( BMT )
0
February 19, 2016
Tags