Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepinga mpango wa madiwani wa Halmashauri ya Meru inayoongozwa na Chadema kukopeshwa magari.
Akizungumza katika ziara ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Lekule Laizer wilayani humo, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Langaeli Akyoo alisema wameshangazwa madiwani kukopeshwa Sh9 milioni kila mmoja, huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kero mbalimbali.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bakari Sajini alipinga tuhuma hizo na kueleza kuwa hakuna kikao cha madiwani kilichopitisha uamuzi huo, lakini kinachofanyika ni madiwani kupitia posho ya Sh350,000 wanayolipwa kila mwezi kuitumia kukopa benki.
“Kama katibu wa baraza la madiwani sina hizo taarifa, ninachojua kuna madiwani wametumia posho zao kukopa benki za CRDB na NMB kulingana na mahitaji yao na jambo hili lipo nje ya halmashauri,” alisema mkurugenzi huyo.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alipinga madai ya CCM akieleza kuwa hataki siasa za malumbano na chama hicho katika jimbo hilo, huku akisisitiza aachwe afanye kazi za kutatua kero za wananchi.
Awali, akielezea kero zinazowakabili wananchi, katibu wa CCM wa wilaya hiyo alisema mojawapo ni kuwapo kwa barabara mbovu.
Alisema kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, halmashauri hiyo ilinunua tingatinga kwa ajili ya ukarabati wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibika kila wakati.
Katibu huyo alisema baada ya uchaguzi huo Chadema ilishinda ubunge na pia kuongoza halmashauri, lakini ilibadili matumizi ya tingatinga na kuanza kulikodisha kwa watu binafsi.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema wakati anahamia alikuta nyaraka ambazo ziliachwa na madiwani waliopita zinazotaka tingatinga hilo kujiendesha.